loader
Picha

Samia: Hatutavumilia wanaohujumu viwanda

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema serikali haitavumilia mtu anayekwamisha ujenzi wa uchumi wa viwanda ikiwa ni pamoja na kuzalisha au kuingiza nchini bidhaa bandia.

Alitoa rai hiyo jana kupitia hotuba ya ufunguzi wa maonesho ya pili ya viwanda mkoani Pwani iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya.

“Serikali haitamvumilia yeyote atakayekwamisha ujenzi wa viwanda ikiwa ni pamoja na kuzalisha au kuingiza bidhaa bandia zinazochafua taswira ya viwanda vya ndani,” alisema.

Alitaka mamlaka zinazohusika na ubora wa bidhaa kuhakikisha zisizo bora haziingizwi nchini. Alishauri pia wenye viwanda kuhakikisha wanazalisha bidhaa zinazotumiwa zaidi na Watanzania.

Alitaka mamlaka za ukaguzi hususani Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Shirika la Viwango (TBS) kuweka sheria, taratibu na kanuni wazi zisiwe kikwazo kwa wawekezaji.

“Haiwezekani tukawa tunahamasisha uwekezaji halafu ninyi mkawa kikwazo” alisema na kuwataka kutoa msaada pale panapohitajika, kushirikiana na wadau na kuhakikisha nchi inapiga hatua za haraka katika ujenzi wa viwanda,” alisema.

Vile vile aliwataka wawekezaji pia kuwa na tabia ya kufuatilia kuhusu nini wanatakiwa kufanya kwa mujibu wa sheria zilizopo na kutekeleza. Alisema Serikali inafanyia kazi tozo mbalimbali 114 zinaoonekana kero na kwamba tayari serikali imefuta tozo 54 na itandelea kufuta nyingine. Makamu wa Rais aliwahimiza Watanzania kupenda kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini kupanua soko la viwanda na hivyo kuviwezesha kutoa ajira zaidi kwa Watanzania.

Aliiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara, kitengo cha masoko kuhamasisha Watanzania kupenda bidhaa zinazozalishwa nchini na kuhakikisha serikali inatumia bidhaa za ndani katika miradi yake. Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais alisema mwaka jana alitoa maagizo kadhaa ambayo alitaka mkoa umpe mrejesho kuhusu utekelezaji wake.

Alitaja maagizo hayo ikiwamo ulinzi wa nafasi za Watanzania kupata ajia zenye staha, kuhakikisha sheria za kazi zinafuatwa na wizara ya kazi kupita mara kwa mara viwandani, kuhakikisha usalama na maslahi ya wafanyakazi yanazingatiwa Maagizo mengine alisema ni kuhakikisha mapato yatokanayo na viwanda yanatumika kuchangia maendeleo ya jamii na kunakuwa na mipango madhubuti ya kulinda ajira kwa wakazi wa Pwani sambamba na kujengwa kwa chuo cha ufundi kuwanoa.

Alisema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya viwanda na biashara ambayo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, kuboresha bandari, kununua ndege kurahisha usafiri wa watu na mizigo pamoja na kuleta umeme wa uhakika.

“Tutaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara kati ya sekta ya umma na binafsi,” alisisitiza Samia.

Alipongeza mkoa wa Pwani kwa kufanikisha maonesho ya viwanda na kusema bidhaa nyingi zilizooneshwa ni bora. Halikadhalika aliwapongeza wamiliki wa viwanda kujitokeza na kuwataka ambao hawajajitokeza kufanya hivyo ili bidhaa zao kufahamika kwa wateja.

Maonesho hayo yaliyozinduliwa jana yatafungwa Oktoba 23 na keshokutwa Jumamosi kutakuwa na Kongamano la Fursa za Uwekezaji. Makamu wa Rais pia alitoa salamu za Rais John Magufuli akisema alitamani kushiriki kwenye maonesho hayo lakini anatingwa na shughuli mbalimbali za kitaifa.

“Rais anawapongeza kwa utayari wenu wa kupokea hivi viwanda na kulinda amani na mazingira yanayowezesha viwanda kufanya vyema... Siku zijazo bila shaka mtatanua wigo na kushirikisha mikoa jirani. Rais anaamini maonesho yatakuwa chachu ya kuvutia wawekezaji zaidi mkoa wa Pwani,” alisema.

Akizungumza kama Naibu wa Viwanda na Biashara, Manyanya alisema wizara yake itahakikisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji zinapatiwa ufumbuzi. “Tutahakikisha katika wizara hakuna visingizio au vichaka vya sheria vinavyoleta usumbufu,” alisema Mayanya.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kushirikiana na Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu, Kibaha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi