loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tusijifanye hatusikii, hatuoni ‘vita’ kuwalinda watoto wa kike

SAFU yako ya Kama Mzazi wiki hii inataka kukabiliana moja kwa moja na wazazi, walezi wa watoto, viongozi wa serikali, wa dini na wa kimila kuchukua hatua za makusudi kudhibiti tatizo la wanafunzi wa kike kukatisha masomo kwa sababu ya kupachikwa mimba.

Jumatano wiki iliyopita, Oktoba 30, 2019 gazeti hili liliandika habari katika ukurasa wa mbele iliyokuwa inaeleza jinni mimba zilivyokatisha masomo wanafunzi 141 Songwe na 100 Tunduru. Hayo ni maeneo mawili tofauti katika mkoa mpya wa Songwe na lingine Tunduru katika mkoa wa Ruvuma.

Maeneo hayo mawili tu yameripotiwa kukumbwa na ‘janga’ la watoto 241 wa kike kupewa na hivyo kuwa sababu ya kuondoka kwenye mchakato adhimu na muhimu wa kupata elimu.

Hao ni watoto wetu wa shule za msingi na sekondari ambao serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kwa makusudi kabisa inawasomesha bure kwa kutumia kodi za wananchi ambapo zaidi ya Sh bilioni 23 kila mwezi zinatumika kugharimia elimu yao.

Ni ukweli usiopingika pia kwamba kila yanapotangazwa matokeo ya mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi kila mwaka hutajwa idadi ya wanafunzi waliojiandikisha walipoanza darasa la kwanza hadi wanapohitimu kwa kufanya mitihani husika huku ikitajwa idadi ya walioishia njiani kwa sababu mbalimbali, kubwa kwa wasichana ikiwa ni kupichikwa mimba na wanaume wapumbavu.

Ni mamia na maelfu ya watoto wetu wa kike hukoseshwa elimu ambayo ni ufunguo wa maisha yao kama wengi tunavyofahamu na hivyo kuwaacha katika hali ngumu ya kukosa ufunguo huo na hivyo kulala nje ya nyumba salama kwa maisha mazuri ya binadamu.

Ikumbukwe kwamba usemi kwamba unaposomesha mtoto wa kike, unasomesha jamii wakati kwa mtoto wa kiume unasomesha mtu mmoja!

Safu hii inawakumbusha wote kuwajibika kudhibiti kadhia hii dhidi ya watoto wetu wa kike kwa sababu uwezo wa kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika na waharibifu wa watoto wetu hao upo.

Wajibu wa kukuza watoto wote; wa kike na wa kiume, ni wa wazazi kwa maana ya wale waliowazaa, walezi kwa wale ambao hawana wazazi kwa sababu yoyote ile, walimu, viongozi wa serikali, dini na wale wa kimila.

Kimsingi, kila mmoja wetu ana nafasi yake katika makuzi ya watoto hawa. Wakati kwa upande wa wazazi na walezi wanatakiwa kuhakikisha mahitaji ya muhimu ya chakula, malazi na mavazi yanapatikana kwa watoto bila ajizi, serikali na jamii kwa ujumla wake ihakikishe kwamba watoto wanasoma shule zilizokaribu na maeneo wanayoishi na zile zilizombali, basi watoto waishi katika mabweni kudhibiti utoro na kudanganywa na wakware kwa upande wa wasichana.

Sambamba na hatua hizo, jamii pia ishikamane kukabiliana na mila na desturi potofu zinazotoa mwanya kwa watoto wa kike kuolewa mapema kwa sababu yoyote ile na wale wanaogundulika kuhusika katika kuwapachika mimba, jamii ihakikishe watuhumiwa wanafikishwa kwenye mkono wa sheria.

Wazazi watakaogundulika kuwakingia kifua wapachika mimba nao wachukuliwe hatua.

Kama Mzazi inapenda kutoa wito maalumu hapa kwamba yeyote atakayetenda kinyume cha matarajio hayo ya msingi ya haki za watoto wetu wa kike kupata haki yao ya elimu kwanza, basi wananchi washirikiane na kushikamana kwa hali na mali kuwapeleka polisi bila kufanya ajizi ili wakapatiwe haki yao kwa mujibu wa sheria.

Tukumbushane kwamba Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere baada ya nchi yetu kupata uhuru alitangazo vita dhidi ya maadui watatu wa taifa letu; ujinga, maradhi na umasikini.

Wakati maradhi na umasikini ulikabiliwa kwa namna yake, vita dhidi ya ujinga dawa yake ni kwenda darasani kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu. Inaelezwa kwamba ukishampiga adui ujinga, basi ni rahisi kuwagaragaraza maaui waliobaki, maradhi na umaskini. S

hime Watanzania, vita dhidi ya ujingha iendelee kuimarishwa. Hili linawezekana kwa kushirikiana na kushikamana.

NATAKA niwe mkweli kwa nafsi yangu kuwa, hata kama tungekuwa ...

foto
Mwandishi: Na Nicodemus Ikonko

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi