loader
Picha

Wanaovunja misingi ya uchumi kuwajibishwa

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, amewataka maofisa wadhamini kuwawajibisha wanaovunja misingi ya kukuza uchumi wa nchi.

Amesema hayo leo katika ukumbi wa kiwanda cha mafuta na makonyo Wawi, wakati alipokutana na watendaji na viongozi wakuu wa serikali pamoja na viongozi wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaofanya kazi zao kisiwani Pemba.

Amesema mwaka jana kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar ilifikia asilimia 7.1 na matarajio ni kukua mwaka hadi mwaka kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii katika visiwa hivyo.

“Mapato yanakusanywa kwa ufanisi mzuri na kinachokusanywa ndicho kinachotumika na hakuna tatizo la matumizi ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hivi sasa,” amesema.

Rais Shein alisema wakati anaingia madarakani mwaka 2010, serikali ilikuwa ikikusanya Sh bilioni 13.5 kwa mwezi, lakini sasa inakusanya Sh bilioni 65.7 kwa mwezi.

Alisema mambo mengi ya maendeleo yanayofanywa na SMZ yanatekelezwa kutokana na fedha zake za ndani japo hakitoshi, hivyo juhudi zaidi zinahitajika.

Hata hivyo, alisema pamoja na juhudi hizo za serikali, wapo wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi na kuisisitiza jamii kulipa kodi sambamba na kuchukua risiti wanaponunua bidhaa ili kuongeza mapato ya serikali.

Kuhusu mfumuko wa bei, Rais Shein alisema kwa Zanzibar uko chini, ambapo wakati anaingia madarakani ulikuwa asilimia 18 na hivi sasa uko chini ya tarakimu moja, huku bei za bidhaa zikiwa zimepungua kwa kiasi kikubwa.

Alisema licha ya kuwapo changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bei za bidhaa pamoja na kufanya magendo, lakini juhudi zinaendelea kuchukuliwa kudhibiti hali hiyo ili kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanaishi vizuri.

Aidha, amesema kuna kila sababu wananchi wa Zanzibar kutibiwa bure ikiwamo kupatiwa huduma zote za uchunguzi wa afya na kuitaka wizara ya afya kusimamia suala hilo na kuwachukulia hatua watakaofanya hadaa washtakiwe kwa kuhujumu uchumi.

Rais Shein alieleza juhudi zinazochukuliwa na serikali kuhakikisha wilaya ya Micheweni inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji safi na salama, huku akieleza kuwa, hadi mwishoni mwa mwaka huu katika mji wa Zanzibar na vitongoji vyake ukiaemo Mji Mkongwe tatizo la maji litakuwa historia.

Aliwataka viongozi hao kuwasikiliza watu wanaokwenda ofisini mwao kufuata huduma na kuwatatulia shida zao.

SHIRIKA la Taifa la Biashara (ZSTC) limesema ni makosa kwa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Zanzibar

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi