loader
Picha

‘Mwenge ni maono ya Nyerere, utaendelea kuheshimiwa’

SERIKALI imesema itaendelea kuuheshimu na kuukimbiza Mwenge wa Uhuru kwa kuwa umetokana na maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ni alama muhimu ya mapambano dhidi ya ukoloni na alama ya uhuru wa Taifa la Tanzania.

Mwenge huo utazimwa leo mkoani Lindi ambapo Rais John Magufuli akitarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzimaji huo.

Miongoni mwa mambo Mwalimu Nyerere aliyasisitiza ni taifa la Tanzania kuendelea kuwa na umoja, uzalendo, kujitegemea na kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.

Hayo yalibainishwa jana mkoani Lindi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Wa- ziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alipofungua Mdahalo wa Miaka 20 ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa Katika Kilele cha Mbio za Mwenge na Sherehe ya Wiki ya Vijana Kitaifa.

Waziri Mhagama aliutaja Mwenge wa Uhuru kuwa miongoni mwa tunu muhimu ambazo Baba wa Taifa aliziacha kwani Mwenge wa Uhuru ni alama ya mapambano dhidi ya ukoloni na uhuru wa taifa la Tanzania na umeendelea kulifanya taifa kuwa pamoja.

Alisema Mwaka 1958 Mwalimu Nyerere alipochaguliwa kuwa Mjumbe katika Baraza la Kikoloni la Kutunga Sheria, ndoto yake ilikuwa kuona Tanganyika na Afrika nzima zinakuwa huru.

Katika hilo, Mhagama alinukuu maneno ya Baba wa Taifa aliyoyasema kuhusu Mwenge wa Uhuru kabla ya kupata uhuru,

“Sisi watu wa Tanganyika tunataka uhuru wetu, mkitupatia, tutauwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki, heshima palipojaa dharau.”

Alisema maneno hayo aliendelea kuyarudia kila wakati na Mwaka 1959 akiwa katika kikao cha Baraza la Umoja wa Mataifa aliyarudia ili kuwa- fanya Wakoloni watambue kwamba alidhamiria kuwa Tanganyika ilitaka uhuru wake.

Mhagama alisema kuwa katika hotuba yake siku ya uhuru, Baba wa Taifa aliwatangazia Watanganyika na dunia nzima akisema

“Sasa tumekwisha kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo palipo na chuki, ulete heshima mahali palipo na dharau.”

Waziri huyo pamoja na watoa mada wengine waliwasisitiza vijana kumsoma Mwalimu Nyerere ili kujua fikra zake na kumuenzi kwa vitendo na kwa dhati ya mioyo yao.

Matunda na faida za Mwenge wa Uhuru Kwa mujibu wa Waziri Mhagama, Mwenge wa Uhuru umekuwa na matunda na faida muhimu kwa taifa ikiwemo kudumishwa kwa Muungano ambao aliuita Muungano kielelezi Afrika na dunia nzima, ukombozi wa Bara la Afrika kwa kuzisaidia nchi nyingi kupata uhuru, kujenga umoja wa kitaifa kwa kutumia Lugha ya Kiswahili.

Alizitaja faida zingine za Mwenge wa Uhuru kuwa umebaki kuwa chom- bo cha kujenga undugu, maelewano na mshikamano wa taifa, alama ya kupambana na ubaguzi, unyonyaji na rushwa, lakini pia umeendelea kubeba ujumbe wa kudumu wa kupiga vita Ukimwi, dawa za kulevya na malaria.

Watoa mada Baadhi ya watoa mada akiwemo Galus Abeid alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ulianza kukimbizwa kwa mara kwanza Juni 26, 1964 na ulikimbizwa na vijana wanne katika vituo vitano jijini Dar es Salaam.

Alisema baadaye Mwaka 1965 ulikimbizwa na Brigedia Jenerali Moses Nnauye na baadaye ukaanza kukimbizwa kitaifa kila mwaka na kuzimwa siku ya Sherehe za Sabasaba ambayo ilikuwa siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa Chama cha TANU.

Kwa mujibu wa Abeid, Oktoba 14, 2000, Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliagiza Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru ziwe zinafanyika Oktoba 14 kila mwaka am- bayo ni Kumbukizi ya Baba wa Taifa.

Naye Profesa Bernadeta Killian wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema Mwenge wa Uhuru ambao ulianzishwa na Baba wa Taifa ni alama kuwa Tanzania ni nchi huru, unahamasisha uzalendo na utambulisho wa Mtanzania, unatambulisha utamaduni wa Mtanzania, unabainisha marafiki na maadui katika ujenzi wa taifa, unajenga umoja wa kitaifa hususani katika zama hizi za vyama vingi.

Kwa upande wake Goodluck Ng’ingo aliwataka Watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli za kupambana na hila za ukoloni mamboleo na ubeberu unaopinga juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Alisema ukoloni mamboleo na ubeberu ndiyo silaha zinazotumiwa na mataifa makubwa duniani kupinga jitihada za nchi maskini za kutaka kujitegemea.

Alisema hata Baba wa Taifa alipoanzisha Elimu ya Watu Wazima, alipingwa lakini Mwalimu alisimamia kidete uamuzi wake huo na kufanikiwa kwa kuwa asilimia 87 ya Watanzania walijua kusoma na kuandika.

Ng’ingo alisema ukoloni mamboleo na ubeberu unazitawala nchi maskini kupitia misaada, mikopo au ushirikiano wa kiuchumi, kupitia viongozi waliotayari kutekeleza mipango yao na ndiyo maana Mwalimu aliupinga kwa kuwa ni mfumo usiolinufaisha taifa.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kushirikiana na Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Na Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi