loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Chana-talaka’, bidhaa iliyoacha gumzo maonesho ya viwanda Pwani

MABANDA mengi ya maonesho yanaendelea kufunguliwa katika viunga vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani asubuhi hii ya Jumapili ya Oktoba 20, 2019.

Watu bado watu hawajawa wengi sana kwenye maonesho haya ya pili ya viwanda na biashara mkoani Pwani, lakini katika banda moja la wajasiriamali wa kundi la Mshikamano kutoka Temeke, tayari kuna watu kadhaa, miongoni mwao ni askari polisi.

Askari hawa walioko kwenye sare, wanaume takribani watano na mwanamke mmoja, siyo kwamba wanalinda hili banda, bali ni wateja waliokuja kununua au kuuliza bidhaa mbalimbali zinazouzwa hapa. Ninapopita pale, ule wingi wa watu na maswali yanayoulizwa na askari hawa, yananifanya nisogee.

Naangalia saa yangu. Ni saa mbili kasoro robo. Katika banda hili kunauzwa bidhaa mbalimbali kama vile viatu vya ngozi vya kike na vya kiume vinavyotengenezwa na wajasiriamali hawa, mikoba na vikapu, shanga, sabuni za karafuu na mkaratusi, viungo vya chai, majiko kwa ajili ya kufugia kuku, mashati ya batiki na mapambo ya ndani.

Lakini ninagundua kwamba bidhaa moja ndio imesababisha ‘kiwingu’ ninachokiona katika banda hili na takribani watu wengi hapa wakiwemo hawa askari wanataka ufafanuzi wa bidhaa hii. Ninaambiwa inaitwa ‘Chana-talaka’.

Ninaona askari wawili wa kiume wananunua baada ya kupata maelezo haya na yale. Ninataka kufanya mahojiano ya kina kuhusu bidhaa hiyo lakini akina mama hawa wako ‘bize’ kuuza na kutoa na maelezo. Maswali ya wateja hususani bidhaa hiyo ni mengi, hivyo ninaamua kuondoka kusubiri hali iwe shwari. Ninarudi kwenye banda hilo jioni baada ya ‘kiwingu’ kupungua.

Ninapojitambulisha na kuomba kufanya mahojiano nao, hususani kuhusu bidhaa ya ‘Chanatalaka’, kiongozi wao anamtoa mmoja wa wanachama wake ili nijitenge naye pembeni wakati wengine wakiendelea kuhudumia wateja. Mwanadada huyu mcheshi, maji ya kunde anajitambulisha kwa jina la Mariam Mwisa na kwamba ni mmoja wa wanachama waanzilishi wa kundi hilo la Mshikamano kutoka Temeke.

Anasema kikundi cha Mshikamano kina wanachama 15, takribani wote ni wanawake kasoro mwanamume mmoja. Anasema waliwezeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na ndio maana wote wamevaa tisheti nyeupe zikiwa zimeandikwa TASAF.

“Sisi tumekuja hapa kwenye Maonesho ya Mkoa wa Pwani kutafuta fursa za kuuza bidhaa zetu lakini sisi tunatokea Temeke, Dar es Salaam. Wengi wetu tulikuwa akina mama wa nyumbani, tukiwa hatuna mitaji lakini TASAF wametuwezesha, hizi bidhaa zote unazoona tunatengeneza sisi wenyewe kwa mikono yetu,” anasema Mariam.

Ninapomuuliza kama wana duka wanapouzia bidhaa zao nje ya maonesho, Mariam anasema wana duka dogo karibu na gereza la Keko, lakini sehemu kubwa wao ni watu wa ‘kunusa’ maonesho na minada ili kuuza bidhaa zao.

“Tunapokuwa kwenye maonesho kama haya tunaacha kadi zetu za biashara (business cards) kwa hiyo wengi wanaotaka bidhaa zetu wanatupigia simu na sisi tunahakikisha tunawafikishia bidhaa wanazotaka. Lakini mtu akija pale Halmashauri ya Wilaya ya Temeke akatuulizia ni rahisi pia kutupata,” anasema.

Baada ya maelezo hayo, sasa tunaingia kwenye bidhaa hiyo iliyoacha gumzo katika maonesho hayo ya viwanda inayoitwa ‘Chana Talaka’. Mariam anafafanua kwamba chana-talaka ni nguo ya ndani, walioibuni kwa ajili ya kuvaliwa na akina mama walio kwenye ndoa na kwamba wanaitengeneza kwa kutumia shanga za kawaida.

“Kama unavyoona, hili ni vazi la ndani na ni mahususi kwa kuvaliwa chumbani. Wateja wetu wenyewe ndio wamelipa jina hilo ‘chana talaka’ kwa sababu wanasema kama baba atakuwa na ghadhabu zake, hata kama atakuwa keshakuandikia talaka halafu akakukuta kitandani umevaa hii nguo, ghadhabu zinapotea na kama ni talaka anaichana chana,” anasema Mariam.

Je, nini kilisababisha wapate wazo la kuunda vazi hilo? Akijibu swali hilo, Mariam anaanza kwa kusema kwamba katika miaka ya karibuni, utamaduni wa wanawake kuvaa shanga umeongezeka sana tofauti na miaka michache iliyopita.

“Sielewi sababu lakini nadhani watu wamegundua kwamba shanga zina nafasi yake muhimu kwa wanandoa wanapokuwa chumbani na ndio maana wengine wanaziita chachandu, yaani kitu kinachoongeza hamu ya kula… Wakati mwingine kupitia utamaduni huu wa shanga, mwanamume hana sababu ya kutafuta dawa ya nguvu za kiume,” anasema Mariam.

Anasema kabla ya kuanza kutengeneza nguo hiyo ya ndani kwa kutumia shanga, walianza kutengeneza mkanda mzito wa kuvaa kiunoni.

“Tulikutwa tunatengeneza mkanda wa shanga wa kuvaa, baadaye tukajaribu kutengeneza kitu kama kibwaya hivi (mithili ya sketi) kwa kutumia shanga na ndipo tukapata wazo la kutengeneza underwear (nguo ya ndani) kamili kwa kutumia shanga,” anasema.

Anasema kwa mara ya kwanza walianza kuuza bidhaa yao hiyo mwaka jana akatika maonesho ya Nanenane, Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro.

“Tuliuza chana-talaka mbili tu mpaka tukakata tamaa, lakini baadaye hao wateja wawili wakaanza kutuletea wateja zaidi kwa sababu walichukua mawasiliano yetu. Yaani kwa sasa karibu kila siku tunatuma Morogoro chana-talaka kupitia kwenye mabasi,” anasema na kuongeza kwamba soko lao limeongezeka Morogoro baada ya kushiriki kwenye maonesho ya Nanenane mwaka huu.

Anasema malighafi wanazotumia kutengeneza chana-talaka pamoja na bidhaa nyingine wananunua Kariakoo na kwamba pale wanapokuwa hawana shughuli nyingi, yeye ana uwezo wa kutengeneza chana-talaka tatu kwa siku. Kuhusu wateja anasema asilimia 70 ya wateja wao katika maonesho mengi wanakokwenda ni wanaume wakifuatiwa na akina dada wasio na waume.

“Wale akina dada waliokaa kibiashara nao ni wateja wetu wakubwa. Kuna wanawake wengine wanaona aibu kununua hizi bidhaa hadharani kwa sababu unaweza kuona mwanamume anakuja kwenye maonesho hapa na mkewe, kisha mumewe anamuuliza, nikununulie chana-talaka, mwanamke anakataa. Lakini wengine baada ya muda mwanamume anarudi kivyake vyake na kununua.

“Nadhani wengine wanaona aibu, lakini wanawakosesha kitu muhimu wenzi wao wa kiume kwa sababu wanapenda. Maisha ya ndoa yanahitaji upendo baina ya mume na mke kwa kila mmoja kumfanyia kitu mwenzie kinachomwongezea hamu ya yale mambo yetu watu wazima,” anasema Mariam Mwisa.

Anasema pia wanapata wateja wengi wa shanga na chana-talaka kwa wenyeji wa makabila ya Pwani, hususani Dar es Salaam na Mtwara. “Inaonekana hawa wenzetu wa mikoa ya Pwani wanajua vizuri umuhimu wa sanaa hii ya shanga… Mimi ninaamini mwanamke ukiwa makini na sanaa ya chumbani inasaidia sana kumfanya baba asichepuke,” anasema.

Anatoa mwito kwa akina mama wenzake kuwa wabunifu katika mambo ya chumbani sambamba na kuwapikia waume zao chakula bora na kuwashauri wafanye mazoezi ili kuboresha afya zao ikiwemo ‘kulinda heshima ya ndoa’.

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi