loader
Picha

JWTZ ‘yatafuna mfupa’ uliowashinda TBA

HATIMAYE Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekamilisha agizo la Rais John Magufuli la kujenga nyumba za makazi ya Askari Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam.

Awali, nyumba hizo zilikuwa zikijengwa na Wakala wa Majengo nchini (TBA) tangu mwaka 2016 kwa gharama ya Sh bilioni 10 na baada ya ujenzi huo kusuasua, ndipo Machi mwaka huu, Rais Magufuli aliamua kuwakabidhi JWTZ kukamilisha kazi hiyo.

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Charles Mbuge, alisema jana kuwa jeshi limeshakamilisha ujenzi wa nyumba hizo tangu Oktoba 15 mwaka huu ambazo ni maghorofa 12.

Kukamilika kwa ujenzi wa maghorofa hayo kunatoa fursa kwa familia 172 za askari na maofisa magereza kuishi ndani yake.

Brigedia Jenerali Mbuge alisema wakati wowote atakwenda kuzikagua nyumba hizo na akijiridhisha atampa taarifa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Jenerali Venance Mabeyo, ili naye azikague na kisha amwombe Rais Magufuli aweze kuzifungua rasmi.

Alisema japo alimwahidi Rais Magufuli kuzikamilisha nyumba hizo katika kipindi kisichozidi miezi miwili na nusu tangu akabidhiwe Machi 16 mwaka huu, lakini kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha haikuwezekana kukamilisha ujenzi ndani ya muda aliosema.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa JKT, kama nyumba hizo zingejengwa kama alivyotaka Rais Magufuli tangu mwanzo, zingeweza kuchukua familia 326.

Wakati alipotembelea ujenzi wa nyumba hizo Machi 16 mwaka huu, Rais Magufuli alichukizwa na kitendo cha TBA kushindwa kukamilisha ujenzi kwa zaidi ya miaka miwili tangu wakabidhiwe kazi hiyo mwaka 2016.

Kutokana na hali hiyo, aliamua kuwafukuza TBA na kuliagiza JWTZ kukamilisha ujenzi wake. Wakati huo akiwa na Cheo cha Kanali ambapo kwa sasa ni Brigedia Jenerali, Mbuge alimhakikishia rais kuwa jeshi lingeifanya kazi hiyo usiku na mchana na kuikamilisha si zaidi ya miezi miwili na nusu kwa kuwa jeshi halishindwi kitu.

“Mimi kwenye serikali nataka kazi, siwezi kwenda kwenye ‘site’ halafu hakuna chochote kinachofanyika tangu mwaka 2016, haiwezekani, si kwa wakati wangu, kuanzia leo, watu wa TBA nimewafukuza, msionekane hapa, nitafanya tathmini ya pesa yangu niliyoitoa Sh bilioni 10 nijue imetumika wapi, ili kusudi kama walitumia vibaya wazitapike, na watazitapika kweli,”alisisitiza Rais Magufuli. Akaongeza:

“Sasa Kanali (kwa sasa ni Brigedia Jenerali), kuanzia leo, hii ‘site’ nimewakabidhi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), TBA nimewafukuza hapa, nimewaleta ninyi msimamie hapa, asiwabughudhi mtu yeyote, mkishamaliza kazi, nitakuja niwakabidhi Magereza.”

Kabla ya kuwakabidhiwa kazi hiyo, alilisifu JWTZ kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kujenga ukuta kuzunguka mgodi wa Mirerani mkoani Manyara pamoja na ujenzi wa nyumba 45 za Makao Makuu Dodoma Baada ya maagizo hayo, alimtaka Birigedia Jenerali Mbuge kumweleza mpango kazi wake utakavyokuwa.

Katika maelezo yake, alimhakikishia rais kuwa siku iliyofuata ya Machi 17 angewapeleka wataalamu kwa ajili ya kuanza ujenzi mara moja na wangeifanya kazi hiyo usiku na mchana.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 utarejea tena Juni ...

foto
Mwandishi: Na Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi