loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Malikale, vivutio lukuki vinavyoiuza Wilaya ya Kisarawe

“TUMEGUNDUA wilaya ya Kisarawe ina fursa na vivutio vingi vya utalii ambavyo havijaguswa wala kutambulika kwa wengi.”

Ndivyo anavyosema Katibu wa Chama cha Watembeza Watalii Kusini mwa Tanzania (STTGS), Dioniz Kazungu katika mazungumzo na uongozi wa wilaya ya Kisarawe kujadiliana masuala ya utalii na fursa lukuki zilizopo katika wilaya hiyo ya mkoa wa Pwani. Anasema waongoza watalii wamegundua Kisarawe ina fursa na vivutio vingi vya utalii ambavyo havijaguswa wala kutambulika kwa wengi.

Mkuu wa Wilaya, Jokate Mwegelo, pamoja na masuala mengine, alitangaza rasmi barabara inayokwenda Hifadhi ya Taifa ya Julius Nyerere kwa wadau hao waitumie kutekeleza azma ya kuhakikisha utalii unachangia mapato wilayani humo. Mkakati wa halmashauri ni kutumia kikamilifu vivutio vya utalii vilivyomo kujiongezea kipato huku barabara hiyo ya kwenda hifadhi ikitarajiwa kufanikisha suala hilo kwa kupitisha watalii wengi.

Katika mkutano uliohudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kisarawe, Mabula Isambula, Jokate anasema Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) amemhakikishia kwamba mwakani barabara hiyo inayokwenda hifadhini itakuwa na ubora utakaowezesha kutumika kwa mwaka mzima.

“Kati ya vitu ambavyo nilikuwa naona Kisarawe tunaweza kufanya vizuri na kujiingizia kipato kama halmashauri na pia kama taifa, ni kupitia utalii,” anasema Jokate na kuomba waongoza watalii kuwa mabalozi wema katika kukaribisha watalii washuhudie vivutio mbalimbali.

Ofisa Utalii wa Wilaya ya Kisarawe, Kenedy Muhoza inasema vipo vivutio vya aina tatu vinavyopatikana katika maeneo ya hifadhi za misitu, taasisi za umma, taasisi za dini na watu binafsi. Vivutio hivyo ni vya asili, malikale na vivutio vya utalii. Vivutio vya asili Muhoza anataja vivutio vya utalii vinavyotapatikana wilayani Kisarawe kuwa ni pamoja na vinavyopatikana katika hifadhi za misitu Pugu na Kazimzumbwi.

Wamo ndege wa ina mbalimbali, vipepeo, bwawa la Minaki, pango la tambiko za asili la Minaki na njia za asili zinazotumiwa na watembea kwa miguu na wapanda milima. Katika misitu ya Pugu na Kazimzumbwi, ipo pia kambi ya mianzini, mbega weupe na weusi, maisha ya mende na popo ndani ya mapango, kambi ya watalii ya Kinyanyiko na milima na mabonde yanayowezesha kuona jiji la Dar es Salaam.

Vivutio vingine vya asili ni wanyamapori wanaohama kutoka Hifadhi ya Taifa ya Julius Nyerere kwenda vijiji mbalimbali ikiwamo Kitoga Chole, Vikumburu, Panga la Muingereza, Sofu, Mafumbi, Ving’andi na Marui, Ngwata, Kihare, Kolesa, Mtunani na Gwata. Wanyama hao ni simba, nyumbu, nyati, twiga, pofu, pongo, digidigi, tembo, nyoka, mijusi mikubwa na midogo. Mto Ruvu ni kivutio kingine cha asili ambacho ndege na wanyamapori wa aina mbalimbali wanapatikana.

Mamba, viboko na samaki pia wanapatikana katika mto huo unaopatikana katika vijiji vya Gwata, Mafizi na Nyani. Bustani ya kufuga wanyama ni eneo linalozalisha na kutunza wanyamapori linalomilikiwa na kampuni binafsi. Eneo hilo lina wanyamapori mbalimbali wakiwamo simba, nyumbu, pundamilia, fisi na wanyamapori wadogo kama vile kima, mbega, nyoka, mijusi na ndege. Malikale Muhoza anataja vivutio vya malikale katika kijiji cha Kisangire ambako kuna boma au ngome ya Mjerumani. Boma hilo limezungukwa na hifadhi ya msitu wa kijiji cha Kisangire.

Kuna maeneo mazuri ya mabonde na milima inayowezesha kuona bonde la Rufiji na Hifadhi ya Taifa ya Julius Nyerere. Aidha, kuna daraja lijulikanalo kama ‘Daraja la Mungu’ lililojengwa kwa nguvu za wenyeji enzi za utawala wa Mjerumani. Katika kitongoji cha Sanze, kata ya Kazimzumbwi lipo kaburi la Chifu Sanze, kaburi la watumwa wengi waliozikwa pamoja, kaburi la Mjerumani wa kwanza kufika kwenye kitongoji hicho pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya wa kwanza wa Kijerumani.

Katika kijiji cha Chang’ombe A na Maneromango Kaskazini kitongoji cha Sembe, yapo mawe mawili makubwa yanayoaminika kuwa ni vimondo vilivyoanguka kutoka angani miaka mingi iliyopita. Chuo cha Biblia Maneromango ni kivutio kingine cha malikale ambacho ofisa utalii anakitaja kuwa kinaandika historia ya Ukristo wilayani Kisarawe.

Chuo hicho kipo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na kilijengwa na wakoloni (Wajerumani) kabla ya vita ya kwanza ya dunia. Hilo ni eneo la historia ya Mjerumani na Ukristo katika wilaya ya Kisarawe lenye mnara wa mwaka 1895. Pia yapo makaburi ya Wajerumani. Vile vile, kipo kijiji cha Panga la Muingereza chenye kaburi la askari wa Kiingereza aliyepigana vita ya kwanza ya Wajerumani. Vita ilipiganwa kwenye ngome ya Mjerumani Kisangire.

“Pamoja na kuwa na maeneo mengi katika wilaya yetu ambayo yana vivutio vya asili na mali kale, pia tuna shughuli mbalimbali za utamaduni ambazo zinavutia watalii wengi kuja kujifunza utamaduni wa mkazi wa Kisarawe,” anasema Muhoza.

Shughuli hizo ni pamoja na vikundi vinavyojishughulisha na uchongaji, kupika vyakula vya asili, kucheza ngoma, mafunzo ya jando na unyago. Muhoza anataja vikundi hivyo kuwa ni Boga, Panga la Mwingereza Dogori, Msimbu, Gurujaisi na Masaki. Akizungumzia utalii wa utamaduni, mkuu wa wilaya, Jokate anasema upo umuhimu wa kuanza kutoa mafunzo kwa watembeza wageni wa ndani ili waibue vipaji vya wana Kisarawe na kutengeneza ajira miongoni mwa vijana.

Jokate anashauri Chama cha Waongoza Watalii kisaidie kwa kushirikiana na ofisa utalii watoe mafunzo yatakayowezesha vijana wazawa kutembeza watalii. Katibu wa chama hicho (STTGS), Dioniz Kazungu anasema waongoza watalii wamegundua Kisarawe ina fursa na vivutio vingi vya utalii ambavyo havijaguswa wala kutambulika kwa wengi.

“Kwa vivutio hivyo sisi kama waongoza watalii au mabalozi wa Tanzania kwenye sekta ya utalii tuko tayari kutangaza Kisarawe kwa watalii kama kivutio cha utalii na kushawishi wavitembelee,” anasema Kazungu.

Waongoza watalii hao na wadau wengi wanatabiria Wilaya ya Kisarawe kukua kimapato sambamba na kupata umaarufu kitaifa na kimataifa kutokana na vivutio lukuki vya utalii sambamba na kufunguka kwa barabara ya Dar es Salaam-Kisarawe hadi hifadhi ya taifa ya Julius Nyerere. Kazungu anasema vivutio vya utalii wilayani Kisarawe vitafahamika na wakati huo huo safari za kwenda hifadhini zitakuwa nyingi ikizingatiwa wilaya ipo karibu na jiji la Dar es Salaam.

Kutoka Dar es Salaam hadi gati la kuingia hifadhi ya Julius Nyerere kwa kupitia barabara hiyo ni takribani Kilometa 152.

“Hii ina maana sasa badala ya kufanya safari zile fupi za Mikumi (Morogoro) ambayo iko mbali, sasa safari nyingi zitakuwa Mwalimu Nyerere National Park,” anasema Kazungu.

Fursa uwekezaji Ofisa utalii huyo wa wilaya, Muhoza anasema zipo fursa malimbali za uwekezaji. Anasema Kisarawe ndiyo wilaya pekee iliyopo karibu na hifadhi ya Julius Nyerere (kilometa 152) na ipo karibu na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na jiji la kibiashara la Dar es Salaam kwa takribani kilometa 15.

Uwekezaji mwingine unaoweza kufanyika ni ujenzi wa hoteli, kambi za watalii na mighahawa katika maeneo ya vijiji vinavyopakana na hifadhi ya Nyerere, hifadhi ya msitu wa Pugu, Kazimzumbwi na mto Ruvu. Nyingine ni maeneo ya utalii wa baiskeli, wapanda milima, utafiti, kupiga kambi, kutengeneza filamu, utalii wa chakula, kuona ndenge na utalii wa picha. Fursa nyingine ni za kuanzisha utalii wa boti kwenye mto Ruvu, kuanzisha bustani za wanyamapori, maeneo ya kutunza nyoka na mabwawa ya kuogelea.

Katika kuhakikisha Kisarawe inauzika na utalii unachangia mapato, ofisi ya mkurugenzi mtendaji imetenga kituo maalumu cha burudani kitakachokuwa pembezoni mwa barabara hiyo ya kwenda hifadhi ambayo ni mwendelezo wa dhamira ya serikali ya kukuza na kuendeleza sekta ya utalii. Chama cha Watembeza Watalii Kusini mwa Tanzania (STTGS) kinasema mkoa wa Pwani umekuwa ukijulikana kwa utalii wa mambo ya kale katika eneo la Bagamoyo na kutengwa katika aina nyingine za utalii hivyo kufanya Pwani iwe na vivuti vichache.

STTGS kinaeleza furaha yake kuona Kisarawe ambayo ni sehemu ya ukanda wa Kusini ikianisha vivutio na ‘kuviuza’ kwa utalii wa ndani na nje pamoja na uwekezaji wa maeneo mbalimbali.

ZANZIBAR, katika visiwa vyake viwili vya ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi