loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kilimo cha maharage na tija za kiuchumi

Maharage ni zao linalotumika siyo tu kwa chakula, bali pia kichumikatika familia na taifa. Nchini Tanzania, zao hili hulimwa zaidi katika mikoa ya Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Manyara, Kilimanjaro, Arusha, Kagera, Kigoma, Morogoro, Iringa, Njombe na Songwe.

Takwimu zilizopo zinaonesha Tanzania inaongoza Afrika Mashariki kwa kuzalisha tani milioni 1.2 wakati mahitaji ni tani milioni 1.3. Hata hivyo, bado hayatoshi kwani hutumika pia kibiashara kwa kuuzwa hata nchi za nje kama Kenya, Malawi, Kongo, Rwanda, Afrika Kusini na Burundi. Mratibu wa Taifa wa Utafiti wa Maharage kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Uyole kilichopo Mbeya, Dk Rose Mongi anasema maharage ni chanzo muhimu cha protini kwa mwanadamu.

Anasema: “Uuzwaji wa maharage nje ya nchi ni fursa kubwa kwa wakulima kuongeza kipato.”

Kimsingi, maharage ni moja ya mazao ya jamii ya mikunde, yenye uwezo mkubwa kurutubisha ardhi kupitia bakteria aina ya raizobia vilivyopo kwenye mizizi. Vijidudu hivyo (bakteria) huchukua hewa ya nitrojen angani na kuibadilisha kuwa mbolea inayotumika kwa mimea na mazao mengine yakiwemo mahindi, mtama na mazao na hivyo, kuchochea uchumi kupitia kilimo.

Kwa mujibu wa Mongi, maharage ya aina yoyote yana madini ya chuma na zinki hayo ni muhimu katika kupunguza tatizo la upungufu wa damu linalowakumba watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, wajawazito na wanyonyeshao.

“Hata tatizo la uzito mkubwa walilo nalo watu wengi hasa wanaotumia nyama kwa wingi, linaweza kupunguzwa kwa kula maharage zaidi kwa sababu hayana mafuta yanayohifadhiwa mwilini,” anasema.

Mongi anasema wamekuwa wakifundisha wakulima na wadau kilimo bora cha maharage ikiwa ni pamoja na kuwazalishia mbegu hizo bora, kutumia mbolea, kudhibiti magonjwa, na teknolojia ya hifadhi ya udongo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tunapozalisha mbegu tunahakikisha zitauzika ndani na nje ya nchi,” anasema. Baadhi ya mbegu zinazozalishwa katika kituo hicho ni Njano Uyole, Calima Uyole, Uyole 18, Uyole 03, Uyole 99, Uyole 04 na Nyeupu Uyole. Changamoto zilizopo ni magonjwa hasa ya majani, yajulikanayo kama madoa pembe, ndui ya maharage, kutu na ugonjwa wa mizizi.

“Ni vigumu kuwa na soko zuri la uhakika ikiwa kila mdau atafanya peke. Muuzaji anahitaji mkulima alime mbegu inayohitajika kwenye soko, mzalishaji mbegu anatakiwa kujua soko linahitaji mbegu ya aina gani na vivyo hivyo kwa wadau wengine walioko kwenye mnyororo wa thamani wa zao la maharage, bila hivyo zitakosekana taarifa nzuri na badala yake ni hasara kwa wadau wote,” anasema.

Anasema katika mkoa wa Mbeya, kuna wafanyabiashara wanaofanya kazi na watafiti, wakulima na wadau wengine ili kulima baadhi ya maharage wanayoyataka na yenye soko.

Akizungumzia uchumi wa taifa anasema:“Hivyo kukiwepo na viwanda vya kutosha badala ya kupeleka maharage nje, tutakuwa tunachakata wenyewe na kuuza bidhaa zetu wenyewe. Katika kuchakata na kuuza, tayari hizo ni ajira kwa watu wetu,” anasema.

Mkurugenzi wa Kituo hicho cha Uyole, Dk Tulole Bucheyeki anasema kituo hicho kina aina 22 za mbegu bora za maharage. “Maharage ya Uyole yanapandwa sehemu yoyote Tanzania na hata nje ya nchi kwa kuwa tuna aina mbalimbali,” anasema.

Anasema zikilimwa eka 10 za maharage, mkulima anapata Sh milioni 20, kwani yanaweza kuzalisha magunia 10 kwa eka. Kwa mujibu Dk Tulole wana tani 187.5 za mbegu na mipango yao mwakani ni kuzalisha tani 8000.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geoffrey Mkamilo anasema taasisi hiyo inajihusisha na usambazaji wa teknolojia kwa wakulima na wadau wengine wa kilimo, kutafiti, kusimamia na kuhamasisha matumizi ya teknolojia kwa wakulima na wadau.

TARI Iinavyo zaidi ya vituo 15 kila kimoja kikiwa na jukumu la kitaifa kutafiti na kuendeleza zao moja au zaidi ya moja. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TARI, Dk Yohana Budeba anasema bila utafiti maendeleo ya kilimo hayawezi kupatikana.

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi