loader
Picha

Siku ya Kimataifa ya Wanawake wa Vijijini na faida kiuchumi

LEO Oktoba 15 ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake wa Vijijini. Siku hii imekusudiwa kutazama masuala muhimu ya wanawake vijijini duniani kote, kwani wao ni taa lakini inayong’aa katika giza nene, hukanyagwa bila kuonekana.

Kimsingi, kuwawezesha wanawake na wasichana wa vijijini ni jambo muhimu ili kujenga mustakabali bora kwa kila mtu duniani. Licha ya shughuli za wanawake wa vijijini kuongeza usalama wa chakula na kuondoa umaskini katika maeneo ya vijijini, umuhimu wao bado ‘unakanyagwa’ kama kwamba hauonekani katika jamii.

Kwa mujibu wa takwimu, idadi ya wanawake wanaohusika katika shughuli za kiuchumi za vijijini hufikia robo ya idadi ya watu duniani. Hivyo, mchango wao katika uchumi nchini na hata duniani, ni mkubwa na wenye thamani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Anthonio Guterres kwenye ujumbe wake anasema uwezeshaji kwa wanawake wa vijijini una umuhimu mkubwa katika ujenzi wa dunia yenye amani na ustawi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa makala moja ya kimtandao ya Vatican News, ripoti iliyotolewa Novemba 25, 2018 na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa na Uhalifu, (UNODC) inasema nyumbani pia pamekuwa mahali hatari zaidi kwa wanawake na hususan kwa mauaji na ukatili, wengi wakipoteza maisha mikononi mwa wenzi wao au familia na kwamba, wanawake 6 huuawa kila baada ya saa moja na watu wanaowafahamu. Guterres anasema: “Wanawake wa vijijini ni msingi kwa maendeleo ya wote.”

Anasisitiza Oktoba 15 iwe siku inayokumbuka kweli wanawake wote vijijini. Anasema ili kuwajengea uwezo wanawake, lazima nchi zihakikishe wasichana na wanawake vijijini wanafurahia haki zao za binadamu. Anataja haki hizo kuwa ni pamoja na uwezo wa kumiliki ardhi, kupata chakula cha kutosha na chenye lishe, maisha yasiyo na vurugu, ukatili wala unyanyaswaji na waweze pia kupata huduma bora ya afya ikiwemo afya ya uzazi bila kusahau elimu bora na nafuu.

Ibara ya 24(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 inasema kila mtu anayo haki ya kumiliki mali, na haki ya hifadhi ya mali yake kwa mujibu wa sheria. Nacho Kifungu cha 3(2) cha Sheria za Ardhi Namba 4 na 5 kinaainisha haki ya kila mwanamke kupata, kumiliki, kutumia na kuuza au kuigawa ardhi. Ifahamike kuwa haki ya mwanamke ni sawa sawa na haki ya mwanamume yeyote kwa viwango vilevile na masharti yaleyale.

Halikadhalika, Kifungu cha 23(2)(c) cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya Mwaka 1999 kimeainisha kwamba, katika kupitisha uamuzi kuhusu maombi ya hakimiliki ya kimila, halmashauri ya kijiji inapaswa kuzingatia maombi ya wanawake sawasawa na maombi ya wanaume. Kimsingi, wanawake wa vijijini hukumbana na changamoto za kimfumo na vizuizi katika kufurahia haki zao kikamilifu licha ya wao kuwa sababu ya chachu ya maendeleo yaliyopo katika maeneo ya vijijini na uzalishaji wa chakula.

Changamoto kubwa inayowakabili wanawake wengi vijijini ni kukosa umiliki wa ardhi wanayolima na mara nyingi hunyimwa huduma za kifedha zinazostahili kuwaondoa katika umaskini, ili waishi bila usumbufu katika kupata huduma zikwemo za afya, elimu, maji safi na salama. Kadhalika katika nchi nyingi, mahitaji ya aina yake ya wanawake hao hayashughulikiwi katika sheria, sera za kitaifa na mikoa, na katika bajeti.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya wanawake, UNWomen, limekuwa likiitaka jumuiya ya kimataifa kufanya kazi na wanawake wa vijijini wakiwamo wasichana kila mahali na kuwekeza katika miundombinu endelevu, huduma na ulinzi, vitu vinavyoweza kubadilisha maisha yao, ustawi na ujasiri wao. Wanawake wa vijijini ndio huzalisha asilimia kubwa ya chakula, ndio hutunza mazingira yanayosaidiakatika kupunguza hatari ya majanga miongoni mwa jamii zao, hivyo kuwawezesha ni muhimu ili kujenga mustakabali bora kwa kila mtu duniani.

UN-Women linasema katika nchi nyingi duniani, wanawake wa vijijini na wasichana wanakabiliwa na changamoto za miundombinu, huduma na kulindwa likisema uwepo wa changamoto hizi unahitaji mabadiliko makubwa ili zisiweze kuendelea kuwepo na kukandamiza maisha ya wanawake na wasichana. Mpango wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake wa Vijijini ulionekana mwaka 1995 katika Mkutano wa Wanawake wa Umoja wa Mataifa.

Mwaka 2007 maadhimisho haya yakafanywa kuwa tukio muhimu na wazo kukubaliwa rasmi kuwa yatafanyika kila Oktoba 15. Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulitambua mchango wa wanawake katika kilimo. 0685 666964 au bjhiluka@ yahoo.com

MTWARA ni mkoa unaojivunia kuwa na maliasili nyingi na maeneo ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi