loader
Picha

Kidato cha 4 kuanza mitihani yao leo

JUMLA ya watahiniwa 485,866 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne (CSEE) utakaoanza kufanyila leo hadi Novemba 22, mwaka huu, huku idadi ya watahiniwa hao ikiongezeka kwa asilimia 1.37 ukilinganisha na mwaka jana.

Kati ya watahiniwa hao, watahiniwa wa shule ni 433,052 na wa kujitegemea ni 52,814 na kwamba idadi ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa mwaka jana ni 427,181, hivyo ni ongezeko la watahiniwa 5,871 kwa mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonde alisema mtihani huo utafanywa katika jumla ya shule za sekondari 4,933 na kwenye vituo 1,050 vya watahiniwa wa kujitegemea.

Kati ya watahiniwa hao wa shule, wanaume ni 206,420 sawa na asilimia 47.67 na wanawake 226,632 sawa na asilimia 52.33.

Pia, watahiniwa wenye mahitaji maalumu wapo 842, kati yao 450 ni wenye uoni hafifu, 42 wasioona, 200 wenye ulemavu wa kusikia na 150 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili.

Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 52,814 waliosajiliwa wanaume ni 23,418 sawa na asilimia 44.37 na wanawake ni 29,396 sawa na asilimia 55.66.

Kati yao watahiniwa hao wa kujitegemea wenye mahitaji maalum wako 28 ambapo wenye uoni hafifu ni 20 na wasioona wanane.

“Ongezeko la watahiniwa linatokana na juhudi za serikali za kutoa elimu bure, hivyo wazazi wamekuwa na mwamko wa kupeleka watoto wao shuleni, pia, udanganyifu kwenye mitihani umepungua nchini na kusababisha nchi mbalimbali kuja kujifunza namna ya kudhibiti wizi na udanganyifu kwenye mitihani, tuendelee kuwaelimisha wananchi madhara ya udanganyifu kwani ufaulu unawezekana bila kudanganya,”alieleza.

Hata hivyo, alisema jumla ya watahiniwa 12,984 wamesajiliwa kufanya mtihani wa maarifa (QT) ambapo kati yao wanaume ni 5,493 sawa na asilimia 42 .30 na wanawake ni 7,491 sawa na asilimia 57.70. Dk Msonde alisisitiza kuwa maandalizi kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mtihani, vijitabu na nyaraka zote muhimu zinahusiana na jambo hilo katika mikoa yote Tanzania bara na Visiwani.

“Mtihani huu ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kwa kuwa hupima uwezo na uelewa wa wanafunzi katika yale yote waliojifunza kwa kipindi cha miaka minne,

Aidha matokeo ya mtihani huu pia ni muhimu kwani hutumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu ya sekondari pamoja na fani mbalimbali za utalaamu wa kazi kama vile afya, kilimo, ualimu hata ufundi,”alifafanua.

Baraza hilo limetoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri kuhakikisha kuwa taratibu za uendeshaji mitihani ya taifa zinazingatiwa ipasavyo kwa kuhakikisha mazingira ya vituo vya mitihani yapo salama, tulivu na kuzuia mianya inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu.

“Wasimamizi wanaelekezwa kufanya kazi yao kwa weledi na kwa kuzingatia Kanuni za Mitihani na miongozo waliyopewa. Pia muhakikishe mnalinda haki ya watahiniwa kwenye mahitaji maalum,” alisema.

Alisema kwa upande wanafunzi wanaamini kuwa walimu wamewandaa vizuri katika kipindi chote cha miaka minne hivyo ni matarajio yao kuwa watahiniwa hao watafanya mitihani yao kwa kuzingatia kanuni za mitihani ili matokeo yaoneshe uwezo wao halisi kulingana na maarifa na ujuzi waliopata katika kipindi hicho.

Baraza hilo limewataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya mitihani na hivyo, hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa mtihani huo na kwamba halitosita kukifuta kituo chochote endapo litajiridhisha kuwa uwepo wake unahataraisha usalama wa mitihani ya taifa.

Aidha baraza hilo limewaasa wasimamizi wa mitihani, wamiliki wa shule, walimu na wananchi kwa ujumla kutojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu kwani hawatasita kuwachukulia hatua wale wote watakaohusika.

“Wadau wote wanaombwa kutoa taarifa katika vyombo husika kila wanapobaini mtu au kikundi cha watu kujihusisha na udanganyifu wa mitihani wa aina yoyote ile, “ alisisitiza Dk Msonde.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Na Francisca Emmanuel

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi