loader
Picha

MIAKA MINNE YA MAGUFULI Mengi aliyoahidi yametekelezwa

KWA miaka minne ya kuwa madarakani, Rais John Magufuli ametekeleza mambo mengi ambayo aliyaahidi wakati akiingia madarakani Novemba 5, 2015.

Katika hotuba yake kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Novemba 20, 2015 mjini Dodoma, Rais Magufuli alieleza jinsi mwelekeo wa serikali yake ya Awamu ya Tano utakavyokuwa.

Aliweka msimamo wa jinsi anavyotaka kuibadili Tanzania kwa kufanya mambo mbali mbali, huku akiahidi kuwa yote ambayo aliahidi kwa Watanzania wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu huo, atayatekeleza.

“Niwahakikishie tu wananchi kuwa mambo tuliyowaahidi tutayatekeleza. Sikusudii kurejea mambo yote niliyoahidi katika hotuba yangu hii ya leo, lakini nataka niwatoe wasiwasi kabisa kwamba tuliyoahidi tumeahidi na ahadi ni deni,” alisema Rais Magufuli wakati wa hotuba.

“Nataka wananchi mniamini kuwa sikutoa ahadi ili tu mnipigie kura, niliahidi kuwatumikia na kuwafanyia kazi, na hicho ndicho nitakachofanya. Ni imani yangu kwamba waheshimiwa wabunge na madiwani pia watafanya vivyo hivyo kama tutakavyofanya sisi,” aliongeza Rais Magufuli.

Katika mambo muhimu aliyoyazungumza katika hotuba yake hiyo ilikuwa ni baadhi ya maeneo yaliyolalamikiwa wakati wa kampeni, ambayo baadhi ni rushwa, ardhi (migogoro ya wakulima na wafugaji), bandari (rushwa, urasimu na ubadhirifu), maji (kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama, na huduma ya maji kupatikana mbali na makazi ya watu).

Nyingine ni huduma za afya – hospitali (huduma kuwa mbali na wahitaji, ukosefu wa dawa, hujuma kwenye vifaa vya vipimo, msongamano wa wagonjwa na tozo zisizostahili, lugha mbaya za watumishi kwa wagonjwa, uhaba wa majengo, vitendea kazi, rasilimali watu na fedha, kushindwa kukusanya mapato yanayowahusu, n.k.) Pia Uhamiaji na ajira (kutoa hovyo hati za uraia, vibali vya kuishi nchini kwa wageni, kushindwa kusimamia ajira za wageni hususan kwa kazi zinazoweza kufanywa na wazawa, elimu (uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, michango mingi isiyo ya lazima, malalamiko ya walimu yasiyoisha, mazingira ya kusomea ikiwa ni pamoja na majengo, madawati, ukosefu wa nyumba za walimu).

Eneo jingine ni Polisi (malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi, upendeleo, madai ya askari, ukosefu wa nyumba za askari, ukosefu wa vitendea kazi vya kisasa); madini (wenyeji kutofaidika, vilio vya wachimbaji wadogo kutengewa maeneo ya uchimbaji na kupatiwa mikopo, kutolipa kodi stahiki, usumbufu kulipa fidia.

Alizungumzia pia ATCL – Kampuni ya Ndege Tanzania (shirika lipo, wafanyakazi wapo zaidi ya 200, na wanalipwa mishahara ila ndege ni moja, Makundi Maalumu (Haki za wazee, walemavu, wanawake na watoto zimekuwa zikikiukwa na wafanyakazi, wasanii na wanamichezo (mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, haki na maslahi yao)..

Lakini licha ya hayo, Rais Magufuli alizitaja baadhi ya kero ambazo serikali yake ingeshughulika nazo kuwa ni kuimarisha Muungano, kuimarisha mihimili ya serikali, uchumi na Matarajio ya wananchi, ujenzi wa viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi, tatizo la ajira na umaskini, afya, elimu, maji, dawa za ku-levya, umeme, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi na kuongeza mapato na kupunguza matumizi ya serikali.

Kwa miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, Rais Magufuli ametembea katika karibu mambo yake mengi aliyoyaahidi katika hotuba yake hiyo kwa Bunge, Novemba 20, 2015. Kwa mfano, katika suala la mapambano ya rushwa na ufisadi, hakuna ubishi kuwa Rais Magufuli amekuwa mkali katika hili.

Ameanzisha mahakama maalumu ya kushughukilia ‘saratani’ hii kwa kuwapo kwa Mahakama Maalumu ya Makosa ya Uhujumu Uchumi ambayo siyo tu baadhi ya vigogo waliokuwapo serikalini wamefikishwa mahakamani, bali hata wafanyabiashara wakubwa nchini, wameburuzwa kortini. Kokote ambako Serikali ya Rais Magufuli imehisi kuwapo kwa rushwa, amechukua hatua kali na za haraka.

Hili linathibitishwa na kuimarika kwa utoaji wa huduma katika taasisi za serikali zikiwamo zile ambazo zilikuwa zimekubuhu kwa rushwa kiasi cha wanyonge kushindwa kupata haki zao.

Katika hotuba yake ya bungeni, Rais Magufuli alisema, “Jambo moja nililolisemea kwa nguvu kubwa wakati wa kampeni ni mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Sikufanya hivyo kwa sababu nilitaka tu kuwarubuni wananchi ili wanipe kura zao na kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili kwa dhati kabisa, na nilichokisema na kuwaahidi wananchi ndicho hasa nilichokikusudia.”

Aliongeza, “Mheshimiwa Spika, mimi nimewaahidi wananchi, na nataka niirejee ahadi yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua majipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu, lakini bahati mbaya halina dawa nyingine. Hivyo ninaomba waheshimiwa wabunge na Watanzania wote mniombee na muniunge mkono wakati natumbua majipu haya.”

Rais Magufuli ametumbua majipu, tena mengine yalikuwa yamejaa usaha ambao unaweza kukurukia mdomoni, lakini hakujali na amefanya hivyo kiasi kwamba sasa rushwa imeanza kuogopwa kama ukoma.

Mfano mwingine wa Rais Magufuli kutembea katika maneno yake ni azma ya Tanzania kuifanya kuwa nchi ya uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025. Amelibeba hili na serikali yake na sasa viwanda vikiwamo vikubwa, vidogo na vya kati vikichanua kila mahali nchini, kiasi kwamba pia limesaidia kuanza kupunguza tatizo jingine la ukosefu wa ajira na umaskini nchini.

Katika maonesho ya viwanda yaliyomalizika karibuni mkoani Pwani, watu wameshuhudia wingi wa viwanda vipya vilivyojengwa katika mkoa huo na kujionea bidhaa nyingi ambazo wengi walidhani zinazalishwa nje kumbe ni Tanzania. Sambamba na hili, ameifufua Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), ambayo hivi karibuni tu amepokea ndege ya nane, ambazo zote zimenunuliwa kwa fedha za walipa kodi, hivyo kusaidia kuitangaza nchi na pia zinategemewa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini.

Serikali ya Rais Magufuli imeongeza mapato na kupunguza matumizi yake kwa kiasi kikubwa kwa kubana safari zisizo za lazima, kuondoa wafanyakazi hewa ambao kabla ya hapo, serikali ilikuwa inalipa Sh bilioni 777 kwa mwezi kwa mishahara, lakini kwa takwimu za mwaka jana kabla ya kuanza kuajiri upya ilikuwa inatumia Sh bilioni 251 tu kwa mwezi kwa mishahara.

Fedha hizi zilizookolewa kwa mishahara hewa na maeneo mengine yakiwamo ya rushwa na ufisadi, ndizo ambazo zimeisaidia nchi kuendesha miradi ya maendeleo, ikiwamo ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), barabara katika maeneo mbalimbali, madaraja, kuboresha elimu, na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu; mambo ambayo aliyaahidi Rais Magufuli miaka minne iliyopita alipochaguliwa kuingia Ikulu ya Magogoni.

Kuthibitisha jinsi Rais Magufuli anavyotembea katika maneno yake na kufanikisha aliyoyaahidi, Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Dk Kitila Mkumbo alieleza katika kongamano la hali ya siasa na uchumi lililofanyika UDSM mwaka jana kuwa serikali hiyo ilikuta machache mazuri kutoka kwa ile ya awamu ya nne na kuyarithi, lakini ilikutana na changamoto nyingi pia.

Kwa mujibu wake, changamoto kubwa iliyoonekana katika awamu ya nne, uchumi ulikuwa unakua, lakini pia kupunguza umaskini, siasa kufanywa kuwa biashara, kukithiri kwa rushwa na ufisadi na watu kuishi kiujanjaujanja. Alisema katika miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano, imejipambanua kulinda mafanikio ya uchumi yaliyofikiwa na awamu iliyopita.

Alisema mambo mengine ni kusimamia weledi katika utumishi wa umma na kukomesha mfumo wa watu kuishi kiujanjaujanja. Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mambo matano makubwa ambayo ni pamoja na kuonesha ujasiri wa kufanya uamuzi sahihi kwa wakati. Alisema jambo jingine ni kufanya uamuzi sahihi bila kujali gharama za kisiasa za muda mfupi, kuonesha uwezo mkubwa katika kufuatilia utekelezaji wa shughuli za serikali, kuwajibisha watendaji wabovu bila woga wala upendeleo na kupambana na rushwa.

Pia alisema Rais katika kipindi kifupi amefanikiwa kuvuruga kabisa mtandao wa wapiga dili serikalini waliokuwa wakiishi kiujanjaujanja, suala ambalo tunastahili kujivunia. Katika kuhakikisha rasilimali za nchi zinanufaisha Watanzania, eneo moja wapo ambalo amelishughulikia vizuri pia ni la madini. Amebadilisha sheria ili kuhakikisha wachimbaji wakubwa hawatuachii mashimo, kuboresha mifumo ya kukusanya mapayo na kuhakikisha wachimbaji wadogo wanalipa kodi stahili ikiwa ni pamoja na kuanzisha masoko ya madini katika mikoa mbalimbali.

TUME ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) imevitaka vyuo vikuu vyote ...

foto
Mwandishi: Mgaya Kingoba

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi