loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wizara- Wahitimu serikali za mitaa msifikirie kuajiriwa

WAHITIMU wa Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) wametakiwa kuacha kufikiria kuajiriwa, badala yake wafikirie kujiajiri na kuajiri wengine.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Profesa Elisante ole Gabriel kwa wanataaluma katika kongamano la 11 la Chuo cha Serikali ya Mitaa.

Amesema wahitimu wa chuo hicho wanatakiwa kuachana na ndoto za kuajiriwa mara wakihitimu chuoni hapo badala yake watafute namna kujiajiri na kuajiri wengine kwa kutumia utaalamu walioupata.

Amesema wachache watakaobahatika kuajiriwa serikalini watumie taaluma yao vizuri kwa ajili ya maendeleo ya nchi na ikibidi kuwa chachu ya kuajiri wengine katika sekta mbalimbali watakazokuwa wakizisimamia pia.

Amesema nchi inaelekea kwenye uchumi wa kati wa viwanda hivyo wahakikishe ifikapo mwaka 2025 wanakuwa na mchango angalau katika uchumi huo kwa kutumia elimu waliyoipata.

Akizungumza, Mkuu wa LGTI, Dk Mpamila Madale amesema chuo hicho kimejipanga kuendeleza elimu na mafunzo bora ili kuhakikisha vijana wanaohitimu wanakuwa na uwezo wa kujiajiri katika nyanja mbalimbali. Alisema chuo hicho kinafanya mjadala na kuweka mkakati wa namna gani kinachangia maendeleo ya viwanda.

“Kwa kuanza imeandaliwa mitaala rafiki inayoakisi matakwa ya umma katika kuwaandaa vijana,”alisema.

Alisema katika kuwaandaa vijana, chuo hicho kimekuwa kikitoa kozi za muda mfupi, cheti, stashahada na kuanzia Novemba mwaka huu kitaanza kutoa shahada kwa ajili ya kuwaandaa viongozi mbalimbali katika Serikali za Mitaa.

Awali, akizungumza wakati wa mjadala katika mada ya mchango wa chuo hicho katika maendeleo ya Serikali za Mitaa, Kamishna wa Bajeti Msaidizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Charles Mwamwaja alisema wakati umefika watafiti na wanataaluma waangalie namna taasisi na vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu vitakavyokuwa imara na kuendelea kukua.

Mhitimu Bora wa Kike wa mwaka huu, Mariam Dominic amesema wamejipanga kutumia elimu aliyoipata kusaidia wananchi wenye changamoto mbalimbali katika Serikali za Mitaa.

Mhitimu bora wa kiume, Rashid Barasha alisema wapo tayari kutumia elimu yao kujiajiri na kuajiri wengine.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi