loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Viziwi wanavyoshirikishwa kuelekea uchumi wa viwanda

JAMII wakati wote inatakuwa kuwapa watu wenye ulemavu wa kusikia au viziwi haki zao za msingi ili kuwawezesha kuishi kama wengine. Miongoni mwa haki ambazo walemavu wakiwemo viziwi wamekuwa wazipata kwa upendeleo nchini ni pamoja na mikopo itokanayo na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri zote.

Walemavu hupata asilimia mbili ya ya fungu hilo tofauti na vijana na wanawake ambao hupata asilimia nne kwa kila upande. Fedha hizi hutolewa kama mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi vya wajasiriamali. Hatua hii inalifanya Taifa kutekeleza wajibu wake kwa walemavu ya kuwatambua na kuwajali. Katika jamii yetu, wakati mwingine hali ya mtu kuwa na ulemavu inaambatana na unyanyapaa unaotokana na mitazamo potofu au mila zilizopitwa na wakati.

Ni katika muktadha huo jamii huwaona walemavu kama watu tegemezi, wasio na uwezo hata wa kujisimamia wenyewe. Lakini ukweli ni kwamba kundi hili likiwezeshwa linaweza. Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 inasema mtazamo huu unasababisha kutengwa kwa watu wenye ulemavu katika maisha ya kila siku na jamii inayowazunguka. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza kwamba binadamu wote ni sawa na kwamba wanastahili kupata haki sawa bila kujali rangi, kabila, jinsi na dini.

Umoja wa Mataifa pia ulipitisha Azimio namba 27 (a) (III) ambalo linaeleza kwamba binadamu wote wamezaliwa huru wakiwa sawa katika haki na kustahili heshima. Kwa kadri ya azimio hili, binadamu, akiwemo mlemavu ana haki ambazo anastahili kuzipata kutoka kwa jamii na pia ana wajibu kwa jamii. Haki hizo ni za kuitumia jamii na rasilimali zake kwa ajili ya maendeleo na usalama wake. Licha ya azimio hili, Umoja wa Mataifa umepitisha maazimio kadhaa kuhusu haki na usawa wa fursa kwa watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali.

Ni kwa kulitambua hili, hivi karibuni Shirika la Viwango nchini (TBS) liliandaa mafunzo ya siku moja ya ujasiriamali kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kusikia kutoka mikoa ya Mbeya na Songwe. Mafunzo haya kwa baadhi ya watu waliyaona kama ya ajabu na huenda kidogo waliwashangaa waandaaji. Hii ni kutokana na dhana potofu iliyokuwa imejengeka ndani ya jamii kuwa watu wenye ulemavu huu hawawezi kufanya ujasiriamali, jambo ambalo si kweli.

Zaidi ya walemavu wa kusikia 50 walishiriki mafunzo hayo wakitokea katika wilaya zilizopo kwenye mikoa ya Mbeya na Songwe, hatua iliyotajwa na TBS kuwa imevuka matarajio ya viziwi 40 waliowatarajia kuhudhuria.

Haukuwa mkusanyiko wenye ugumu kuelewana kutokana na uwepo wa wataalamu wa kutafsiri lugha za viziwi waliowasaidia wawasilishaji wa mada na waongozaji wa semina.

Mafunzo haya yalilenga kutoa elimu ya ujasiriamali katika nyanja za kutambua na kuzingatia ubora wa bidhaa, viwango vinavyohitajika sokoni, kuyatambua masoko na pia kuzijua fursa za ujasiriamali zinazowazunguka walengwa na kuzitambua mamlaka zilizowekwa kwa ajili ya kuwasaidia.

Ni kupitia mafunzo haya Katibu Tawala wilaya ya Mbeya, Hassan Mkwawa, alipata wasaa wa kuwasihi viziwi katika mikoa ya Mbeya na Songwe kuunda vikundi vya ujasiriamali ili kuweza kunufaika na fursa za mikopo zilizopo kwenye halmashauri zao na nyingine zinazoandaliwa na kuletwa na wadau.

Mkwawa aliyemwakilisha, mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kufungua mafunzo hayo ya siku moja anasema walemavu hususani wa kusikia ni miongoni mwa makundi ambayo awali yalionekana kutengwa kwenye shughuli za uzalishaji mali jambo ambalo limewasababishia kuchelewa kupiga hatua kiuchumi.

Anasema ni wakati sasa kwa watu wa kundi hilo kuchangamkia fursa zilizowekwa na serikali na wadau wengine ikiwemo kutenga sehemu ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kuwakopesha wajasiriamali walemavu.

Anasisitiza kwamba wakati Serikali ikipigania kuelekea uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ni wajibu wa kila kundi kutoa mchango wake kulingana na mazingira yanayolizunguka kushiriki kwenye mipango mikakati iliyowekwa ili kufikia lengo kwa pamoja. “Msibaki nyuma walemavu… Undeni vikundi, nendeni kwenye halmashauri zenu mkachukue mikopo. Serikali imejipanga kuwasaidia na ndiyo sababu mnaona hata hii leo TBS wamewaandalia mafunzo haya yatakayowawezesha pia kutambua ubora wa bidhaa mnazopaswa kuzalisha.

“Mkitoka hapa kaweni mabalozi wazuri kwa wajasiriamali wengine kwa kuhakikisha mnatumia ujuzi wenu kuzalisha bidhaa zilizo bora na si bora bidhaa. Tunataka bidhaa zenu zikawe na ushindani kwenye soko la ndani na nje ya nchini kwa kuwa mteja haangalii bidhaa imetengenezwa na kiziwi au nani bali anataka ubora.

“Lakini ni muhimu halmashauri pia zikalenga kuwakopesha wajasiriamali vitendea kazi badala ya kuwapa fedha. Mkimkopesha mfugaji wa kuku fedha akinunua vifaranga vikifa vyote na mtaji wake umepotea. Ni tofauti na mkimkopesha mashine ya kutotoleshea mayai. Vifaranga wakifa atanunua mayai kwingine atatotolesha tena na hawezi kupata hasara kama awali kwa kuwa atakuwa na uzoefu tayari kutokana na hasara aliyoipata mwanzo,” anasisitiza Mkwawa.

Kwa upande wake, Mkuu wa TBS Kanda ya Nyanda za juu kusini, Abel Mwakasonda, anasema shirika hilo kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) wanatambua uwezo walio nao walemavu wa kusikia katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali hivyo ni muhimu kundi hilo likapewa elimu ya kutosha juu ya njia sahihi za ujasiriamali.

Anasema TBS imejipanga kukutana mara kwa mara na viziwi kama ilivyo kwa watu wa makundi mengine ili kuwapa mwongozo ulio sahihi na kuwapitisha kwenye mnyororo utakaowawezesha kuwa wajasiriamali watakaonufaisha familia zao, jamii na Taifa kwa ujumla. Janeth Shawa, Afisa Biashara wa Shirika la Sido mkoa wa Mbeya anasema katika mada yake walemavu wasijifiche majumbani bali waende kwao kuangalia ni ujuzi gani wakifundishwa unaweza kuwasaidia kwenye ujasiriamali ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Sido ni ofisi, ipo kwa ajili yenu njooni… Hatuna ubaguzi ninyi mnaweza kuungana siku moja mkaja kututembelea kisha kila mmoja wenu akachagua anachotaka kujifunza tukamuunganisha na wajasiriamali wengine wanaojifunza. Mnaweza kupangiwa madarasa hata huko wilayani tukawafuata kulingana na ratiba. Pale tutawaunganisha pia na watu wanaotengeneza vifungashio vya bidhaa. Tunaye mtu pale kwetu anatengeneza,” anasema Ni kupitia semina ya mafunzo haya viziwi na wao wakatoa ya moyoni.

Baadhi yao wanasema semina imekuwa na manufaa makubwa kwao kwani walikuwa wamekwishaanza ujasiriamali lakini njia sahihi za kufuata hawakuzijua. Wanasema wamekuwa wakifanya biashara kibubububu kwa kukosa utaalamu na ushauri sahihi.

Tusye Mwalyego, Mwenyekiti wa Chama cha viziwi (Tamavita) mkoa wa Mbeya anasema yeye ni mjasiriamali wa usindikaji maziwa ambapo amekuwa akiuza maziwa mgando katika masoko ya kienyeji. Anasema hii ni kutokana na kukosa utaalamu zaidi na pia kutotambua wapi anaweza kupata vifungashio ili maziwa yake yadumu kwa muda mrefu sokoni.

Lakini nasema kupitia mafunzo ya Sido sasa amepata uelewa wa nini afanye. Queen Maghembe anasema amekuwa akifanya biashara pasipo kujua wapi ni sehemu sahihi ya kuanzia, nini afanye na wapi anakwenda. Anasema alikuwa anajua biashara ni kujianzia tu kumbe kuna mamlaka unapaswa uanze nazo ili pia biashara yako iwe halali.

“TBS tunawaomba huu usiwe mwisho... Uwe mwanzo wa kutupa elimu hii na ifike wilayani maana wapo wengine ambao hawajafikiwa. Sido pia wasibaki ofisini,” anasema Queen.

Kwa upande wake Lilian Johnson anasema huenda kwa kuendesha biashara bila elimu wamekuwa wakiziendesha kinyume cha sheria za nchi.

“Siyo mimi pekee niliyekuwa sijui. Wapo viziwi wengine bado hawajui wanachofanya ni kibaya. Sasa tutaweza kuunda vikundi vidogo, kisha tupate mafunzo Sido, tutafuata sheria na kuanza biashara ndogo na hata kubwa. Viziwi tunaweza kufungua makampuni makubwa makubwa kumbe,” anasema Lilian.

Hatua hii ya makubaliano baina ya Taasisi za kiserikali na walemavu hawa inatia moyo hakika kuwa kundi hili halitoachwa kwenye harakati za kitaifa za kupambana na umasikini, harakati za kuelekea uchumi wa kati wenye kutegemea viwanda.

Pamoja na kuwa changamoto ya mawasiliano ndani ya jamii baina ya walemavu wa aina hii na watu wengine ni kubwa, umuhimu ni kuwatambua na kuwawezesha ni mkubwa zaidi. Sasa kazi kwa halmashauri kuwapa mikopo ili waingie kazini.

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi