loader
Picha

Utabiri mvua za vuli unavyosaidia kukabili maafa

KIWANGO cha utabiri wa hali ya hewa nchini kinazidi kukua kila mwaka kiasi ambacho wananchi wanazidi kutumia utabiri katika shughuli mbalimbali.

Katika utabiri wa mvua za msimu wa vuli kwa kwaka huu,umeonesha wazi mvua licha ya kuwa baraka kwa kupata maji, mavuno na mengineyo lakini kwa baadhi ya maeneo na sekta mbalimbali mvua inaweza kuwa balaa kama hatua madhubutu hazitachukuliwa.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekuwa ikijitahidi kutoa utabiri wa hali ya hewa ili kusaidia kukabiliana na majanga, kujiandaa kwa kilimo pamoja na kusaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Kuanzia mwezi huu mwanzoni Tanzania iko katika msimu wa mvua za vuli zimegawanyika katika maeneo mawili kwa mikoa inayopata mvua mara moja kwa mwaka na ile inayopata mvua mara mbili kwa mwaka.

Katika maeneo ya mvua zinazoendelea katika mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Agness Kijazi anataja maeneo hayo kuwa ni Ukanda wa Ziwa Victoria mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara ambayo yanapata mvua nyingi mpaka Januari mwakani.

Maeneo mengine ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro mikoa itakayokuwa na mvua chache za wastani mpaka chini ya wastani zitakazomalizika mwisho wa Desemba,mwaka huu.

Anasema maeneo ya Pwani ya Kaskazini mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro Kaskazini mvua za vuli zitakuwa za wastani na chini ya wastani hivyo kukosa mvua za kutosha ambazo zilianza wiki ya pili ya mwezi ujao hadi Desemba.

Katika kipindi hiki , tayari mrejesho mzuri wa mvua hizo zinazotarajia kuisha Desemba mwaka huu kwa mvua nyingi kunyesha maeneo mbalimbali ikiwemo jijini Dar es Salaam.

Kutokana na utabiri wa hali ya hewa kumekuwa na udhibiti wa maafa katika kilimo na sekta nyingine kuchukua tahadhari ya kutosha kulingana na hali ya utabiri wa maeneo husika ili kuepuka majanga ya ukosefu wa chakula, mafuriko, uharibifu wa miundombinu, maradhi na mengineyo.

Anasema maeneo mengine ya kati, kusini na magharibi mwa nchi hupata mvua mara moja kwa mwaka na utabiri wake wa mvua umetolewa wiki hii.

Katika utabiri wake wa mwelekeo wa msimu wa mvua za mwaka kwa kipindi cha mwezi Novemba 2019 hadi Aprili 2020 Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dk Kijazi anasema msimu huo ni mahususi kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka ikiwa ni mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Njombe,Iringa, Lindi, Dodoma, Singida, Mtwara na Kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Anasema mvua zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Kusini mwa mkoa wa Morogoro, Lindi na Mtwara.

Kwa upande mwingine maeneo ya mikoa ya Kigoma, Katavi, na Rukwa yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Pia ,vipindi vya mvua nyingi vinatarajiwa katika miezi ya Novemba 2019 na Januari 2020, mvua zinatarajiwa kupungua katika baadhi ya maeneo kwa miezi ya Disemba, 2019 na Februari, 2020.

Huku mvua zikitarajia kuanza wiki ya nne ya mwezi huu kwa maeneo ya mkoa wa Kigoma na kutawanyika katika mikoa mingine katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba, 2019. Pia katika wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2020 mvua zinatarajiwa kuisha katika maeneo mengi ya nyanda za juu kusini magharibi na pwani ya kusini.

Aidha kwa maeneo mengi ya kanda ya kati na magharibi, mvua zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2020.

Anaeleza mifumo iliyotumika kupata utabiri huo ni katika bahari ya Hindi, eneo la magharibi mwa bahari hiyo linatarajiwa kuwa na joto la juu zaidi ya wastani kulinganisha na eneo la mashariki mwa bahari hiyo (Pwani ya Indonesia).

“Hata hivyo, joto la juu zaidi linaonekana katika eneo la kati ya bahari ya Hindi na Pwani ya Somalia. Joto la bahari katika eneo la kusini-magharibi mwa bahari ya Hindi linatarajiwa kuwa la juu ya wastani hali inayotarajiwa kusababisha kutokea kwa migandamizo midogo ya hewa na vimbunga katika eneo hilo,”anasema.

Anasema migandamizo midogo ya hewa pamoja na vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi inatarajiwa kuvuta upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Congo na hivyo kusababisha mvua katika maeneo mengi hapa nchini.

Huku katika eneo la mashariki mwa bahari ya Atlantiki, joto la bahari linatarajiwa kuwa la juu ya wastani na hivyo kuwa na mchango mdogo kwa mifumo na mwenendo wa mvua katika maeneo ya magharibi mwa nchi.

Mkurugenzi huyo anatoa ushauri kwa mamlaka husika kuwa katika sekta za Kilimo, Mifugo na Wanyamapori katika kipindi hicho hali ya unyevunyevu wa udongo kwa ustawi wa mazao vinatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi.

Hata hivyo, mazao yasiyohitaji maji mengi, kama vile mahindi, maharage na mtama,yanaweza kuathiriwa na hali ya unyevunyevu wa kupitiliza na maji kutuama mashambani hususan kwa maeneo yanayotarajiwa kuwa na mvua za juu ya wastani hadi wastani.

“Aidha, magonjwa ya wanyama na uharibifu wa miundombinu ya kilimo vinaweza kujitokeza huku upatikanaji wa malisho na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori vinatarajiwa kuwa vya kuridhisha katika maeneo mengi,”anabainisha.

Anataka wananchi kutumia teknolojia ya uvunaji maji ya mvua ili kuhifadhi maji kwa matumizi katika kipindi cha baadae huku akishauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa kupata ushauri kwa wataalam wa sekta husika ikiwemo maafisa ugani.

Anasema katika sekta ya uvuvi kuwa kutakuwa na maji ya kutosha na ziada katika maziwa, mito na mabwawa na hali hiyo inatarajiwa kuchangia kuongezeka kwa chakula cha samaki na kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya Uvuvi.

Huku menejimenti ya Hifadhi ya Chukula wanatakiwa kuimarisha maghala ya hifadhi za chakula katika ngazi mbalimbali ili kuwa na nafasi ya kutosha kuhifadhi ziada ya chakula kitakachozalishwa.

Pamoja na kuandaa na kusambaza viwatilifu vya kutosha kwa wakati ili kukabiliana na ongezeko la wadudu waharibifu mashambani na kwenye maghala ya hifadhi za chakula.

Dk Kijazi anataka sekta za Nishati, Madini na Maji kuwepo kwa ongezeko la maji katika mabwawa hivyo kunufaisha matumizi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme.

Anasema katika sekta ya madini, wachimbaji, hususan wale wadogo wadogo wanashauriwa kuwa makini kwani ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha maporomoko ya ardhi na maji kujaa kwenye migodi.

Kwa mujibu wa Dk Kijazi wakazi katika maeneo ya mito yenye historia ya kujaa na kuleta mafuriko wachukue tahadhari mapema wakishirikiana na taasisi na mamlaka husika katika maeneo yao.

Katika vipindi vya mvua kubwa vinavyotarajiwa kujitokeza, anazishauri mamlaka za miji na jiji zinashauriwa kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa mifumo na njia za kupitisha maji zinafanya kazi katika kiwango cha kutosha ili kuepusha maji kutuama na kusababisha mafuriko, uharibifu wa miundombinu na upotevu wa maisha na mali.

Huku sekta ya afya zikitakiwa kuchukua hatua kwani mvua kubwa zinaweza kusabibisha magonjwa ya mlipuko yanayohusiana na maji, wakati menejimenti ya maafa inashauriwa taarifa zitolewe kwa wakazi wa maeneo ya mabondeni, karibu na mito, na yale ya tambarare, kupitia ngazi zinazohusika kama vile Kamati za maafa za Mkoa na Wilaya. Kamati zinashauriwa kufanya maandalizi ikiwemo kutafuta na kutenga rasilimali za kukabiliana na maafa yanayoweza kujitokeza.

Aidha, taasisi, kampuni za ujenzi na usafirishaji pamoja na wadau wengine wanashauriwa kujiandaa kuchukua hatua za dharura iwapo kutatokea uharibifu wa miundombinu ili kupunguza athari na hasara zinazoweza kutokea.

Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, wananchi na wadau wengine wanashauriwa kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii kama kawaida.

“Naendelea kutoa rai kwa wananchi wa mikoa husika kuzitumia mvua hizi kwa kupanda mazao sahihi kwa kufuata ushauri wa wataalamu, kama tunavyoona maeneo mengi yatarajiwa kuwa na mvua za juu ya wastani hadi wastani,” anasema Dk Kijazi.

Anataka katika maeneo yote kuendelea kutoa utabiri wa siku 10 ili sekta hizo zijipange huku wananchi wkaifuatilia tahadhari na angalizo zinazolewa na mamlaka ikiwa kuna mvua kubwa,upepo na mawimbi ili kujikinga na maafa na shughuli nyingine za maendeleo.

MTWARA ni mkoa unaojivunia kuwa na maliasili nyingi na maeneo ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi