loader
Picha

JPM akata mzizi wa fitna uteuzi CAG

BAADA ya kuwepo mjadala mkubwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu uteuzi na utenguzi wa nafasi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Rais John Magufuli amemaliza mijadala hiyo kwa kuweka bayana kuwa nafasi hiyo, haipo juu ya mamlaka ya mihimili mikuu mitatu ya nchi yaani Serikali, Bunge na Mahakama.

Aidha, Rais Magufuli amesema kuna mambo watu hawaelewi kwamba ikiwa Rais ana mamlaka kisheria ya kumteua mtu (akiwamo CAG), basi ijulikane kuwa anayo mamlaka ya kumtengua wakati wowote kwa kufuata utaratibu uliopo. Rais Magufuli alieleza hayo jana, Ikulu, jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni akiwemo CAG mpya, Charles Kichere ambaye uteuzi wake uliibua mjadala baada ya kutemwa kwa mtangulizi wake, Profesa Mussa Assad.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli alisema,“Kuna mambo hayaeleweki kwa baadhi ya watu labda nieleze kidogo hapa. Mkataba wa CAG kisheria ni miaka mitano, lakini pia unaweza kukaa mwaka mmoja.

“Taratibu za kukutoa zipo, zinafanywa na Rais. Duniani ukipewa mamlaka ya kuteua hukosi ya kutengua. Aliyekuwepo sasa anamaliza muda wake saa sita usiku leo (jana), kipindi cha miaka mitano kinaisha. Nenda kesho kafanye kazi,” Rais alimwagiza CAG mpya Kichere.

Maelekezo mengine kwa CAG Magufuli alimtaka Kichere asiende kujifanya mhimili mwingine na kumtaka kujua kuwa, mihimili ni mitatu tu katika nchi na kama alivyofanya kiapo cha utii wa Katiba na sheria nyingine za nchi, akatii sheria hizo.

“Nafasi yako ni Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali. Mwenye serikali yupo. Kafanye kazi zako vizuri bila kuonea watu. Ukipewa maagizo na Bunge tekeleza, ukipewa na Mahakama tekeleza, usibishane nao, wewe ni mtumishi,” Rais alimweleza CAG mpya.

Alimtaka akasimamie ofisi hiyo vizuri na kuondoa uchafu wote uliopo, ikiwamo wa baadhi ya maofisa wanapotumwa kwenda kukagua Balozi , wanalipwa hapa nchini na wakifika kaika ofisi za Balozi hizo wanadai malipo mengine.

“Ofisi ya CAG si ‘clean’ (safi) kama mnavyofikiria. Mauchafu uchafu haya ukayasafishe. Hatukosei tunapochagua, najua ulipata division one (daraja la kwanza) kidato cha nne na cha sita, una degree (Shahada) ya Sheria na Uhasibu ulipata daraja la juu la pili (Upper Second), una Masters (Shahada ya Uzamili) hukuwahi kupata supplement (kushindwa somo), umefanya kazi kwingi.

“Una unyenyekevu, ulitolewa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) hukusema neno. Wengine ukiwateua wanafikiri nafasi ni zao, ukimteua u-DC (Ukuu wa Wilaya) ukimtoa analalamika, mbona alipoteuliwa hakulalamika,” alisema Rais.

Aidha, Rais baada ya kumueleza CAG mpya Kichere kuhusu mamlaka yake ya kuteua na kutengua, alimtaka asiogope bali akafanye kazi kwa kuhakikisha anaondoa uchafu wote katika ofisi ya CAG na mambo mengine asiyoyajua, ataelezwa na Wizara ya Fedha na Mipango huku akimtaka akamtangulize Mungu mbele.

CAG Kichere azungumzia uteuzi na kipaumbele chake Kichere akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuapishwa, alisema maagizo yote ya Rais atayatekeleza na kueleza kipaumbele chake ni ukaguzi katika serikali za mitaa, alikobaini kwa kipindi akiwa Katibu Tawala Mkoa wa Njombe kuwa hesabu katika eneo hilo hazijakaa vizuri.

“Siwezi kuzungumza mengi sasa lazima nifike kwanza ofisini. Lakini lile agizo la Rais kuhusu posho kulipwa mara mbili nitalipiga marufuku kwa kuandika barua na kuzisambaza katika Balozi zetu zote nje ya nchi kwa kuwa double payment (malipo mara mbili) ni kosa na hatuwezi kusimamia na kushauri wengine kama sisi tunatenda hayo,” alisema Kichere.

Kuhusu mtazamo wa jamii alipoteuliwa RAS alishushwa, Kichere alisema anaamini na ni msimamo wake kuwa katika Serikali kuna mgawanyo wa majukumu na si kulalamika.

“Nimekuwa Naibu Kamishna TRA, kisha Kamishna Mkuu TRA na nikapelekwa kuwa RAS na sasa CAG, haya yote ni majukumu tu. Namshukuru sana Rais kwa kuniamini, nimekaa Serikali Kuu kwa muda, nimeenda Serikali za Mitaa na sasa CAG, nimejifunza mengi katika Serikali za Mitaa, nilienda kule si kufanya kazi tu bali kujifunza.

“Nina nyuzi 360 katika kuielewa Serikali za Mitaa, nimejifunza mambo mengi hasa usimamizi na matumizi ya mapato katika halmashauri, nimeziona changamoto nyingi huko. Ukaguzi katika Serikali za Mitaa haujakaa vizuri, nitaanza nako huko,” alieleza Kichere.

Alimpongeza Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo kwa namna anavyopambana kushughulikia changamoto katika halmashauri na serikali za mitaa, aliomba ushirikiano zaidi kusimamia eneo hilo ambako ndiko waliko wananchi wa kawaida. Kichere aliahidi kufanya kazi bega kwa bega na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kueleza kuwa kama alivyosema Rais Magufuli, anatambua mihilimi ipo mitatu na wa nne usio rasmi ni vyombo vya habari.

Alisisitiza kuwa CAG si tu jicho la Bunge, bali ni macho, kwani anaenda kuangalia kwa macho mawili kwa kina na kufanya kazi kwa niaba ya mhimili huo. Alisema akiwa Kamishna Mkuu TRA, alifanya kazi kwa karibu na kamati za Bunge hivyo kupitia kamati nne atakazofanya nazo kazi moja kwa moja (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), atafanya kazi kwa niaba ya mhimili huo.

Spika Ndugai ampokea Kichere Viongozi wawili pekee jana walipewa nafasi ya kutoa salamu baada ya wateuliwa kuapa ambao ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Akizungumza kuhusu CAG mpya, Ndugai alisema,”Kichere karibu sana, sisi Bunge tunaanza shughuli zetu kesho (leo) na tutaangalia mipango ya kitaifa kuisaidia Serikali kuona bajeti ya mwaka 2020/2021”.

Ndugai alisema eneo muhimu la hesabu za serikali na matumizi yake, Bunge linamtegemea sana CAG, kwani ndiye jicho pekee na chombo muhimu cha kuona na kushauri kuhusu matumizi mbalimbali.

Alimweleza Bunge lipo tayari kufanya naye kazi kupitia kamati zake nne (PAC, LAAC, PIC na Bajeti) na kamati zote za Bunge na kutambua kuwa taarifa yake Bungeni ni ya muhimu na huwa zinajadiliwa kwa umakini mkubwa. Awali, Ndugai alimpongeza Rais kwa uteuzi huo na kuwaeleza wateuliwa kuwa Watanzania wanahitaji huduma yao na wanaamini kama ambavyo Rais amewaamini.

“Hivi karibuni Rais alitembelea gereza la Butimba, tulijionea mahabusu waliokaa muda mrefu. Wabunge tunapata muda wa kutembelea mahabusu, kule kwangu Kongwa kuna mambo mengi yanaweza kukutoa machozi.

Mkasaidie mahabusu hawa, wenye kutoka watoke na wa kubaki wabaki. Jaji Mkuu awapa somo majaji wapya Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Juma, pamoja na kumpongeza Rais kwa uteuzi huo wa majaji 12 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, aliwatahadharisha majaji wapya kuwa wahakikishe wanaitunza imani walioaminiwa na Watanzania kupitia Rais na ikiwa vinginevyo, wakiipoteza, sheria itatumika kushughulika nayo.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu alimuomba Rais awafikirie kuongeza zaidi majaji, kwa kuwa bado kuna uhitaji mkubwa hasa kutokana na idadi ya majaji hao wapya 12 kufanya kuwe na majaji 78 kutoka 66 wa awali.

“Hata hivyo idadi hiyo inapungua zaidi kwa kuwa majaji wawili wana kazi maalum na wengine wawili watastaafu mwishoni mwa mwaka huu na tunabaki 74,” alisema Jaji Mkuu.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, kila Jaji anashughulia mashauri 518 kwa mwaka wakati uwezo ni mashauri 220 kwa kila Jaji kwa mwaka. JPM na majaji na wateuliwa wengine Akizungumza na Majaji, Rais Magufuli aliwataka kuzingatia viapo na kufanya kazi yao ya ujaji, huku wakitambua kuwa mwenye mamlaka ya hukumu ni Mungu na wao hapa duniani wamepewa dhamana hiyo, hivyo wakatoe hukumu ya haki.

“Pia haki msizicheleweshe, changamoto tunayo katika maeneo mbalimbali. Najua Jaji mmoja wenu hapa (Deo Nangela) alitaka kufukuzwa katika Tume ya Ushindani. Alisimamia haki, walimshangaa asiyependa rushwa, mchezo ukachezwa afukuzwe, ulikaa nje kidogo (huku akimwangalia Jaji Nangela aliyekubaliana na Rais kwa kutingisha kichwa).

“Alisimamia haki huko leo ni Jaji, amepitia changamoto nyingi na kila mmoja wenu amepitia changamoto zake, nendeni mkatumikie wanyonge, haki zao zinapotea,” alisisitiza rais.

Alimtaka Mwenyekiti mpya wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mathew Mwaimu na Makamishna wa Tume hiyo walioapishwa wakatimize wajibu wao kwa uhuru na uwazi na kuhakikisha wanaangalia haki za watu walionyimwa haki.

Kwa upande wa RAS, alimpongeza kwa kufanya kazi kubwa akiwa Msajili wa Mahakama na kumtaka nguvu kubwa zaidi aielekeze Njombe ili kuisaidia Serikali na mkoa huo wenye hazina na rasilimali nyingi kukua kiuchumi.

Magufuli alimtaka Kamishna wa Kazi, Francis Mbindi, mwenye cheo cha Kanali katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kushughulikia vibali hewa vya wageni wanaoingia nchini na kuchukua nafasi za kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.

“Pale kuna vibali hewa, watu wanaletwa kufanya kazi, wanaendesha ‘magreda’ wanauza chipsi, Mheshimiwa Malata (Gabriel aliyeteuliwa kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali) alifanya kazi kazi nzuri, nimeangalia kote nikaona hapa panahitaji mwanajeshi, umepitia vyuo vya kijeshi, umefanya kazi nzuri East Africa, Kanali sasa kawanyooshe Wizara ya Kazi,” alisema Rais.

Aliongeza; “Malata alilalamikiwa kwa mengi, nataka wewe ukalalamikiwe zaidi. Ile ofisi ukaisimamie kweli kweli, vibali vya hovyo hovyo, vya kugushi, wanashirikiana na wizara nyingine. Kasimamie,” alimwagiza Kamishna wa Kazi, Mbindi.

Kuhusu Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Aisha Amour, alimtaka akahakikishe misaada zaidi nchi ikapate kutoka Kuwait na kumuhakikishia kuwa kwa kuwa yeye ni Mhandisi, ana imani Tanzania itanufaika zaidi. Utouh atoa neno Kwa upande wake, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mstaafu, Ludovick Utouh amewataka watanzania kujenga tabia ya kusoma sheria, badala ya kuzungumza au kulishwa mambo wasiyofahamu. Utouh aliyasema hayo wakati alipohojiwa katika kipindi cha Power Breakfast, kinachorushwa na Redio Clouds.

Alisema hawezi kuzungumzia kwa undani suala la uteuzi na kutenguliwa kwa CAG, isipokuwa sheria iko wazi kuwa kila CAG kwa mujibu wa sheria, anatakiwa kutumikia miaka mitano na baada ya hapo anaweza kuendelea au kung’atuka.

Pamoja na hayo, Chama cha Mapinduzi wilayani Tarime kimempongeza kwa dhati Rais John Magufuli kwa kumteua aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Kichele kuwa CAG. Pongezi hizo kwa Rais Magufuli zilitolewa jana jijini hapa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Ngicho alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 utarejea tena Juni ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi