loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tamasha la Urithi Wetu linavyolinda utamaduni

“KWA hiyo hatuna haja ya kwenda kuwaona Wadatoga kwao? Tutaweza kuonana nao hapa hapa Karatu?” Hili ndilo swali alilouliza mmoja wa watalii alipofahamishwa kuwa, Tamasha la Urithi liko mjini Karatu na yeye baada ya kutoka Ziwa Manyara jioni ile, angeweza kufahamu zaidi kuhusu maisha ya watu wa kabila la Wahadzabe akitembelea tamasha hilo linalofanyika katika viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu.

Tamasha la Urithi Wetu linalofanyika kwa mwaka wa pili sasa baada ya kuzinduliwa mwaka jana, ni tamasha linalolenga kwenda katika mikoa tofauti kwa lengo la kupeleka salamu mbalimbali za kuenzi, kudumisha utamaduni na kuvutia watalii kuona mambo anuwai yaliyopo nchini yakiambatana na dasturi zetu. Tamasha hili ambalo mwaka huu lilipoanza Dar es Salaam lilichanganywa na JamaFest la Afrika Mashariki, ni mwisho wa ubishi kwani limekusanya watu wengi katika zama ya kujitambua na siyo kuenzi tu, bali kuuza tamasha kama sehemu ya huduma za utalii.

“Hii ndio nia halisi ya tamasha hili, na kwa kweli imetudhihirishia wazi kuwa dhana ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya kupanua mazao ya utalii kwa kutumia utamaduni, inaanza kuleta manufaa,” anasema Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo.

Katika Tamasha la Urithi lililofanyika Karatu matukio yaliyotia fora ni maonesho ya mila na jadi za Wahadzabe na Wadatoga, wamiliki wa tamaduni za kale ambazo zinaenziwa duniani kwa utambulisho wake wa elimu na ufanisi wa tamaduni za Kiafrika.

Ujuzi wa uwindaji na utafutaji maji wa Wadatoga na Wahadzabe na ufahamu wao wa elimu ya nyota, ni moja kati ya urithi mkubwa walio nao kupitia tamaduni na mali kale za Tanzania. Vyote vinadhihirishwa katika sanaa mbalimbali zilizokuwepo katika maonesho hayo.

Akizungumzia umuhimu wa sanaa na mali kale za Tanzania, Mkurugenzi wa Sanaa, Joyce Fissoo, aliyehudhuria tamasha hilo anasema: “Wasanii ni warithi wakubwa wa tamaduni zetu na ndio walinzi wa urithi wetu.”

Alikuwa akimaananisha kwamba kupitia sanaa, maisha na utamaduni wa Mtanzania yanaendelea kuwapo. Tamasha la Urithi ambalo wiki hii litakuwepo Bagamoyo, Dodoma, Geita na kuhitimishwa Mwanza baadae lina kila aina ya utamu ambao mtu anauhitaji hasa kizazi cha sasa ambacho hakijaelewa hasa urithi nini. Tamasha hili limeshafanyika Kigoma ambapo mengi yalielezwa kama ilivyokuwa Karatu.

Kiukweli makabila ya Wahadzabe, Wairaqwi, Watatoga na Wamasai yenye sifa duniani kwa kuthamini na kutunza tamaduni halisi za Kiafrika ni sehemu nzuri ya taifa la Tanzania kujiangalia na kujitathmini.

Kwa kusikiliza kauli ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe katika ufungaji wa Tamasha la Urithi mjini Karatu, utaona kwamba ametoa angalizo zuri kwa makabila mengine mengi nchini kuona namna gani urithi wa kikabila unaweza kuwa sehemu ya utamaduni wa nchi na pia kuwa chnzo cha maarifa zaidi katika jamii.

Alisema tamaduni na jadi za makabila hayo ambazo ziliangaziwa na kupewa kipaumbele katika maonesho ya Tamasha la Urithi mwaka huu yalitokana na umuhimu wake kwenye mambo ya mazingira na utalii na kwa kukuza na kuendeleza mazao ya kiutamaduni pia taifa linaongeza mazao mapya ya utalii.

“Ni matarajio ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa tamasha hili;Urithi Festival, itazalisha matunda mema ya kuufanya utamaduni kuwa zao la utalii na kutuongezea idadi ya wageni kwa Tanzania na wilaya yetu hivyo, kukuza uchumi wetu kwa kupanua wigo wa biashara za utalii, kuwapa fursa wasanii, wasindikaji wa vyakula vya asili kutengeneza masoko ya bidhaa zao.,” anasema Waziri Mwakyembe.

Anaongeza kuwa, tamasha limeonesha wazi kuwa, upo wigo mpana zaidi wa kuwekeza katika utalii na kuzitaka sekta binafsi kuchangamkia fursa zilizopo ambazo ni zaidi ya kampuni za kupokea watalii na hoteli “Vivutio vya utalii vinavyoangazia malikale ni sehemu ambayo bado inahitaji uwekezaji mkubwa.

Kuna fursa nyingi pia katika uwekezaji unaolenga watalii wa aina fulani maalum,” anasema na kutoa mfano wa mikutano ya kimataifa, michezo, malikale za kihistoria, jadi na utalii wa rika tofauti. Kinachotakiwa ni ubunifu katika kutafuta na kuendeleza fursa nyingi zilizopo nchini,” anasema.

Kiukweli, ukiangalia mambo yanayoendelea katika Tamasha la Urithi, utaona chachu ya kukuza, kulinda na kutangaza utamaduni na malikale za Tanzania na kuvigeuza kuwa zao la utalii. Tamasha hili litawaweka Watanzania pamoja zaidi na kudumisha umoja, utaifa na uzalendo kwa nchi yao. Oktoba 13, mwaka jana, wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifunga tamasha za Urithi lililofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015/2020, inaitaka serikali kuongeza msukumo katika kukuza utalii na kutangaza vivutio vyetu vya utalii vikiwemo utamaduni na malikale na uwepo wa Tamasha la Urithi ni kutekeleza ilani hiyo.

“Mtakubaliana nami kwamba, tunapaswa kuendeleza mila, tamaduni na desturi zetu kwani ndizo kichocheo muhimu cha uzalendo tulio nao hususan katika suala zima la maadili. Vilevile, utamaduni ni zao la uhakika kwenye sekta ya utalii na ukarimu.”

Anasema thamani ya utamaduni mara nyingi imekuwa ikionekana kwenye sekta nyingine kama elimu, afya, michezo, kilimo, viwanda na maendeleo ya jamii. Anatoa rai kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, wadau wote wa utalii hususani sekta binafsi na wananchi kwa jumla washirikiane katika kulinda, kutunza, kutangaza na kuendeleza vivutio vya utalii nchini Mwaka huu tamasha likiwa linafungwa Mwanza, Novemba 2 inafaa kukumbusha pia kwamba, mwaka jana lilitolewa agizo na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan la kuzitaka Wizara ya Maliasili na Utalii; Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mkoa wa Dodoma, kutenga eneo mahususi litakalotumika kwa ajili ya Tamasha la Urithi kila mwaka kitaifa mkoani Dodoma. Makamu wa Rais alitoa agizo wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo Septemba 15, 2018 jijini Dodoma.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Suzan Mlawi akizungumzia Tamasha la Urithi anasema taifa lisilo na utamaduni ni taifa lililokufa na kupoteza rasilimali husika kwani utamaduni ni kivutio kibwa cha utalii.

“Tusipoenzi na kuzitunza tamaduni hizo, utu wetu na rasilimali zetu zitapotea, kwani utamaduni wetu ni kivutio kikubwa cha utalii,” anasema Suzan.

Tamasha linaendelea na linakumbusha mambo mengi ya kimila na asili ya Mtanzania kwa makabila yao kuanzia maisha ya kila siku ya tamaduni za makabila, ndoa, vyakula na muziki wa asili vitu ambayo vijana wengi wa sasa hawana historia navyo, lifuate kujishibisha zaidi.

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi