loader
Picha

Ukitembelea Hifadhi ya Mkingu utajuta kuchelewa

HIFADHI ya mazingira ni juhudi zinazofanywa na binadamu ili kuhakikisha ulimwengu tunamoishi usiharibiwe na utendaji wake, bali uweze kuwafaa watu wa vizazi vijavyo.

Mazingira ni vitu vyote vinavyoizunguka jamii ya watu. Kwa mfano: miti, mito, maziwa na nyumba. Mazingira yanafaa kuwekwa safi wakati wote kwani yana faida kubwa katika maisha ya mwanadamu.

Tanzania ni nchi iliyojaliwa kuwa na mazingira mazuri ya kuvutia, ikiwa na maeneo saba muhimu yanayofaa kuwekezwa katika sekta ya utalii, ikwemo hifadhi za taifa; maziwa na mito; milima; maeneo ya kihistoria; mapori ya akiba n.k. Hifadhi za taifa zilizopo nchini ni pamoja na Ruaha, Katavi, Rubondo, Ziwa Manyara na Mikumi.

Kwa mujibu wa machapisho ya utalii, zipo hifadhi za taifa 16 ambazo zina fursa kubwa za uwekezaji na kuvutia wageni. Naamini watu wengi wanayafahamu maeneo haya ya hifadhi za taifa, ni maeneo yanayohifadhiwa kwa umakini mkubwa, ni maeneo ambayo shughuli za kibinadamu kama kilimo au ufugaji haviruhusiwi, Haya ni maeneo ambayo hata uwindaji wa kitalii haurususiwi, yamehifadhiwa kwa ajili ya wanyamapori na miti au uoto mwingine wa asili.

Maeneo haya ni maarufu kwa utalii wa picha. Utalii wa picha ndiyo shughuli kubwa ya utalii inayoruhusiwa. Hivyo basi maeneo haya yana vivutio vingi sana vya wanyamapori, uoto wa asili, milima na tabia mbali mbali za nchi. Hivyo kuwa sehemu zenye mvuto wa kipekee sana. Moja wapo wa hifadhi hizi ni Hifadhi asili ya Mkingu iliyopo Wilaya ya Mvomero katika mkoa wa Morogoro.

Hifadhi hii ni eneo muhimu sana kiutalii kutokana na upekee wake wa maisha ya viumbe, mimea pamoja na maisha ya binadamu kwa jumla. Hifadhi hii ina ukubwa wa hekta 26,334 na imezungukwa na vijiji vitano ambavyo vipo ndani ya kata sita na tarafa mbili. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS) imekuwa ikihudumia hifadhi hii kutokana na kuwa na mimea na viumbe ambavyo ni vivutio pekee vya utalii nchini, ambavyo havipatikani mahali popote duniani.

Mhifadhi Mkuu wa Mazingira asili ya Mkingu amenukuliwa akisema kutokana na sifa hizo za kipekee zinazopatikana katika hifadhi hiyo, imekuwa na umuhimu wa aina mbili. Anasema umuhimu wa kwanza ni wa kidunia na mwingine ni umuhimu wa kitaifa. Umuhimu wa kidunia upo katika viumbe, mimea na wanyama.

Kindo anasema hifadhi hii ina wanyama wenye uti wa mgongo 392, kati ya hao 32 hawapatikana mahali popote duniani isipokuwa Mkingu tu. Aidha, kuna vyura na ndege wanaopatikana katika hifadhi hiyo tu. Kindo anasema hifadhi hiyo imejaliwa kuwa na wanyama wanaotambaa 42, kati ya hao 14 hawapatikani mahali popote duniani isipokuwa Mkingu tu, pamoja na aina ya ndege 214, kati ya hao ni aina nne ndiyo wanaopatikana katika hifadhi hiyo.

Mbali na hiyo, ndani ya hifadhi hiyo kuna msitu unaotumika kwa masuala ya mila za Waluguru, ni eneo hilo ni zuri sana ambalo nalo ni kivutio cha utalii ndani ya msitu huo. Aidha, hifadhi hiyo ndiyo chanzo cha Mto Wami, Mto Ruvu na Mto Mkingu ambapo maji hayo yamekuwa yakitumika katika shughuli za kiuchumi kama vile kilimo, uvuvi, mazalia na makazi ya mimea na wanyama bila kusahau kuwa maji hayo ndiyo hutumika kuwanywesha wakazi wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Kama hiyo haitoshi, ndani ya Hifadhi ya Mazingira asili ya Mkingu yapo maporomoko ya Lusingizo yenye mita zaidi ya 50 ambayo ni mojawapo ya kivutio cha utalii, na inasemekana kuwa kwa sasa kuna wawekezaji waliojitokeza kuzalisha umeme katika kivutio hicho cha utalii.

Mbali ya kupatikana kwa wanyama, mimea na vyanzo vya maji katika hifadhi hiyo, kuna pango la Malolo ambalo wenyeji wa Mkindo wana historia kubwa ya pango hilo linalosemwa kuwa wenyeji hawataweza kusahau, kwani kuna mwanamume mmoja aliiba mke wa mtu akaishi naye ndani ya pango hilo kwa muda wa miaka 3 bila kujulikana kijijini.

Pango hilo lina vyumba mithili ya nyumba iliyojengwa. Ndani ya hifadhi hiyo kuna pango ambalo ukikaa nje kuna upepo unaotoka ndani unaopuliza ikiwa ni ishara tosha kuwa, humo ndani ya pango kuna uhai. Mhifadhi wa Mkingu anabainisha kuwa hifadhi hiyo ina jiwe lenye alama za nyayo za binadamu na kwato za mifugo, hiyo ikiwa ni ishara tosha kuwa maisha ya kale ya binadamu yalianzia ndani ya hifadhi hiyo.

Mbali ya mapango yaliyopo ndani ya hifadhi hiyo, pia kuna magofu ya kale ya Wajerumani walioishi ndani ya hifadhi hiyo kabla Vita Kuu ya Pili ya Dunia na baada ya kuondoka kwa Wajerumani ilifanywa kuwa Shule ya Msingi ya kijiji cha Mafuta, na baada ya eneo hilo kutangazwa kuwa hifadhi, shule hiyo ilihamishwa na kujengwa kijijini. Kimsingi, Hifadhi ya Mkingu ni hifadhi iliyojaa vivutio na ukitembelea, lazima utajuta kuchelewa, lakini utafurahi kuanza.

0685 666964 au bjhiluka@ yahoo.com

MTWARA ni mkoa unaojivunia kuwa na maliasili nyingi na maeneo ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi