loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Noti haramu-10

BENARD baada ya kufanikiwa kumteka Diana kimapenzi. Anatambua Diana ni ofisa katika kampuni yenye pesa nyingi. Anazitama. Anafikia na kuamua ’kujilipua’. Benard anaamua kumwambia wazi Diana kuwa yeye ni jambazi, lakini jina hilo analikwepesha na kujiita mhangaikaji. Diana anamkubalia washiriki mpango huo. Endelea.

“Mh!” Benard anaguna anamuuliza swali lingine hapohapo: “Je, mara nyingine huwa unajua oda zinazotolewa na wasafirishaji wa mizigo, na siku ya kuja kulipia gari atakalolikodi?” Diana anajibu: “Mara nyingi wateja huja siku hiyo hiyo na kulipia, na kisha kuchukua gari.” “Ah,” Benard anakunja uso na kuendelea.

“Lakini…” “Subiri,” Diana anamkatiza kauli. “Nimekumbuka, huenda kesho jioni fedha zitaingia...” “Ndiyo...” Diana anasema na kuendelea. “Mteja kaahidi kuja saa kumi na moja za jioni, kwani ana mzigo wake unaopelekwa Mwanza…”

“Akishalipia, fedha hizo mnazipeleka benki?” “Hapana,” Diana anakataa. “Kwa kesho itakuwa siyo rahisi. Labda kesho kutwa ndiyo nitakwenda kuzipeleka Benki.” “Vizuri sana. Mteja huyo anategemea kulipa shilingi ngapi?” “Anasafirisha mitambo ya ujenzi kuelekea Jijini Mwanza. Hivyo atalipa kama shilingi milioni 400 hivi kwa usafirishaji, na atakodi malori matano hivi, ni fedha nyingi.” “Analipia kwa kwa hundi au keshi?”

“Tumemshinikiza kuleta fedha tasilimu, hasa ukizingatia siyo mteja wetu wa mara kwa mara. Yeye anatokea jijini Mwanza, anapofanyia biashara zake za mitambo ya ujenzi.” Kinafuata kimya kifupi, wakati Benard anawaza, “Milioni mia nne?” Ananong’ona kwa furaha. Anayaondoa macho kwa Diana, anaanza kukuna kidevu chake chenye ndevu kidogo hivi. Anayarejesha macho yake kwa Diana, halafu anasema: “Nadhani hutachezea bahati hii, kwani ni nafasi nzuri kwa sisi kubadilika, eti?” “Mh!” Diana anaguna. Hajibu zaidi ya kutabasamu! “Diana unanipenda?” Benard anamuuliza. “Ndiyo, nakupenda Benard…” Diana anasema kwa kauli ambayo inatoka kwa dhati!

“Na mimi nakupenda Diana. Kama tunapendana, basi uwe radhi, fedha hizo tuzichukue, sawa?” “Hakuna tatizo Benard,” Diana anasema huku anamwegemea kifuani kiasi cha kufanya miili yao isisimke! “Mambo si hayo?” Benard naye anamwambia huku anamkumbatia kwa mahaba mazito! Hatimaye ‘yanafuata ni mengine’.

Wanafikia makubaliano kwamba waifanye kazi hiyo ya ‘kukata na shoka’ siku ya tatu. Ama kweli wamedhamiria!

********

Sauti ya muziki laini kama wa chombezo inasikika kutoka ndani ya spika mbili zilizotundikwa kwenye pembe za ukuta, kwenye ukumbi wa vinywaji ndani ya Zebra Inn, mtaa wa Zanaki, eneo la Kisutu. Ni muziki laini ambao siyo wa kukera ndani ya masikio ya wote waliomo humo, zaidi ya kuwaburudisha nafsi zao. Wateja siyo wengi sana hasa ukizingatia ndiyo wanaingia mmoja baada ya mwingine.

Muda huo wa saa kumi na mbili za jioni, ndani ya baa hiyo, wanaonekana wanaume watatu wameizunguka meza moja yenye vinywaji juu yake. Wanakunywa na pengine wanatafuna nyama za kuku kwa kishushio cha bia wanazokunywa. Wanaume hao, Benard Kenga, Tom Koka na Chuma Mtambo, wako katika kikao kingine. Ni miongoni mwa vikao vinavyofanywa na watu hao watatu, kinachofanyika ndani ya hoteli hiyo ya Zebra Inn kama walivyozoea.

Ni wanaume wa shoka, wenye maumbile yaliyoshupaa. Wote hao wanafanya kazi haramu zinazowapatia fedha ambazo siyo za halali, ambazo zinazokubalika na serikali, au jamii ya kitanzania. Ni kazi ambazo wanapozifanya na kufanikiwa, hawapendi kuiona sura ya askari polisi yeyote akiwafuatilia!

Hata wanapozungumzia mpango wa kuwaingizia fedha nyingi, huwa wanachagua hoteli hiyo ya Zebra Inn, ambayo huwa na sehemu nzuri ya kuongelea na hakuna anayefuatilia mambo yao wakionekana ni wateja waliozoeleka. Ni hilo linalowafanya pia waichagua baa hiyo ambayo kwa jioni ya saa kumi na mbili, kuna wateja wasiozidi kumi, kila mmoja amekaa peke yake anajinywea bia yake taratibu. Hivyo inafanya wanaume hao waone kuwa hakuna wa kufuatilia maongezi yao.

Benard ndiye kiongozi kwenye kikao hicho. Baada ya kumaliza mazungumzo mengine yasiyo rasmi, anavuta pumzi ndefu na kuzishusha. Kisha anawaangalia kwa zamu wenzake, Tom na Chuma, kana kwamba anawakagua. “Natumaini sote tu wazima...” Benard anawaambia Tom na Chuma kwa upole. “Sisi wazima kabisa...” Tom na Chuma wanajibu kwa pamoja. “Basi, tumekutana tena hapa baada ya kutoonana kwa muda, tokea siku ile tulipokutana hapa Zebra Inn Hotel,” Benard anasema.

Anaongeza: “Na yote hiyo ni baada ya dili zote kushindikana, kila kona imebana kabisa. Sasa nimeona tukutane hapa niwajulishe kitu muhimu sana!” “Ni sawa, mkuu…” Chuma anasema kwa niaba ya mwenzake, Tom, ambaye ametegesha masikio yake kama mbawala tayari kwa kusikiliza kitakachosemwa na Benard. “Madhumuni yangu ya kutaka tukutane hapa, ni kwamba nataka niwajulishe kuwa nimepata mwanamke bomba sana, na mwenye nazo!” Benard anasema huku anatabasamu kidogo.

“Umepata mwanamke?” Chuma anauliza huku naye anaunda tabasamu la mshangao! “Ndiyo,” Benard anajibu. “Ah, acha masihara mkuu. Sasa umetuitia mambo ya demu wako?” Chuma anauliza kwa ghadhabu kidogo! “Hapana…siyo hayo niliyowaitia…” “Isipokuwa…” “Ni kwamba mwanamke huyo anafanya kazi sehemu ambayo tunaweza kupata fedha chekwa!” “Hayo ndiyo maneno…hebu tupashe mkuu!” “Basi, ni mwanadada huyo mrembo. Anafanya kazi kwenye kampuni ya usafirishaji mizigo ya A.B. Logistics Co. Ltd., iliyoko eneo la Mtava, Barabara ya Nyerere...” Chuma na Tom wanamsikiliza kwa makini

. “Nimeongea naye vizuri sana. Amekubali kutoa ushirikiano ili tuweze kukomba fedha nyingi kama shilingi milioni mia nne hivi, zinazotakiwa kupelekwa benki.” “Tupe michapo bosi…” Tom anacheka huku anakenua meno yake baada ya kusikia ni mambo ya fedha! “Sasa ndiyo tupange jinsi ya kwenda kuzikomba!” Benard anasisitiza! “Hakuna shaka, kama kuna uhakika wa fedha hizo zipo, tupange jinsi ya kuzipata kwa kutumia mtutu!”

“Maadam silaha zetu tunazo, basi tupange vizuri na siku hiyo tuwavamie! Na kwa vile ni mchoro, basi kuna uhakika wa kuzipata kirahisi…” Chuma anaendelea kuunga mkono. “Mpaka sasa hivi andikeni kuwa tumeshapata!” Benard anawaambia ili kuwapa moyo! “Tunakuamini mkuu…” “Ok, mipango mingine tutapanga tena tutakapokutana katika chumba chetu cha siri kule Ubungo Kibangu…” “Hakuna shaka.” Wanaendelea kupanga mpango wao kabambe hadi wanamaliza kuupanga.

Hata hivyo, wanaendelea kunywa vinywaji huku wanaongea hili na lile katika maongezi mengine tofauti na ya kikazi. Wanapomaliza vinywaji vyao, wote wanaagana na kila mmoja anachukua usafiri wa teksi anaelekea nyumbani kwake.

Lakini Benard harudi nyumbani kwake, mtaa wa Tabora, Ilala, bali anaelekea kwenye kituo cha teksi ambacho hakiko mbali sana na Hoteli ya Zebra Inn. Ni mwanzoni mwa mtaa wa Libya, baada ya kufika anaiendea teksi moja kati ya teksi zinazopaki hapo, ambayo ni ya jamaa yake anayemfahamu. Mara nyingi huzoea kuikodi anapokuwa katika shughuli zake za halali na zisizo za halali.
Dereva huyo anajulikana kwa jina la Makwanja. Amesimama nje ya teksi akisubiri wateja, na pia anaangaza macho kwa kila mpita njia anayepita. Ndipo anapomwona Benard anaijongelea gari yake kwa mwendo wa taratibu. “Ohooo…Ben…karibu…” Dereva Makwanja anamwambia. “Ahsante sana Makwanja...” Benard anasema huku anaufungua mlango wa mbele. Anaingia ndani. Makwanja naye anaingia garini na analitia moto.

 

Itaendelea

Hadithi hii huchapwa kila Ijumaa katika gazeti lako, HabariLeo.

Gwiji la Habari

 

 

NATAKA niwe mkweli kwa nafsi yangu kuwa, hata kama tungekuwa ...

foto
Mwandishi: Patrick Massawe

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi