loader
Picha

Serikali yaingilia kati mgogoro RT

SERIKALI imeingilia kati mgogoro unaofukuta chini kwa chini ndani ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na kuamua kukutana nao haraka iwezekanavyo ili kujua kinachoendelea.

Hivi karibuni nahodha wa timu ya taifa ya riadha iliyoshiriki mashindano ya dunia ya riadha Doha, Qatar, Felix Simbu, alisema hawakufanya vizuri kutokana na viongozi wa juu RT kuendekeza malumbano badala ya kuandaa timu.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Dk Yussuf Singo, alisema jana kwa njia ya simu kutoka Dodoma kuwa, wameliona hilo na ameliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuandaa haraka kikao na kamati nzima ya RT ili kujua nini tatizo.

“Ni kweli tumeliona hilo na tayari nimeliagiza Baraza la Michezo kuandaa haraka kikao na kamati nzima ya RT ili tulizunguze hilo,”alisema baada ya kuulizwa kuhusu kuwapo mgogoro ndani ya RT.

Singo alisema endapo kuna matatizo ndani ya RT au la watajua baada ya kufanyika kwa kikao hicho ambacho bado hakijajulikana kitafanyika lini, lakini aliwataka BMT kukiandaa mapema ili wakutane haraka. Simbu alimaliza katika nafasi ya 16 na kushindwa kutetea medali yake ya shaba aliyoipata katika mashindano ya dunia ya riadha yaliyofanyika London 2017, huku wenzake alioshiriki nao marathon, Augustino Sulle, Stephano Huche na Failuna Abdi, walishindwa kumaliza mbio hizo sababu ya joto kali.

Alisema tofauti na wakati wa maandalizi ya mashindano ya mwaka 2017, ambapo viongozi wa RT walikuwa karibu sana na timu, mwaka huu hawakuonesha ushirikiano kabisa na kila mwanariadha alifanya mazoezi kivyake na hakukuwa na kambi ya pamoja.

Singo alipoulizwa kuhusu waraka mzito uliojaa tuhuma mbalimbali za viongozi wa RT uliowasilishwa kwake kama ameupata, alisema hafahamu lolote kuhusu hilo. Baadhi ya tuhuma hizo ni ubadhirifu wa fedha, uwapo wa akaunti `feki’, kutelekezwa kwa kocha wa riadha (Mmarekani Ron Davis), matumizi tofauti ya gawio kutoka Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha (IAAF) (Olympic Dividend).

Gawio hilo hutolewa kwa ajili ya masuala ya mafunzo ya riadha, programu ya watoto, lakini badala yake yake sehemu ya fedha hizo inadaiwa zilitumika kwa ajili ya kulipia madeni waliyokuwa wakidai wanariadha walioshinda mbio za Hapa Kazi Marathon Dodoma.

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi