loader
Picha

Wataopata mikopo HESLB kujulikana Alhamisi

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) itatangaza orodha ya kwanza ya majina ya wanafunzi walioomba na kupangiwa mikopo keshokutwa Alhamisi.

Hatua hiyo inatokana na kukamilika kwa kazi ya uchambuzi wa maombi ya mikopo 55,444 ya wanafunzi ambao wamepata udahili katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul- Razaq Badru, amesema wanafunzi watakaopangiwa mikopo watapata taarifa zao kupitia akaunti zao kwenye mtandao wa taasisi hiyo.

Amesema HESLB pia imeamua kutoa fursa kwa waombaji 4,794 ambao hadi sasa hawajakamilisha maombi yao kwa kuambatisha nyaraka muhimu mtandaoni.

“Tulitoa siku sita ambazo zinakamilika kesho, Oktoba 15, lakini bado kuna hao ambao tunawaona katika mfumo kuwa bado hawajakamilisha, inawezekana wapo ambao hawahitaji tena mkopo, lakini inawezekana wapo wahitaji wa kweli, kwa hiyo tumeamua hatutafunga mfumo wetu na wanaweza kuendelea kukamilisha.”

“Wanaweza kuingia katika akaunti zao na kukamilisha, lakini kwa wale ambao watafika vyuoni wakiwa bado hawajakamilisha, tunakutana na maofisa mikopo Ijumaa wiki hii mjini Morogoro na wawahudumie wanafunzi hawa wakiwa vyuoni kwa kupokea nyaraka zinazokosekana na kuziwasilisha kwetu ili wote wenye uhitaji wapangiwe mkopo,” amesema Badru.

Alisema utoaji wa mikopo pia huzingatia makundi maalum kama yatima waliowasilisha nakala za vyeti vya vifo vya wazazi wao, wenye ulemavu walioambatisha barua kutoka kwa waganga wakuu wa wilaya au mkoa na waombaji mkopo ambao kutokana na hali duni ya kiuchumi walifadhiliwa katika masomo yao ya sekondari au stashahada.

Kuhusu malengo ya mwaka huu wa masomo, Badru alisema serikali imetenga Sh bilioni 450 ambazo zitawanufaisha wanafunzi 128,285, kati yao, zaidi ya 45,000 watakuwa ni wa mwaka wa kwanza na wengine 83,285 ni wanaoendelea na masomo.

Bajeti ya HESLB ya mwaka wa masomo 2018/2019 ilikuwa Sh bilioni 427.5 na iliwanufaisha wanafunzi 123,329.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kushirikiana na Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi