loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

CHINA KWA MACHO YANGU: Uhusiano kati ya maendeleo ya kushangaza ya China na ustawi wa mfumo wa elimu ya msingi

“MUSTAKABALI wa Taifa umejikita katika elimu. Elimu ni jiwe la msingi la uhuishaji wa taifa na maendeleo ya jamii.

”Aya hii ipo katika Mpango wa Kitaifa wa Maendeleo ya Elimu ya China. Katika muhtasari huo, Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kimeahidi kuipa elimu kipaumbele na kugeuza taifa la China kuwa nchi tajiri katika suala la nguvukazi.

Kwa hakika, chama tawala pamoja na serikali vimeipa elimu thamani ya juu . Tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, vizazi vya uongozi wa CPC kuanzia enzi za Mao Zedong, Deng Xiaoping, Jiang Zemin, Hu Jintao na Rais wa sasa Xi Jinping, vimemakinika na kufanya kila juhudi kuhakikisha kuwa mamilioni ya Wachina wananufaika na haki ya kupata elimu. Leo hii, China ina mfumo mkubwa zaidi wa elimu duniani.

Ni mfumo ambao unawaelimisha takriban vijana 300,000,000, na kuwaajiri walimu zaidi ya 20,000,000. China ni taifa lenye raia wengi sana. Kutokana na hali hii, usawazishaji wa maendeleo ya elimu katika maeneo ya vijijini na mijini daima ungekuwa changamoto kubwa. Katika siku za mwanzo punde tu baada ya kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949, takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha kutojua kusoma na kuandika katika taifa hilo kilikuwa asilimia 80. Iwapo nchi hiyo ilinuia kuwa na nafasi yoyote ya kujiendeleza, basi haikuwa na budi ila kuwaelimisha raia wake.

Miaka ya 1980 iliashiria mwamko mpya nchini China, huku kukiwa na enzi mpya ya mageuzi ya elimu, yenye sifa ya uwajibikaji na kujitolea kwa uongozi wa nchi hiyo. Ili kuhakikisha kuwa raia wote wa China wanapata elimu, chama tawala cha CPC kilizindua mpango wa kubadilisha muundo wa elimu kwa kuanzisha elimu bure na ya lazima kwa raia wote hadi watakapotimia umri wa miaka 15.

Mpango huo ulipanuliwa kwa haraka na kutekelezwa katika maeneo yote ya nchi. Katika China ya leo, wanafunzi lazima wakamilishe miaka tisa ya elimu ya lazima bila malipo. Wanafunzi wengi wanachukua miaka sita katika shule ya msingi. Hii inafuatiwa na miaka mitatu ya elimu ya sekondari ya chini maarufu kama ‘junior secondary’. Serikali iliondoa mfumo wa kushiriki mitihani ili kuhakikisha kuwa raia wote wanasajiliwa kufikia kiwango hiki cha elimu.

Tangu kuzinduliwa kwa mageuzi haya, upeo wa elimu nchini China ulizidi kupanuka hadi kufikia huu wa leo. Viwango vya kutojua kusoma na kuandika baina ya watu wenye umri wa miaka 15 vimeshuka kutoka asilimia 80 hadi asilimia tano pekee. Katika mwaka 2014, kwa mfano, data kutoka taasisi ya takwimu ya UNESCO, UIS, zilionesha kuwa idadi ya wanafunzi walioandikishwa elimu ya msingi iliongezeka kwa asilimia 103.

Kiwango cha wale waliojiunga na elimu ya sekondari ya chini nacho kilikuwa kwa asilimia 94 kikilinganishwa na asilimia 64 mwaka 2006. Bila shaka, mpango wa elimu ya msingi nchini China umekuwa ukipanuka kwa haraka. Kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za serikali kuhusu mafanikio ya elimu ya China mwaka 2017, idadi ya shule za chekechea, msingi na sekondari ilifikia 498,500 mwaka 2017, kutoka 436,400 mwaka 2010. Idadi ya wanafunzi walioandikishwa shule ikafikia takriban 204,000,000, ikilingalishwa na 176,000,000 mwaka 2010. Tathmini ya karibu inaonesha kwamba China tayari imeandikisha historia katika kuendeleza mfumo wake wa elimu ya msingi, kwa kutoa elimu yenye ubora na kwa usawa kwa watoto wote wa umri wa kwenda shule, pamoja na kuandaa walimu wenye ushindani mkubwa kote nchini. Aidha, serikali yenye makao yake jijini Beijing, imekuwa ikiwekeza rasilimali nyingi kwenye sekta ya elimu kutoka kwenye pato la taifa.

Takwimu za Wizara ya Elimu zinaonesha kuwa bajeti ya elimu iliongezeka kwa asilimia 10 mwaka 2017 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha uwekezaji katika elimu, shule mpya 300,000 zimejengwa, wanafunzi 30,000,000 kuandikishwa, na walimu 2,000,000 kuajiriwa kutoka 2013 hadi 2018.

Kuongezeka kwa bajeti ya elimu pia kumesaidia kuinua viwango vya elimu katika maeneo ya vijijini na kuviweka nafasi sawa na vile vya mijini. Ili kuhakikisha kwamba elimu ya lazima inapatikana kwa watoto wote, serikali iliwaondolea wanafunzi wote wa vijijini ada zote za shule tangu mwaka 2006. Msamaha huu umewafaidisha mamilioni ya wanafunzi. Serikali pia imesambaza vitabu vya kusoma kwa wanafunzi wote wa vijijini bila malipo.

Zaidi ya hayo, serikali inatoa misaada ya kujikimu kwa wanafunzi kutoka familia zisizojiweza kiuchumi. Katika Yunnan Mkoa wa mpakani uliopo Kusini Magharibi mwa China, kwa mfano, msaada hutolewa kwa wanafunzi kutoka familia zilizosajiliwa chini ya Mtandao wa Kitaifa wa Kupambana na Umasikini ili kuhakikisha kuwa wako shuleni nyakati zote.

Mfumo wa Uboreshaji wa Lishe ya Bure kwa Wanafunzi pia umetekelezwa kote nchini, na kwa sasa umewafaidisha zaidi ya wanafunzi 36,000,000 wa vijijini.

Na kutokana na maendeleo ya teknolojia katika miaka ya hivi karibuni na kuongezeka kwa upatikanaji wa intaneti, serikali imeweka mpango mahsusi wa kupanua upatikanaji wa rasilimali za kufundishia za dijitali wakati wote zikiwemo tovuti za kufundishia. Programu hizi ni vyombo muhimu kwa ajili ya kuboresha masomo katika maeneo ya vijijini, kwa vile vinawawezesha walimu wa vijijini kupata rasilimali za kutoa elimu kwa wanafunzi.

Walimu wenye ushindani

Baada ya kutenga kitita kikubwa cha fedha kufadhili elimu, serikali ilielekeza macho na nguvu zake na kutoa kipaumbele kwenye ujenzi wa nguvu kazi ya walimu wenye tajiriba ya juu. Serikali Kuu ilizindua sera mfululizo kwa ajili ya kuwajengea uwezo walimu wa vijijini. Mpango huo wa kutoa msaada kwa walimu wa vijijini wa mwaka 2015- 2020, hasa, unabainisha kiwango cha ruzuku na posho itakayotolewa kwa walimu katika shule za vijijini, mipango ya fidia ya malipo kwa walimu wa mijini na vijijini, uhamisho wa mara kwa mara kwa walimu kutoka shule za mijini hadi vijijini, miongoni mwa motisha nyingine zilizotolewa kwa walimu wanaofundisha vijijini.

Sera hii ya utoaji posho imewanufaisha mamilioni ya walimu hasa katika maeneo ya vijijini, ikiwa ni pamoja na wale wanaofanya kazi katika maeneo ya mbali yasiyo na maendeleo. Mamilioni ya nafasi maalumu za walimu wa kutoa mafunzo zimeundwa katika mchakato wa kuongeza rasilimali za elimu kwenye maeneo ambayo umasikini umekithiri.

Zaidi ya walimu 20,000,000, wakiwemo walimu wote wanaofanya kazi katika maeneo ya vijijini, wamepokea masomo chini ya Mpango wa Mafunzo ya Walimu wa Kitaifa wa Mwaka 2010. Walimu wa vijijini sasa wanashikilia nafasi nzuri katika jamii kuliko hapo awali pamoja na kutunukiwa fursa zaidi za kuendeleza taaluma zao.

Katika hati ya sera ya kihistoria iliyotolewa Januari 2018, Serikali Kuu iliahidi kubadili mtazamo kuhusu taaluma ya ualimu na kuifanya iwe kazi inayovutia zaidi.

Ili kuendeleza ubora wa walimu, serikali pia ilianzisha mchakato wa walimu kuchukua upya vyeti vya mafunzo. Ndani ya muundo huu, kila mwalimu wa shule ya msingi, sekondari na ufundi lazima asajili upya vyeti vyake vya kufuzu kila baada ya miaka mitano. Walimu ambao wangeshindwa kujisajili upya kwa wakati, wangepoteza nafasi zao za kufundisha.

Mageuzi ya mtaala wa elimu

Tangu mwaka 2012, China imejihusisha na mageuzi ya kimsingi ya elimu ili kukuza maendeleo ya wanafunzi kwa kila hali. Wizara ya Elimu ilianza kutekeleza mpango ambao ulibadili utoaji wa mafunzo darasani kwa wanafunzi kwa ajili ya kupata maarifa pekee na kufanya masomo kuwa ya kushinikiza umuhimu wa fikra chanya, na maadili ya msingi ya ujamaa. Katika mpango huu, mkazo uliwekwa katika maendeleo ya kimaadili, kiakili na kimwili kwa wanafunzi ili kukuza maadili, nidhamu, utamaduni, na wema.

Mabadiliko mengine yaliyotekelezwa hivi karibuni yanalenga kutimiza mahitaji tofauti ya wanafunzi, na kuwapa uhuru zaidi wa kuchagua taaluma wanayotaka kujifunza. Bila shaka, maendeleo ya elimu yameimarisha ubora wa taifa lote, na kuchochea ubunifu zaidi katika sayansi na teknolojia, hivyo kutoa mchango muhimu katika ukuaji wa uchumi wa China, maendeleo ya jamii, na kuboreshwa kwa maisha ya kila siku ya raia wote.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: MWANDISHI MAALUM

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi