loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mikakati ya China katika kupambana na maambukizi ya Ukimwi na unyanyapaa kwa watu walioathirika

JANGA la UKIMWI nchini China ni hadithi ambayo ni ya kipekee mno. Mgonjwa wa kwanza kuwahi kutambulika mwaka 1985 kuwa na maradhi ya ugonjwa huo nchini humo hakuwa mwenyeji ila mgeni.

Ugonjwa huo baadaye ulipatikana katika bidhaa za damu kutoka mataifa ya nje, na hivyo kuipa nguvu imani ya kwamba virusi hivyo viliingizwa China kutoka nje ya mipaka yake. Matokeo yake ni kwamba Ukimwi ulionekana kama ugonjwa sugu ulioenezwa kutokana na kuwasiliana na mataifa ya nje na hivyo Serikali ya China iliweka mikakati ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kuingia nchini humo.

Viongozi wa nchi waliahidi haraka kuhakikisha kuwa hakuna mtu ambaye angeambukizwa maradhi hayo hasa kupitia njia ile. Kanuni hizo zilianza kufanya kazi mara moja na hii ilimaanisha kuwa wageni ambao walikusudia kukaa mwaka mmoja au zaidi pamoja na wakazi wa China wanaorejea kutoka mataifa ya nje ilibidi wapimwe virusi vya Ukimwi.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, matokeo zaidi ya kitaifa yamemaanisha kwamba kiwango cha maambukizi mapya kimepungua kutokana na kuboreshwa kwa maisha ya watu wanaoishi na virusi hivyo.

Mwaka 1998, serikali ilitoa Mpango wa Miaka 13 wa Kuzuia na Kudhibiti Ukimwi, ambao una lengo la kuhakikisha waathiriwa wa ugonjwa huo hawazidi watu 1,500,000 katika nchi hiyo yenye watu karibu bilioni 1.4. Mwaka uliofuata, Wizara ya Afya ilitoa mwongozo wa kiusimamizi, ukisisitiza kulindwa kwa haki za watu walioambukizwa virusi.

Maofisa wa Afya walibaini kwamba idadi ya watu wanaoishi na maradhi hayo iliongezeka baada ya miaka kadhaa. Hata hivyo iliibuka dhana kuwa watu wengi waliambukizwa kwa njia ya ngono. Pia iliibuka dhana kwamba wasambazaji wakuu wa virusi hivyo walikuwa wale wanaochangia sindano hasa watumiaji wa dawa za kulevya pamoja na matatizo yatokanayo na uchangiaji wa damu.

Maambukizi mengine yaliripotiwa miongoni mwa wanaume wanaojamiiana na wanaume wenzao. Janga hilo limebadili mwenendo kutoka kwa watumiaji wa dawa za kulevya na kuwa jambo la kuogopewa na wananchi wote. Katika mwaka 2014, asilimia 92 ya maambukizi mapya ilipatikana kwa njia ya ngono.

Na jinsi vijana wanapozidi kuwa na uhuru wa kujichagulia wanachotaka, ndivyo ilivyo mtazamo wao kuhusu ngono kabla ya ndoa. Wale wanaofanya biashara ya ukahaba pia ni sehemu muhimu zaidi ya utafiti wa jinsi Ukimwi ulivyo katika China.

Utafiti uliofanywa mwaka 2014 na Kituo cha Kitaifa cha China cha Ukimwi ulikadiria kuwa asilimia 60 ya watu wenye ugonjwa wa Ukimwi ni wale ambao wamekuwa na athari za virusi hivyo kupitia biashara ya ngono. Kufikia sasa hakuna idadi kamili ya wale wanaofanya ukahaba nchini China.

Lakini wengi wanakadiria kwamba kuna watu elfu kadhaa wa kundi hili ingawa biashara hiyo ni kinyume cha sheria nchini China. Ni kutokana na hali hii ndipo uongozi wa kisiasa nchini China umekuwa ukiahidi kila mara kuimarisha juhudi za kuzuia na kutibu maambukizi ya Ukimwi, pamoja na kutambua kwamba hii ni sehemu muhimu ya afya ya umma.

Baada ya uamuzi huu wa kihistoria, matibabu, utunzaji na usaidizi kwa wale walioathirika umekuwa wazi. Idadi ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi ambao wako katika matibabu pia imeongezeka kwa kasi.

Mnamo Disemba 2003, China ilianzisha sera ambayo ingewawezesha waathiriwa kupata dawa za bure za ARV, kuzuia kuenezwa kwa ugonjwa huo kutoka kwa mama hadi mtoto, utoaji wa ushauri nasaha na upimaji wa bure, utoaji wa masomo bila malipo kwa watoto walioachwa yatima baada ya wazazi wao kufa kutokana na ugonjwa huo, pamoja na huduma za utunzaji kutolewa kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi. Mpango huu umepanuliwa na kusambazwa kufikia maeneo zaidi ya 120 kote nchini China.

Sehemu ya watu ambayo imeathirika sana kutokana na ugonjwa huu ni vijana. Kituo cha Kitaifa cha Kudhibiti Maambukizi ya Ukimwi nchini China kilizin dua ripoti iliyoonesha kuwa asilimia 15 ya maambukizi mapya mwaka 2015 yalikuwa kati ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 24.

Licha ya takwimu hizi kuonekana ndogo, kuna ongezeko la wasiwasi kuhusu madhara ya janga la Ukimwi kwa kizazi hiki chenye umri mdogo. Huku ikitambua umuhimu wa elimu inayotokana na masomo ya kijinsia, China imebuni na kutekeleza sheria na sera mbalimbali katika miongo minne iliyopita. Idadi kubwa ya huduma za Ukimwi na elimu hasa inayolenga vizazi vya watu wenye umri mdogo vinavyoathirika vilianzishwa kwa haraka.

Watoto na vijana sasa wanafundishwa vipengele vya elimu ya ngono shuleni. Mwaka 2016, katika jitihada za kupambana na kuongezeka kwa maambukizi mapya ya Ukimwi miongoni mwa vijana, China ilichukua hatua mwafaka na kutangaza kwamba wanafunzi wa shule ya kati na sekondari walikuwa wanatakiwa kuhudhuria madarasa ya elimu juu ya ngono.

Mwaka 2017, China iliendelea kufanyia majaribu juhudi za kuzuia maambukizi ya Ukimwi katika vyuo vikuu, huku ikishirikisha mpango wa kutoa masomo kuhusu virusi vya Ukimwi katika mtaala wake. Zaidi ya hayo, China inahimiza raia wake kutambua hali yao ya Ukimwi kwa kupimwa na tayari imesajili mafanikio katika kuimarisha juhudi za kutoa ushauri na kupimwa kwa Ukimwi katika miaka ya hivi karibuni.

Kati ya mwaka 2008 na 2017, idadi ya vituo vya kupima Ukimwi iliongezeka kutoka 7,600 hadi 30,500. Idadi ya watu wanaopima hali zao za ugonjwa huo kwa mwaka iliongezeka kutoka 45,000,000 hadi 201,000,000.

Na kutokana na watu kuukumbatia mwito wa kupimwa, idadi ya maambukizi mapya iliyoripotiwa iliongezeka kutoka 56,350 hadi zaidi ya 134,500.

Katika mwaka 2017, utafiti ulionesha kuwa mbinu ya watu binafsi kujipima na kujua hali zao za Ukimwi ni jambo ambalo linapokelewa vyema na kuonesha uungwaji mkono kutoka kwa wale wanaougua ugonjwa huo.

Mbinu hii inalenga kubadili mwenendo wa utoaji wa matibabu ya Ukimwi, kupitia kwa kupunguza muda na idadi ya safari kuelekea hospitali au kliniki kwa ajili ya kupimwa au kuanzishiwa matibabu ya ugonjwa huoI.

Ni muhimu pia kutaja kuwa mipira ya kondomu imekuwa mingi zaidi nchini China katika mwongo mmoja uliopita. Hata hivyo, matumizi yake bado yako chini kwani idadi kubwa ya watu wanaichukulia kama njia moja ya kupanga uzazi.

Mwaka 2017, harakati nyingine zilizinduliwa katika jitihada za kutokomeza maambukizi ya Ukimwi ya Mama kwa Mtoto. Juhudi hizo zilichukua mwelekeo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) la kusaidia maendeleo ya mpango uliounganishwa ili kuondoa usambazaji wa virusi kutoka kwa Mama hadi kwa Mtoto, ugonjwa wa kaswende na homa ya manjano au Hepatitis B.

Hii imepelekea kupunguzwa kwa idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa na virusi hivyo kutoka asilimia 7 mwaka 2001 hadi asimilia 5 katika mwaka 2014. Kufikia mwishoni mwa 2017, kulikuwa na zaidi ya watoto 5,500 wenye umri wa chini ya miaka 15 walioathirika waliokuwa wakipokea dawa za kukinga makali ya maambukizi ya Ukimwi za ARVs.

Wakati huo huo, China inafuatilia kwa karibu mwongozo wa WHO wa mwaka 2016 unaopendekeza utoaji wa dawa kwa watu wote wanaoishi na virusi vya Ukimwi bila malipo bila kujali hesabu ya chembechembe ya CD4 mwilini.

Hii ndio sababu mwaka 2016, China iliahidi kutoa dawa za ARVs kwa watu wote wanaoishi na virusi vya Ukimwi ambayo iliongeza idadi ya wanaonufaika kupitia mpango huo kutoka asilimia 67 mwaka 2015 hadi asilimia 80 mwaka 2017.

Kufikia mwishoni mwa 2017, idadi ya watu waliokuwa wakipokea matibabu hayo ilikuwa 609,500, huku jumla ya watu 131,500 wakijiandikisha ili kufaidi kutokana na mpango huo kwa mara ya kwanza. Ama kwa kweli, kanuni mpya kuhusu virusi vya Ukimwi zilitolewa na baadhi ya mikoa ambazo ni pamoja na masharti kuhusu kuzingatia haki za watu wanaoishi na virusi hivyo.

Kwa mfano, katika jimbo la Yunnan kanuni zinazuia mtu yeyote kukataza matibabu kwa watu wanaoishi na maradhi hayo. Pia vitengo vinavyoshughulikia ajira vimezuiliwa kuwabagua watu wanaoishi na Ukimwi pamoja na wanafamilia wao. Katika China ya leo, sheria za nchi huwalinda walioathirika na unyanyapaa na ubaguzi kwa misingi ya kijinsia.

Katika miaka ya hivi karibuni, China imekuwa ikiongeza uwekezaji katika mpango wa kukabiliana na maradhi yanayotokana na Ukimwi.

Mwaka 2017, China ilitumia takriban dola za kimarekani bilioni 1 katika kukabiliana na maradhi ya Ukimwi hii ikiashiria ongezeko la zaidi ya asilimia 5 kutoka mwaka 2016. Mwaka 2015, serikali iliandaa hazina maalum ya kukabiliana na janga la Ukimwi nchini China kwa shirika lisilo la kiserikali ili kusaidia mashirika ya kijamii kushiriki katika kukabiliana na maradhi hayo.

Hili ni jambo la kutia moyo unapozingatia uendelevu wa mpango wa kukabiliana na Ukimwi kitaifa. Utafiti wa hivi karibuni unaonesha kwamba China iko njiani kutimiza malengo ya Shirika la Kupambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa (UNAIDS), ya 90-90-90.

Hii ni kwa sababu China imetenga rasilimali ambazo zinahitajika kwa minajili ya utoaji wa matibabu bora kwa waathiriwa wa Ukimwi. Pili taifa hilo limehakikisha upatikanaji wa rasilimali hizi ili kuzuia maambukizi mapya.

Mbinu ya China ya kushirikisha sekta mbalimbali kwenye vita dhidi ya Ukimwi, inayoleta pamoja serikali, asasi za kiraia na sekta binafsi inatoa funzo muhimu kwa nchi nyingine hasa kwenye suala la ushirikiano katika kila jambo ili kupata ufanisi.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi