loader
Picha

Umuhimu wa jamii kujua matatizo ya afya ya akili

OKTOBA 10 kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Afya ya Akili. Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka huu, ‘kila sekunde 40, mtu mmoja hupoteza maisha kwa kujiua’.

Watu takribani 800,000 hufa kwa kujiua kila mwaka kwa mujibu wa WHO na kwamba, tatizo hili halijazungumzwa vya kutosha miongoni mwa jamii. Vitendo hivi huathiri watoto, wazazi, wenza na marafiki. Hata hivyo, matukio haya hutokea zaidi kunapokuwa na mizozo, au nyakati ambazo watu wanakuwa na msongo wa mawazo, matatizo ya kifedha, kuvunjika kwa uhusiano, maradhi sugu na maumivu yasiyokwisha.

Idadi kubwa ya watu wanaojiua ni wale walio mijini, na makundi ya watu wanaokabiliwa na unyanyapaa kama vile wakimbizi na wahamiaji, watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja na wafungwa.

Kwa mujibu wa WHO, sababu nyingine ni mizozo, majanga, machafuko, unyanyasaji, kupoteza wapendwa na kutengwa. WHO inasema kuwa, mzigo wa matatizo ya afya ya akili miongoni mwa vijana barubaru unasababisha mambo makubwa matatu: msongo wa mawazo, kujiua ikiwa ni sababu inayoshika nafasi ya pili kwa vifo vya vijana kati ya umri wa mika 15-19 na tatizo linaloongoza ni matumizi mabaya ya pombe na mihadarati.

Tatizo la matumizi mabaya ya pombe na mihadarati hufanya matatizo ya akili kuwa moja ya changamoto kubwa kwa nchi nyingi duniani na huchangia kuwaweka vijana kwenye hatari kama ya kufanya ngono isiyo salama, na hata uendeshaji mbovu wa magari unaosababisha vifo vya vijana wengi. Athari za kutoshughulikia matatizo ya afya ya akili kwa vijana ni kubwa kwa mujibu wa WHO na mara nyingi zinaendelea hadi ukubwani na kuwakosesha fursa ya kushamiri katika maisha yao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hii anasisitiza kwamba, ni muhimu serikali zikawekeza na kuhusisha sekta za afya, elimu na jamii katika kudhibiti janga hili ili kuhakikisha ajenda ya 2030 ya maendeleo haimuachi yeyote nyuma, wakiwemo vijana wenye matatizo ya akili ambao hunyanyapaliwa na kukosa msaada wakati mwingine.

Matatizo ya afya ya akili ni nini? Inaelezwa kuwa tatizo la afya ya akili linahusiana na namna mtu anavyojihisi na akili yake inavyofanya kazi. Mtu hushindwa kuzuia namna anavyojisikia moyoni, na kushindwa kuzuia tabia zake. Mara nyingi, hali hiyo inazuia uwezo wa mtu wa kushugulika na wengine au kushugulikia mambo yake ya kimaisha. Kwa watu wengine, dalili zinaweza kuwa nyingi na zinaweza kuonekana kwa muda mrefu, ikitegemea mtu husika, tatizo, na hali.

Matatizo ya afya ya akili yanaweza kuwapata watu wa jinsia zote, wa rika zote, desturi zote, rangi zote, dini zote, walio na elimu na wasio na elimu, matajiri na maskini. Matatizo ya afya ya akili hayatokani na udhaifu wa mtu au tatizo katika hali ya mtu. Kupitia kuwajali na matunzo mazuri, watu wanaweza kupona na kuishi maisha yenye furaha.

Kwa nini afya ya akili ni muhimu? Afya ya akili ni muhimu kwa sababu inaweza kuathiri afya ya kimwili na ustawi wote wa mtu. Wakati mtu ana shida ya afya ya akili, inamaanisha ustawi wake wa akili hauko sawa kama vile mwili wake unapoumia.

Kuna sababu nyingi ambazo watu hupata masuala ya afya ya akili. Wanaume wengine huzaliwa katika hatari kubwa zaidi na wengine wana hatari baada ya kukabiliana na mambo kama msongo wa mawazo au shida. Wakati mwingine, matatizo ya afya ya akili yanaweza kuwa madogo na kuisha kwa urahisi. Nyakati nyingine, yanaweza kuwa mabaya na kufanya iwe vigumu kwa watu kufanya kazi kama kawaida.

Wanaume wanaojamiiana na wanaume wengine wanaweza kupata matatizo ya afya ya akili kama huzuni na wasiwasi, siyo kwa sababu ya wale wanaojamiiana nao, bali kwa sababu wanaweza kupata unyanyasaji, unyanyapaa, na ubaguzi. Kuwa na uwezo wa kutambua tatizo la afya ya akili ni muhimu kwa sababu wakati mwingine, kunaweza hata kukuongezea uelewa wa namna ya kuepuka hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU). Uelewa huo unaweza pia kusaidia kuepusha matumizi au ongezeko la matumizi ya vilevi na hata kusaidia kuepusha matumizi ya ngono isiyo salama.

Kulingana na WHO, watu wengi wenye tatizo la afya ya akili wanajizuia kutafuta huduma kwa sababu ya aibu inayoletwa na tatizo hilo. Nusu ya magonjwa yote ya akili duniani yanaanza katika umri wa miaka 14 na mengi hayabainiki wala kutibiwa, suala linaloweka mustakabali wa vijana wengi njia panda, limesema WHO. Daktari bingwa wa magonjwa ya akili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Praxeria Swai anasema, vifo vinavyotokea, katika kundi la vijana kati ya miaka 15 hadi 29, vitokanavyo na kujiua vinachukua nafasi ya pili vikitanguliwa na ajali.

Dk Swai anasema kuwa kuna sababu nyingi zinazofanya kundi la vijana hawa kutaka kujiua. Anasema vijana wengi huwa ndiyo umri wa kubalehe na wanapitia changamoto nyingi. Hawa, mara nyingi huwa wanajaribu vitu vingi katika maisha yao. Familia na vijana mara nyingi huwa wanakuwa hawaelewi, malumbano mengi, hawana taarifa sahihi ya kile kinachoweza kutokea na wanataka kujaribu kila kitu ikiwemo vilevi. Lakini pia, inawezekana hawana taarifa sahihi ya kitu wanachopaswa kufanya wakipitia changamoto ya aina hiyo.

Wengi huwa wana maumivu ya kihisia, ndiyo maana wanafikia katika maamuzi kama hayo. Vijana wa kiume wanatajwa kujiua zaidi ya wa kike. Wanaume wanaweza kujiua mara tatu zaidi ya wanawake ambao huwa wanaishi na mawazo ya kutaka kujiua mara tatu zaidi ya wanaume. Wanaume wachache sana wanajaribu kujiua na kupona, wengi huwa hawaponi. Dk Swai anasema kuwa kuna kiwango kikubwa sana cha vijana wanafika wakiwa na tatizo la sonona na afya ya akili. 0685 666964 au bjhiluka@ yahoo.com

TANGU maambukizi ya virusi vya corona yabishe hodi nchini Machi ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi