loader
Picha

Kusanyiko la kipekee chachu ya mageuzi China

NI bayana kwamba China ina desturi ya kipekee ya kisiasa kote duniani.

Kinyume na hali ilivyo katika maeneo mengine ya dunia ambapo Bunge la umma la China lina kalenda ya shughuli nyingi kwa mwaka mzima.

Wabunge wa Bunge la Umma na wajumbe wa Baraza la Mashauriano ya kisiasa nchini humo hukutana mara moja tu ndani ya miezi 12, na halmashauri ya kudumu katika vyombo hivyo viwili husimamia shughuli zote katika kipindi ambacho mkutano wa mwaka haufanyiki.

Wachina wanataja hali hii ya siasa kama sababu kuu ya maendeleo ya haraka ya kiuchumi yanayoshuhudiwa katika nchi hii.

Kila mwaka, mwezi wa Machi, China inaandaa mkutano wa wajumbe wote wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China (CPPCC) na mkutano wa wabunge wote wa Bunge la Umma la China (NPC), kwa pamoja itambulikanayo kama Mikutano Miwili Mikuu au ‘Lianghui’ kwa Kichina.

Ni tukio kubwa la kisiasa la mwaka nchini China ambalo linawaleta pamoja wabunge na wajumbe takriban 6,000 katika Jumba maarufu la Mikutano ya Umma la Beijing.

Mikutano hii inatoa nafasi kwa taifa kutafakari kuhusu mwelekeo na sera ya nchi. Sura muhimu hasa ya kusanyiko hili ni matokeo yake.

Mikutano hii inatoa fursa muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kuangalia kwa makini mwelekeo ambao nchi hii yenye uchumi mkubwa wa pili duniani unachukua.

Kwa kweli, mikutano hiyo miwili inavutia jamii ya kimataifa kwani inatoa taswira mahususi ya jinsi mambo yalivyo nchini China.

Masuala yanayohusu maslahi ya umma kama vile uchumi, juhudi za kupambana na ufisadi, ulinzi wa mazingira ya asili, jitihada za kupunguza umasikini, usalama wa jamii na hali ya makazi zinajadiliwa kati ya wakuu wa wizara za serikali, maofisa viongozi kutoka nyanja zote za maisha na umma, kabla ya mipango kuangaliwa upya au kutekelezwa.

Ni kweli kwamba mikutano hii kimsingi inajadili masuala muhimu yanayowakabili Wachina, huku mapendekezo kuhusu suluhisho lao yakitolewa. Ni vigumu kwa wengi kuelewa kwamba si rahisi kwa yeyote kufanya uamuzi wa moja kwa moja nchini China.

Kwanza, kunatakiwa mashauriano ya kina, kisha makubaliano ya kimkakati yanaafikiwa. Matokeo yake yanaratibiwa kupitia mikutano ya kila mwaka kama vile Mikutano Mikuu na kwenye mipango ya maendeleo ya miaka mitano.

CPPCC ni chombo cha mashauriano ya kisiasa nchini China, huku NPC ikiwa chombo kikuu cha utungaji wa sheria nchini humo. Vyombo hivi viwili vimeundwa kwa njia tofauti sana ikilinganishwa na taasisi za kisiasa katika mataifa mengine.

Kulingana na Wachina, CPPCC ni chombo muhimu cha kuhakikisha mashirikiano baina ya vyama vingine vya kisiasa na mashauriano ya kisiasa chini ya uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ambayo ndio njia muafaka ya kukuza demokrasia ya kijamaa nchini humo.

Moja ya matukio muhimu wakati wa mikutano hiyo ni utoaji wa ripoti ya kazi za serikali ambayo inatathmini hali ilivyokuwa mwaka uliopita na kutoa mapendekezo ya mipango ya kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo ya taifa kwa mwaka unaofuatia.

CPPCC inajumuisha wajumbe kutoka Chama tawala cha CPC na vyama vingine vya kidemokrasia pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii na kikabila.

Wengi wao ni viongozi mashuhuri wa kisiasa, wasomi na raia maarufu kama vile mwanzilishi wa kampuni ya Tencent Pony Ma, mwigizaji Jackie Chan na nyota wa mpira wa kikapu aliyewahi kuchezea nchini Marekani (NBA) Yao Ming.

Jukumu kuu la CPPCC ni kuangalia jinsi serikali inavyotekeleza wajibu wake na kisha kutoa maoni na mapendekezo kuhusu jinsi serikali inavyoweza kuboresha wajibu huo.

Maoni na mapendekezo haya yatasaidia seriali kutoa maamuzi yanayohusu maisha ya kila siku ya raia wa China.

Wakati wa mikutano hiyo ya wiki mbili, kuna vikao vingi vya mikutano mikuu, kisha kuna majadiliano ya makundi yaliyogawanyika katika maeneo tofauti kulingana na mada. Ni hapa ambapo shughuli kamili hutekelezwa.

Aidha, wajumbe wa CPPCC wanatoka maeneo mbalimbali ya China ikiwa ni pamoja na Taiwan, Hong Kong na Makau na fani mbalimbali, mirengo tofauti ya kisiasa na nyanja mbalimbali ya maisha.

Wote kwa kawaida wana mitazamo tofauti. Siku mbili tu baada ya vikao vya baraza la CPPCC kuanza, wabunge zaidi ya 3,000 wanakusanyika Beijing kuhudhuria vikao vya Bunge la Umma la China (NPC).

Kazi kuu ya NPC ni kuthibitisha ripoti ya kazi za serikali za mwaka uliopita, ripoti za kazi za Mahakama Kuu na Idara Kuu ya Uendeshaji Mashtaka za mwaka uliopita, kujadili na kupitisha bajeti ya serikali na kupiga kura juu ya sera na sheria za kitaifa.

Baadhi ya majukumu makuu ya NPC ni pamoja na uchaguzi wa Rais wa China, na maofisa viongozi.

Majukumu yake mengine ni pamoja na kutunga na kurekebisha sheria za jinai, asasi, taasisi, na sheria nyingine za kimsingi.

Wakati sheria zinapigiwa kura ndani ya NPC, tayari zinakuwa zimejadiliwa mara kadhaa katika mwaka, na maridhiano kuafikiwa na tofauti zilizoko kuondolewa.

Hata ingawa hadi sasa NPC bado haijakosa kuthibitisha ripoti ya kazi za serikali au kukataa kuidhinisha maofisa viongozi walioteuliwa, kura nyakati zote hazikosi pingamizi.

Kumekuwa na matukio ambapo muswada wa kutunga sheria uliowekwa mbele na Baraza la Serikali la China umeondolewa au kurekebishwa kutokana na pingamizi ndani ya NPC.

Nchini China, NPC ina nguvu sana kiasi kwamba, mamlaka yake inajumuisha kubadilisha Katiba ya nchi. Pia inatunga na kurebisha sheria, kuhakikisha utekelezaji wa sheria pamoja na kuchagua na kuamua nafasi za wakuu wa serikali.

Aidha NPC inaelekeza uongozi wa serikali na mahakama na kuamua masuala muhimu ya serikali. Isitoshe, NPC ina uwezo wa kumteua na kumsimamia Rais, Jaji Mkuu na Mwendesha Mashtaka Mkuu.

Lakini vikao hivi vya Mikutano Miwili vina maana gani kwa dunia? Mbali na kujikita kwenye mambo ya ndani, vikao vya kila mwaka vya NPC na CPPCC vina ushawishi unaosambaa kote hasa kwa masuala ya kimataifa.

Wajumbe wa NPC wanachagua uongozi mpya wa nchi ikiwa ni pamoja na Bunge la Umma, Rais na Makamu wake.

Wajumbe hao pia huamua juu ya uteuzi wa Waziri Mkuu, Manaibu wake bila kusahau orodha ya Baraza la Serikali la China. Sera ya nje ya nchi pia ni moja ya majukumu ya kusanyiko hilo la kila mwaka.

Mikutano hiyo imeangaziwa sana kwa miaka ya hivi karibuni tangu China ilipozindua mfumo mpya wa ushirikiano na mataifa mengine duniani.

Idadi kubwa ya mataifa sasa yameingia makubaliano juu ya maendeleo na China kupitia mpango wa ‘Ukanda Mmoja, Njia Moja’, programu inayolenga kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja.

Mpango huu umejadiliwa kwa mapana na marefu wakati wote vikao hivyo vinapofanyika.

Wakati ambapo dunia inashuhudia mabadiliko katika mazingira ya kiuchumi na kuinuka kwa sera ya kujilinda kibiashara na vitendo vya upande mmoja, China inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuzidisha mageuzi na kufungua mlango zaidi kwa mataifa ya nje wakati wa Mikutano Mikuu.

MTWARA ni mkoa unaojivunia kuwa na maliasili nyingi na maeneo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi