loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hifadhi za taifa zaongezeka, utalii wapaa

BAADA ya Bunge la Tanzania kuridhia mabadiliko ya kuligawa pori la akiba la Selous katika maeneo mawili kwa agizo la Rais John Magufuli ili kuwa na hifadhi ya Taifa ya Nyerere na eneo lingine kubaki kuwa pori, Tanzania sasa ina hifadhi za taifa 18 kutoka hifadhi 16 zilizokuwepo hadi mwaka 2015.

Hatua hii ilikuja miezi michache baada ya Rais John Magufuli kuridhia mapendekezo ya kuanzisha kwa hifadhi nyingine mpya nchini ya Burigi-Chato. Kama alivyosema bungeni wakati wa kupitisha azimio la kuanzisha hifadhi ya Nyerere, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla alisema: “Malengo ya nchi yetu, siyo kuwa na maeneo ya hifadhi na kuwa nayo tu, bali kuyafanya maeneo haya yatusaidie katika kupambana na umaskini.”

Kwa mujibu wa Dk Kigwangalla, hatua za kuongeza hifadhi zinalenga kuongeza pato la taifa kwa kuongeza idadi ya watalii, kuwezesha jamii kunufaika na fursa za utalii, kuimarisha uhifadhi, kutunza vyanzo maji, kuhifadhi mazalia ya samaki, kuboresha miundumbinu ya barabara na faida nyingine lukuki.

Katika makala yake kuhusu umuhimu wa kuanzisha hifadhi ya Nyerere, mchambuzi Ernest Makunga aliandika katika gazeti hili kwamba hifadhi hiyo inayogusa mikoa ya Lindi, Ruvuma, Morogoro na Pwani ni ya pili baada ya Serengeti kwa wingi wa aina za wanyamapori.

Akaandika: “Hatua ya Rais Magufuli ya kuanzisha Hifadhi hii ya Taifa ya Julius Nyerere katika eneo la Selous ni ya kupongezwa sana kwani eneo hili licha ya kuwa na vivutio vingi vya asili vya utalii, ni watalii wachache waliokuwa wakilitembelea, tena watalii wawindaji.”

Ni kwa mantiki hiyo mchambuzi huyo anasema kwamba pori la Selous halikuwa na tija sana katika kuliingizia mapato taifa ukilinganisha na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo inafanana sana na Selous kwa wingi wa wanyamapori wa aina tofauti tofauti. Mchambuzi huyo anaamini kwamba hifadhi hii itavutia watalii wengi na inaweza ikakaribiana, kulingana au hata kuzidi hifadhi ya Serengeti iliyoshinda mara mbili tuzo ya kimataifa ya kuwa hifadhi bora Afrika na hivyo kuiingizia nchi yetu fedha nyingi za kigeni mbali na kuongeza ajira.

“Sababu zinazoifanya Selous kuwa hifadhi itakayokuwa bora ziko nyingi, miongoni ni kuwa pori ambalo bado halijatumika sana kwa shughuli za kitalii, hivyo kuwa na uasili mwingi kama vile misitu ya asili, maporomoko ya maji ya asili na mito ya asili,” aliandika Makunga.

WATALII WAONGEZEKA

Taarifa zilizopo zinaonesha kwamba licha ya idadi ya watalii kuongezeka kutoka wastani wa watalii milioni 1.2 mwaka 2016 hadi kufikia watalii milioni 1.5 mwaka jana, watu kadhaa mashuhuri duniani wamekuwa wakizuru vivutio vya Tanzania katika kipindi hiki cha miaka minne ya utawala wa awamu ya tano. Miongoni mwa watalii mashuhuri ni pamoja na mwigizaji maarufu wa filamu kutokea Hollywood nchini Marekani, Will Smith na mkewe Jada Pinkett- Smith.

Smith na mkewe wakijivinjari katika mbuga ya Serengeti walikutana na msanii mwingine kutokea huko huko Marekani ambaye ni mwanamitindo na mrembo, Chanel Iman. Mbali na hao, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Taifa la Israel, Ehud Barak naye alitembelea hifadhi za nchi yetu pamoja na Miss World wa 2018, Vanessa Ponce. Watu maarufu wengine waliotembelea Tanzania ni mwanasoka wa zamani wa kimataifa wa Uingereza, David Backham, mchezaji wa taifa wa Ufaransa anayekipiga Crystal Palacem Mamadou Sakho na mchezaji wa Evarton Morgan Schneiderlin.

Mwezi Aprili mwaka huu, Tanzania ilipokea watalii 1,000 kutoka Israel na kuifanya kuwa nchi ya sita kwa kuleta watalii wengi nchini kutoka ya 20 ndani ya kipindi cha miaka mitatu. Mwezi huo huo, meli ya Silver Whisper iliwasili jijini Dar es Salaam ikiwa na watalii 333 kutoka mataifa mbalimbali duniani. Mwezi uliofuata wa Mei, Tanzania ilipokea watalii 343 kwa mpigo kutoka China ikiwa ni kundi la kwanza la watalii kutoka nchini humo kati ya watalii 10,000 wanaotazamiwa kutembelea Tanzania kutoka China ndani ya mwaka mmoja.

MAPATO UTALII YAONGEZEKA

Kutokana na ongezeko la watalii nchini, mapato ya serikali yamekuwa yakiongezeka pia mbali na ongezeko la ajira katika sekta hiyo ya utalii. Mwezi Agosti mwaka huu, Katibu wa Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda alisema kwamba kutokana na utafiti uliofanywa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Idara ya Uhamiaji mwaka 2018, walibaini kwamba mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 2.3 mwaka 2017 hadi dola biliobi 2.4, sawa na ongezeko la asilimia 7.2. Aliongeza kwamba sekta ya utalii pia inaonesha kwamba ndiyo inayoingiza fedha nyingi za kigeni kwa kuchangia asilimia 25 ya fedha zote za kigeni huku ikichangia asilimia 17 ya pato la taifa (GDP).

YAJAYO YANATIA MATUMAINI

Katika kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la watalii, mengi yamekuwa yakifanywa na serikali ikiwa ni pamoja na kuendelea kununua ndege hatua ambayo inaelezwa kwamba itachangia kuongeza idadi ya watalii nchini. Hatua ya kununua ndege inakwenda sambamba na ujenzi wa viwanja vya ndege katika mikoa mbalimbali kikiwemo kile Chato ambacho kinatazamiwa kuhudumia hifadhi mpya ya Burigi-Chato. Dk Kigwangalla amekuwa akisema kuwa hatua ya kufufua na kuboresha Shirika la Ndege (ATCL) na ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) vitaongeza maradufu watalii nchini siku zijazo.

Imekuwa kwamba licha ya ndege kutangaza nchi kimataifa, lakini watalii wanakuwa na uhakika wa kuja nchini moja kwa moja bila kuzunguka zunguka wanapokuwa wanatumia mashirika mengine ya ndege.

Tayari kuna mipango ya ndege za Tanzania kwenda Uingereza, China na mataifa mengine ya Ulaya ambapo kwa sasa zinakwenda pia India, hatua ambayo inatazamiwa kuvutia watalii zaidi kuja. Katika kuimarisha uhusiano katika nyanja za utalii, Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) na Kampuni ya Touchroad International Holdings Group (TIHG) ya nchini China wameshatia saini mkataba wa kufanya majadiliano ya kibiashara ya namna ya kuwasafirisha watalii zaidi ya 10,000 kuja Tanzania.

Lakini uwepo wa ndege nyingi na viwanja kunamaanisha pia kuwawezesha watalii wanapokuwa nchini kufika maeneo mbalimbali ya nchi ili kujionea vivutio kuliko kutegemea ndege za kukodi kama ilivyokuwa huko nyuma.

Hivi karibuni Tanzania imepokea ndege nyingine kubwa aina ya Boeing 787 Dreamliner kutoka nchini Marekani ambayo ni ya saba kati ya 11 zinazotarajiwa kununuliwa na serikali hadi kufikia mwaka 2022. Ndege hiyo ina uwezo wa kubeba jumla ya abiria 262 na uzito wa tani 227. Waziri Kigwangallah amekuwa pia akisema kwamba ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), mbali pia na kuboresha usafiri wa watalii, utachangia pia kuinua utalii wa picha nchini.

Kuhusu kuleta watalii kwa njia ya meli, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii zilishakutana na kujadili namna ya kutekeleza mkakati wa muda mfupi na muda mrefu wa kuongeza idadi ya meli za utalii nchini.

Wizara hizo zilipeana majukumu katika kuboresha miundombinu ya kuhudumia meli za kitalii ili ziweze kufunga katika gari maalumu ndani ya bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na watalii kutumia gati jipya linalojengwa huku mipango ya muda mrefu ikiwa ni kupata gati maalumu kwa ajili ya meli za kitalii. Makala haya yameandaliwa na Hamisi Kibari kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi