loader
Picha

Ukiona dalili hizi, msaidie mtu asijiue

KATIKA miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko la watu kukatisha uhai wao kwa kujiua. Haya hayatokei Tanzania pekee bali dunia kote. Hali kama hiyo inaelezwa kuwa inatokana na watu hao kukumbwa na msongo mkali wa mawazo, yaani sonona.

Hali hiyo inaelezwa kusababishwa na vitu mbalimbali ikiwemo ugonjwa, kukosa kazi, kufanya kazi ambayo haiwapi amani, matatizo kwenye mahusiano na mengineyo. Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Praxeda Swai, anasema ripoti zilizopo zinaonesha kwamba kila mwaka takribani watu 800,000 hupoteza maisha kwa kujiua kutokana na sonona.

Kwa takwimu hizo ni sawa na kusema kwamba kila baada ya sekunde 40 mtu mmoja hujiua duniani ambayo pia ni sawa na kusema kwamba katika kila saa moja, watu 90 hujitoa uhai duniako kote. Dk Swai anasema ukubwa wa tatizo la watu kujiua lipo zaidi kwa kundi la vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 29 na wazee kuanzia miaka 75 na kuendelea.

Anasema mtu anayetaka kujiua huwa amedhamiria kufanya hivyo wala sio bahati mbaya lakini kunakuwa na kitu kimemfanya akaamua kufanya hivyo. Anasema kabla mtu hajaamua kujiua, huwa kuna viashiria ambavyo jamii inayomzunguka inapaswa kuvijua na kuvitilia maanani. Viashiria hivyo ni pamoja na hali ya huzuni nyingi au mihemko na hasira zisizotarajiwa kuongezeka kwa mhusika mwenye changamoto ya afya ya akili.

Kiashiria kingine kinachotajwa ni mhusika kuonesha kukosa matumaini juu ya nini kitafuatia wakati ujao na kuamini kwamba hali alio nayo kwa wakati huo kamwe haiwezi kuboreka. Pia mhusika huweza kuwa mkimya ghafla au kuonesha wasiwasi mkubwa.

Hali hiyo ikionekana basi mtu huyo ameshafikia uamuzi mbaya. Kujitenga na kujiepusha na ndugu, marafiki au kwenye matukio ya kijamii pia ni dalili za kuangalia kw amtu mwenye sonona. Hii ni pamoja na kupoteza hamu ya kufanya shughuli ambazo amezoea kuzifanya.

Mabadiliko katika tabia na utendaji uliozoeleka kama vile kuzungumza kwa sauti ya chini au ya juu sana na kutozingatia mambo ni dalilia pia. Dalili nyingine ni mhusika kuwa na tabia hatarishi kama vile kuendesha gari bila kujali/kuzingatia uslama wa barabara, kujihusisha na ngono zisizo salama, kuongeza matumizi ya vilevi na kuonesha waziwazi kwamba mhusika hathamini tena uhai wake.

Kufanya matayarisho kama vile kuweka biashara yake katika utaratibu inaweza kuwa dalili nyingine ya kuangalia. Hii inaweza kujumuisha kutembelea marafiki na wanafamilia, kutoa mali zake, kusafisha chumba chake au nyumba yake. Wengine huandika maelezo kwa nini wanaona kujiua ndio suluhisho. Matayarisho mengine yaweza kuwa ni pamoja na kununua vitu vya kujiulia kama silaha, sumu, kamba ya kujinyongea na kadhalika.

Lakini kubwa ambalo watu wanapaswa kuzingatia ni mhusika kutoa kauli au vitisho vya kujiua. Inaelezwa kwamba asilimia 50 hadi 75 ya wale wanaofikiria kujiua hutoa vistisho vya namna hiyo kwa ndugu, rafiki au jamaa wa karibu. Hata hivyo, la kuzingatia ni kwamba sio kila mtu anayefikiria kujiua atatoa onyo au vitisho na sio kila mtu anayetishia kujiua atatekeleza hilo.

Lakini kila tishio la kujiua linapaswa kuzingatiwa kwa uzito mkubwa. Dk Sawai anasema kwa upande wa watoto ripoti zilizopo zinaonesha kwamba wengi wao walishapitia changamoto nyingi zikiwemo kunyanyasika kingono, kimwili au kihisia. Watoto wengine walifanyiwa vitu ambavyo havikustahili ikiwa ni pamoja na kuachwa na wazazi. Anasema kuna watu wengine wazima wanaishi na magonjwa sugu yanayotibika.

Watu hao anasema huendelea na maisha yao ya kila siku lakini kuna ambao baada ya kubaki na mateso kwa muda mrefu, hufanya maamuzi ya kujitoa uhai wakiamini ni namna nzuri ya kupumzika.

Dk Swai anasema mtu akiona dalili za mtu kutaka kujiua, ni vyema kumsaidia kwa kumwongezea upendo, kutomdhihaki na kumpa moyo huku akimshawishi kwamba ukomo wa madhila yanayomkabili hauko mbali. Kwa upande mwingine, Dk Swai anaishauri serikali kudhibiti vitu vinavyoweza kuondoa uhai wa mtu mwenye sonona kama vile wanaouza dawa za binadamu pamoja na upatikanaji wa silaha kiholela.

Naye Mwanasaikolojia ya tiba ya akili ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili Tanzania (MEHATA), Dk Isaac Lema, anasema suala la afya ya akili ni muhimu kwani ubora wa afya ya mwili unapaswa kuanza na afya ya akili. Anasema afya ya akili inamwezesha mtu kufikiria kufanya uamuzi wa kuwasiliana na watu mbalimbali na kufurahia maisha. Siku ya Afya ya Akili mwaka jana iliadhimishwa kwa kwa ngazi ya vijana kuzungumzia tatizo la afya ya akili na mwaka huu kaulimbiu ya maadhimisho ya siku hii ni ‘Kuhamasisha Afya ya Akili na Kuzuia Hali Inayosababisha watu Kujiua’.

AFYA YA AKILI KAZINI

Dk Lema anasema takwimu zinaonyesha kuwa katika watu wanne, kuna mmoja anakabiliwa na changamoto ya afya ya akili na kwamba katika maeneo ya kazi mtu moja kati ya watano anakabiliwa na tatizo hilo.

“Katika mazingira ya kazi wakati mwingi matatizo yanakuwa yakiongezeka. Ukiona watu mara kwa mara wanakuwepo kazini lakini hawawezi kufanya kazi zao za kila siku ni kiashiria pia cha wahusika kuwa na sonona.

“Ama mwingine anakuwepo lakini hafanyi kazi yake ya kila siku ama haishi kuomba ruhusa ya kwenda nyumbani kutokana na mambo mengi yanayomkabili. “Mwingine anakuwa na mabadiliko ya kimwenendo na kihisia maeneo ya kazi, kwa dalili kama hizo ni muhimu watu kuzingatia afya ya akili,” anasema.

Dk Lema anasema sababu kubwa ya kuzingatia afya ya akili kazini ni kwamba mtu anakaa muda mwingi katika eneo hilo la kazi na kukutana na watu wengi hivyo ni vema mazingira ya kazini yakawa salama kwa kila mmoja. Anasema mtu akishindwa kukabili msongo wa mawazo humletea uchovu wa kiakili na kusababisha kuacha kazi au kubadili kazi.

“Mwisho wa siku mtu huyo kwa kuwa hafurahii mazingira yaliyopo kazini kwake husema anafanya kazi hiyo kwa ajili ya familia yake lakini haifurahi,” anasema.

Anasema kuna watu wameacha kazi siyo kwa kukusudia bali ni kutokana na sonona na hii ni kwa kuwa muda mwingi huutumia wakiwa kazini kuliko nyumbani.

“Hivyo mazingira ya kazi yanapaswa kuboreshwa ili kupunguza athari zinazoweza kumpata mtu na la kuangalia sana ni kuona mtu yupo kazini lakini hawezi kufanya kazi kwa ufanisi. Hapo ujue kuna shida,” anasema.

Anasema tukifanya maeneo ya kazi yakawa ni ya kutunza afya ya akili, wengi watafurahia kazi na hivyo kuzalisha kwa tija.

TANGU maambukizi ya virusi vya corona yabishe hodi nchini Machi ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi