loader
Picha

Boeing 787-8 Dreamliner nyingine katika majaribio ya mwisho

NDEGE mpya ya pili aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyonunuliwa na serikali hivi karibuni inatarajiwa kuwasili nchini wiki chache zijazo baada ya kukamilika kwa matengenezo yanayofanywa na Kampuni ya Boeing ya Marekani.

Ndege hiyo mpya imepewa jina la Kisiwa cha Rubondo na taarifa zake pamoja na picha ilitolewa kwa mara ya kwanza Oktoba 7, mwaka huu na Mtandao wa kijamii wa Twitter wa Uwanja wa Ndege wa Paine.

Mtandao huo wa Uwanja wa Ndege unaoitwa Paine Airport @mattcawby uko Washington, Marekani na unatumiwa na Kampuni ya Boeing watengenezaji wa ndege za 747, 767, 777 na 787 kufanyia majaribio ndege hizo.

Wakati maandalizi ya ndege hiyo yakiwa kwenye hatua hiyo nzuri, Rais John Magufuli jana mkoani Lindi amezungumzia ujio wa ndege hiyo kwenye kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru ulioambatana na Kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Wiki ya Vijana.

Akizungumzia ujio wa ndege hiyo, Rais Magufuli alisema ndege hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 262, na kusema itawasili katika kipindi tajwa ikiwa ni mpango wa serikali kuongeza huduma za usafiri wa anga nchini.

Alisema kuja kwa ndege hiyo na nyingine aina ya Bombardier 8-Q400 itakayowasili baadaye mwaka huu, ni maboresho yanayoendelea kufanywa na serikali chini ya mkakati wa kuboresha sekta ya usafiri wa anga ambayo kwa kipindi kirefu ilikuwa ikisuasua.

Mwaka 2016 baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani, alizungumza na wananchi na kuahidi serikali itanunua ndege sita zikiwemo ndege kubwa tatu za abiria ikiwa ni juhudi za kufufua Kampuni ya Ndege la Tanzania (ATCL).

Katika kuonesha dhamira ya dhati kwenye hilo, Rais alikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko ya Afrika wa Kampuni ya Boeing yenye makao yake nchini Marekani, Jim Deboo, Ikulu jijini Dar es Salaam. Ahadi ya rais ilitimia kwa ndege mbili mpya aina Bombardier Q400 Dash 8 NextGen zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 160 hadi 240 zilinunuliwa na kuwasili nchini Septemba mwaka 2016 zikitokea Canada zilikotengenezwa.

Baadaye Rais aliahidi serikali itanunua tena ndege nyingine mpya aina ya Boeing Dreamliner ambayo ndiyo iko kwenye hatua za mwisho za majaribio kabla ya kuhakikiwa na timu ya wataalamu kwenda kukagua kisha kuileta.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi alikiri ndege hiyo iko kwenye hatua za mwisho za matengenezo na wanasubiri nyaraka kutoka Boeing inayotengeneza ndege hiyo ili kujua siku itakayowasili nchini.

“Tunachosubiri kwa sasa ni ‘delivered note’ (nyaraka za kuwasili) na ndipo tutakapotoa taarifa rasmi kuwa lini ndege hiyo itawasili nchini, lakini kwa sasa siko kwenye nafasi nzuri ya kueleza suala hilo kwa kuwa watengenezaji wake bado hawajatuletea nyaraka hizo,” alisema Matindi.

Awali taarifa zilizotolewa na kwa nyakati tofauti na viongozi mbalimbali akiwemo Rais Magufuli, zilibainisha kuwa ndege hiyo na nyingine aina ya Bombardier Dash 8 -Q400 zingewasili katika kipindi cha Oktoba na Novemba mwaka huu, suala linalochochea dalili za karibu za kuwasili kwa ndege hiyo.

Kukamilika kwa ndege hiyo kutaifanya serikali kufikisha idadi ya ndege nane zikihusisha ndege za Bombardier -8 Q400 tatu, mbili ambazo zilifika nchini Septemba 2016 na moja Juni 2017; Airbus A220-300 mbili na Boeing 787 Dreamliner ambazo zilitua nchini kati ya Mei na Julai mwaka jana.

Kabla ya hapo, ATCL zamani ikijulikana kama Air Tanzania lilikuwa na ndege moja ya Bombardier -8 Q300 iliyokuwa ikihudumu tangu 2011 kabla ya mpango wa Rais Magufuli wa kulifufua shirika hilo lililoanzishwa 1977.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kushirikiana na Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi