loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tukiamua, maziwa ni ‘mgodi’ wenye fursa nyingi za ajira

WAHENGA waliwahi kunena ya kwamba, Mungu aliumba ardhi ili iwe makazi, chanzo muhimu cha maisha na ajira.

Ardhi ina umuhimu mkubwa wa kumlisha mwanadamu kupitia kilimo ambacho akimua kukifanya kuwa tegemeo la maisha, ndicho kinatajwa kuwa ajira nambari moja tangu kuumbwa kwa dunia.

Ni ardhi hiyohiyo iliyomfanya mwanadamu apate fursa nyingine ya ajira kupitia ufugaji wa wanyama wa aina mbalimbali. Ukweli huu ndiyo unaotoa tafsiri iliyo sahihi, kwamba kila binadamu anayeamua kujiajiri kupitia ardhi, anaweza akayamudu maisha kupitia shughuli za kilimo na ufugaji.

Mathalani, katika sekta ya ufugaji, kuna mifano mingi ya watu waliofanikiwa baada ya kuamua kurasimisha ardhi katika muktadha huo kwa ajili ya kujikimu kimapato. Katika jiji la Tanga, eneo la Pongwe, kuna kijana mmoja anayetoa ushuhuda wa namna ambavyo ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ulivyomwondoa katika fikra za kudhani kuwa, kila aliyebahatika kupata elimu ya kiwango cha juu ni lazima aajiriwe.

Huyu ni Albert Mmesa ambaye alimaliza elimu ya kidato cha sita mwaka 2015 jijini Tanga. Baada ya kuhitimu masomo yake akilini mwake alikuwa akifikiria jambo moja pekee, kutafuta kazi. Ilimchukua miaka mitatu ‘kusaga soli za viatu’ vyake akitafuta kazi kupitia mashirika na idara mbalimbali pasipo mafanikio hasa baada ya matokeo yake ya kidato cha sita kutokuwa mazuri sana.

Mwisho alikata tamaa, akaamua kubaki mitaani kwa kuishi maisha ya ‘bora liende’. Ilikuwa mwanzoni mwa 2018, aliposafiri kwenda katika jiji la Mombasa, nchini Kenya kumtembelea kijana mwenzake aliyemaliza naye kidato cha sita ambako ndiko alikopata darasa lililompa mwamko mpya katika maisha. Likamfanya aachane na mawazo ya kufikiria ajira rasmi za serikalini au katika sekta binafsi. Anasema John Kiambu, ndiye aliyekuwa mwenyeji wake ambaye tangu alipomaliza masomo yake mjini Tanga, aliamua kujikita moja kwa moja katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Hadi anatembelewa na Albert, tayari alikuwa na ng’ombe saba, ambao kila mmoja alikuwa ana uwezo wa kutoa maziwa lita kumi kwa siku. Hivyo kwa idadi hiyo ya ng’ombe, Kiambu alikuwa na uhakika wa kuzalisha lita sabini kwa siku, kiasi kilichotosha kumfanya awe anaingiza kiasi kikubwa cha fedha kupitia mradi huo wa ufugaji. Maisha aliyokuwa anaishi Kiambu na hata kiasi cha fedha alizokuwa anaingiza kwa siku (zaidi ya Sh laki moja kwa siku) ilitosha kuwa darasa kwa Albert aliyerejea jijini Tanga akiwa na wazo moja tu, kuwa mfugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Akitoa ushuhuda wake mbele ya waandishi wa habari wanaounda Kituo cha Habari dhidi ya Umasikini Tanzania (MeCAP), kijana huyu anasema hadi kufikia mwezi uliopita (Septemba 2019), Albert naye alikuwa na ngombe saba, ambao kwa mujibu wa maelezo yake anakamaua lita 70 za maziwa kwa siku. Waandishi wa MeCAP walikuwa katika ziara ya kuangalia namna sekta binafsi katika mkoa wa Tanga inavyochangia kuondoa umasikini kwa jamii.

Kwa sasa, Albert ni mmoja wa wanachama wanaounda Ushirika wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa katika mji wa Tanga wanaokusanya maziwa na kuyauza katika kiwanda cha kinachosindika bidhaa zitokanazo na maziwa cha Tanga Fresh. Sasa anauzungumzia ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kama mkombozi sahihi wa maisha yake na hana sababu tena ya kufikiria ajira.

Anasema kwa lita anazoziuza kila siku katika ushirika wao, ana uhakika wa kujiingizia Sh 140,000 na katika mwezi mmoja ana uhakika wa kupata takribani shilingi 4,200,000. Anasema nusu ya kiasi hicho cha fedha anazozipata zinatumika katika kununulia vyakula na gharama za matibabu ya ng’ombe anaowamiliki na kiasi kinachobaki ndicho mshahara wake.

“Ukibakiwa wastani wa Sh milioni mbili katika pato ninaloliingiza kwa mwezi inatosha kuuita ni mshahara. Hiki ni kipato kikubwa kwangu kwa kila mwezi. Ni zaidi ya mshahara ambao nisingeweza kulipwa hata ningepata nafasi ya kuajiriwa serikalini,” anasema.

Anaongeza kwamba sasa sekta ya maziwa ina fursa nyingi za ajira kwa kila anayeamua kuirasimisha. Katibu wa Chama cha Ushirika wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa kilichopo Muheza Tanga, Kudra Tindwa, anasema kupitia ushirika wao wenye wanachama 252, wameweza kumiliki kituo cha ukusanyaji maziwa na kuyauza katika kiwanda cha Tanga Fresh na wanachama kujipatia fedha. Anasema, jumla ya lita 2,600 hadi 3,000 hukusanywa kila siku na ushirika wao, ambapo kila mwanachama ana uhakika wa soko la maziwa anayoyazalisha.

“Kupitia ushirika huu, kila mfugaji ana uhakika wa soko la maziwa kupitia kampuni ya Tanga Fresh ambao ndiyo wadau wetu wakubwa kwa hapa mkoani Tanga,” anasema Tindwa.

Anasema pamoja na kuwa na uhakika wa soko, pia ushirika wao umekuwa dhamana kubwa kwa wanachama wafugaji pindi wanapotaka kukopa katika taasisi za kifedha, hasa kutokana na ukweli kuwa, kipato kinachotokana na uuzaji wa maziwa kinawafanya wawe na uwezo wa kufanya marejesho ya mikopo. Kwa upande wake, John Tesha ambaye ni mkazi wa Muheza na mwanachama wa ushirika huo anasema ufugaji umekuwa mkombozi sahihi kwa watu wanaotaka kujiajiri wenyewe.

Anasema, kwa upande wake anamiliki jumla ya ng’ombe kumi ambapo anakamua lita kati ya 20 hadi 30 kwa siku na kwamba ana uhakika wa soko la maziwa kupitia chama chao cha ushirika.

“Awali tulikuwa hatuna uhakika wa soko na wapi unakwenda kuuza maziwa. Lakini, ushirika umetuwezesha kupata soko ambako ni Tanga Fresh, ninajikuta ninafuga kwa malengo na kipato ninachokipata kinaniwezesha kujikimu kimaisha,” anasema Tesha.

Pamoja na uhakika wa soko, pia kuna suala la elimu, ambapo ushirika kwa kushirikiana na Tanga Fresh huwa wanaandaa semina kwa ajili ya kuwaongezea uelewa wa ufugaji bora na wenye manufaa, badala ya kufuga kwa mazoea. Meneja Mkuu wa Kiwanda cha usindikaji wa bidhaa za maziwa cha Tanga Fresh, Michael Karata anasema sekta ya maziwa inaweza kupunguza tatizo la ajira nchini na kwamba wafugaji wanaweza wakawa waajiri wakubwa kwa vijana wanaomaliza elimu za msingi na sekondari.

“Kama tukiamua kufuga kwa utaratibu wa kisasa na malengo, sekta hii ina nafasi kubwa ya kuwaajiri vijana wengi walioshindwa kuendelea bna masomo, kwa sababu ufugaji wa kisasa unahitaji watu wengi wa kutoa huduma kwa wanyama hawa.

“Kuna vijana wanaoweza wakatumika kama wahudumiaji wa ng’ombe, kuanzia wachungaji, wakata majani, wakamuaji na hata wanaokwenda kuuza maziwa kupitia vyama vya ushirika vya wafugaji,” anasema Karata.

Anasema wao Tanga Fresh pekee tayari wameshatoa ajira kwa zaidi ya Watanzania 2,000 kupitia bidhaa za maziwa wanayoyazilisha, ambapo, kati yao ni wale wanaotumika kuuza maziwa kwa njia ya rejareja mitaani.

“Kwa pale kiwandani pekee tuna wafanyakazi 120 na vibarua zaidi ya 1,000 achilia mbali wale wanaojiajiri kupitia uuzaji wa bidhaa zetu kote nchini, hivyo, sekta hii ina nafasi kubwa ya ajira kwa sababu ina wanufaika wengi,” anasema.

Anaiomba serikali kuitazama sekta ya maziwa kwa kujengea uwezo wa masoko ya uhakika, sambamba na kuongeza idadi maofisa ugani wa mifugo ili wafugaji wawe na mifugo bora zaidi.

“Sekta ya maziwa ina uwezo wa kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na pia ni mwajiri mkubwa wa kitaifa, kwa sababu mfugaji mmoja anayefuga kisasa ana uweza kuajiri zaidi ya watu kumi, hivyo kupunguza tatizo la ajira nchini,” anasema Karata.

Pamoja na kuwa chanzo cha ajira, pia sekta ya maziwa ni muhimili mkubwa wa uchumi wa nchi, kwa sababu taifa linahitaji watu walio na utimamu afya inayotokana na unywaji wa maziwa bora.

Kwa mujibu wa takwimu zinatolewa kila mara na Shirika la Afya la Dunia (WHO) kila mtu anahitajika kunywa lita 200 za maziwa kwa mwaka. Mwandishi wa Makala haya ni Mkurugenzi wa Kituo cha Habari dhidi ya Umasikini Tanzania (Me- CAP).

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Mawazo Lusonzo, MeCAP

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi