loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ningekuwa Muhenga ningebadili methali

MAKALA haya yanaelezea jinsi baadhi ya maana za methali zinavyopotosha wanajamii kwa kuamini kwamba ujumbe unaotokana na methali hizo ni ujumbe wa moja kwa moja.

Hivyo ukiukosoa ni sawa na umevunja sheria za wahenga kwani methali siku zote tunajua ni kauli za wahenga ambao kwa kiasi kikubwa wanaaminika sana ndani ya jamii kutokana na busara na hekima walizojijengea.

Lakini ikumbukwe kuwa katika jamii kuna makundi mbalimbali ya watu wenye marika tofauti na kuendelea kuamini ujumbe unaotoka kwa wahenga bila ya kuwasahihisha au kuwakosoa vizazi vijavyo vitakuja kuangamia ukizingatia dunia sasa ni ya utandawazi. Makala haya pia yanatoa pendekezo la matumizi sahihi ya methali hizi ndani ya jamii kwani zile za mwanzo zinaonekana kupitwa na wakati.

Kwa kuanza tuone maana ya methali kutoka Kamusi Kuu ya Kiswahili; ni usemi wa kimapokeo wenye kutoa kauli kimafumbo na kimuhtasari kama njia ya kusisitiza, kuelimisha au kuonya na kupongeza kwa njia ya busara. Zifuatazo ni baadhi tu ya methali ambazo kwa namna moja au nyingine maana zake hupotosha jamii.

Aliye juu, mgonje chini; Maana ya methali hii ni kwamba mtu aliye juu kama vile juu ya mti au mlimani usihangaike kumfuata msubirie chini kwani lazima atashuka. Pia methali hii ina maana kwamba mtu tajiri na asiye tajiri kamwe hawawezi kuwa sawa. Jambo la msingi ni kumsubiria hadi afilisike ndipo mkutane na yeye.

Methali hii ina upotofu ndani ya jamii kwani kusubiria mtu chini unaweza ukachoka na ukakata tamaa. Aidha, mtu kufikia hatua ya kufilisika sio rahisi kwani matajiri wengi huendelea kuwa matajiri kwa kurithishana mali. Pendekezo la methali hii ni “aliye juu mfuate hukohuko” kwa sababu ukiendelea kumsubiria chini utapoteza muda wako. Mtoto akililia wembe, mpe umkate; Maana ya methali hii ni kuwa mtoto mdogo huwa na kawaida ya kulilia vitu vingi vibaya au vizuri.

Hivyo watu wanaitafsiri methali hii kuwa mtoto akililia wembe mpe akijikata atajua mwenyewe. Aidha, maana yake mtu aking’ang’ania jambo hata kama ni baya mwachie tu akipata madhara shauri yake. Upotoshaji wa methali hii ndani ya jamii ni pale inapotumika huku watu wakijua fika madhara ya mambo yatakayompata kwa sababu jambo linaonekana wazi lina madhara lakini bado unamwacha mtoto au mtu apatwe na madhara hayo.

Ni sawa na kukusudia kufanya jambo fulani ambalo ni kosa kisheria. Pendekezo la methali hii ni kwamba “mtoto akililia wembe usimpe” Riziki hupangwa na Mungu; Maana ya methali hii ni kwamba neema na baraka hutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Methali hii inapotosha wanajamii kwani inahamasisha uvivu na umwinyi ndani ya jamii kwa kudhania kuwa hata usipofanya kazi ipo siku Mungu atakupatia riziki yako. Watu wengi hupotoka na kukaa bila kujishughulisha na kazi wakitegemea mgao kutoka kwa Mungu. Jambo ambalo linazidi kuwaweka watu katika umaskini au hali duni ya maisha kwa kizazi hadi kizazi.

Pendekezo la methali hii ni kuwa “riziki hutokana na kufanya kazi kwa bidii” Polepole, ndio mwendo; Maana ya methali hii ni kwamba siku zote anayetembea taratibu ndiye anayekwenda. Aidha, kufanya kazi kwa umakini bila ya pupa ni vizuri zaidi kwani itakamilika kwa ufasaha.

Methali hii inaleta taswira hasi ndani ya jamii kwani watu wengi huaminishwa na methali hii na baadaye kuchelewa vitu vya msingi kwa kufanya jambo polepole kama vile kuchelewa kazini, kuchelewa usaili, kuchelewa basi na kadhalika. Pia, katika maana nyingine inategemeana na aina ya kazi kwa mfano katika mashindano ya riadha huwezi kutumia akili sana na itakubidi ufanye jambo haraka au upesi sana ili kushinda mbio. Pendekezo la methali hii ni kwamba “polepole na harakaharaka vyote ni mwendo”.

Mtoto wa nyoka ni nyoka; Maana ya methali hii ni kwamba nyoka ambaye ni kiumbe hatari siku zote huzaa nyoka. Pia, mtoto hurithi tabia alizonazo mzazi wake mathalani kama mzazi ni mwizi, malaya, mzinzi au jambazi mtoto lazima awe na tabia alizonazo mzazi wake. Methali hii inapotosha watu kwa sababu kuna wakati mzazi kweli ni jambazi lakini wanajamii wanamhukumu mtoto kwa sababu baba yake alikuwa jambazi kwa kudhani kuwa mtoto naye atakuwa jambazi. Jambo hili huweza kufika wakati mtu kushukiwa ni mwizi hata kama hajaiba, kwa sababu tu mzazi alikuwa jambazi.

Vilevile, mzazi anaweza akawa mcha Mungu lakini mtoto akaja kuwa jambazi au tapeli. Pendekezo la methali hii ni kuwa “mtoto wa nyoka ni nyoka lakini sio kila nyoka hudhuru” wengine hutumika hata kuchezea ngoma. Siku za mwizi ni arobaini; Maana ya methali hii ni kwamba mtu huweza kufanya maovu kwa muda mrefu bila kujulikana lakini ipo siku lazima atabainika tu.

Methali hii hupotosha jamii hususani kundi la watoto ambalo halijui maana fiche ya methali hii wakidhani huwezi kukamatwa ukiiba siku ya kwanza mpaka zifike siku arobaini jambo ambalo sio kweli kwani unaweza ukakamatwa siku ya kwanza tu utakapoiba. Pendekezo la methali hii liwe “siku za mwizi ni kukamatwa kwake” Mkamatwa na ngozi ndiye mwizi; Maana ya methali hii ni kwamba mtu aliyekutwa na kitu kilichoibwa yeye ndiye aliyeiba hata kama yeye hakuiba kwani ndicho kithibitisho.

Methali hii ina potosha jamii kwa sababu sio kila mtu mwenye kukamatwa na ngozi ni mwizi. Inawezekana mtu kwa kutaka kumkomoa mtu mwingine akaiba kitu sehemu Fulani na akaja nyumbani kwako akakiacha kitu hicho, pia kuna watu wengi huvalishwa ngozi na wanajamii bila ya kufanya utafiti kwa kupewa kifungo palepale mathalani watu wengi hubambikiziwa kesi za wizi lakini katika mazingira ya kawaida walengwa ni watu wengine kabisa. Pendekezo la methali hii ni kuwa “mkamatwa na ngozi ndiye mwizi lakini wapo wanaosingiziwa.”

Kufa kufaana; Maana ya methali hii ni kwamba mtu akifa huwa ni furaha kwa wengine kama wauza majeneza, sanda au hata walala hoi ambao hufaidika na chakula kinachopikwa msibani. Pia mtu anapopata matatizo watu wengine hufaidika kupitia matatizo yake kama vile mtu akifukuzwa kazini mwingine hukaimu au kupewa nafasi hiyo. Methali hii inapotosha jamii kwani matatizo ya mtu sio vizuri kufurahia kwa sababu huwezi jua ya kesho na methali hii ni moja ya methali inayosababisha migogoro mingi sana ndani ya jamii. Pendekezo la methali hii ni kwamba “kufa kamwe si kufaana”.

Mwisho wa makala haya ninapendekeza mabadiliko ndani ya jamii yaende sambamba na mabadiliko ya methali kwani kuna methali zimepitwa na wakati na bado zinaendelea kutumika. Hivyo ningekuwa muhenga ningefanya mabadiliko ya methali zilizopitwa na wakati ili kuzifanya ziendane na wakati.

Mwandishi ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) anayefanya mazoezi Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita). Anapatikana kwa:+255782416744, +255675153838 na bakaryhery1993@ gmail.com

foto
Mwandishi: Bakary Shabani

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi