loader
Picha

Kichere atema cheche, Profesa Assad afunguka

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mpya, Charles Kichere ameanza kazi rasmi jana na kuzitaka taasisi na idara za serikali kukaa mguu sawa, kwani hatofumbia macho madudu na ubadhirifu wa fedha pindi ofi si yake itakapobaini.

Wakati Kichere akieleza msimamo wake, CAG aliyemkabidhi kijiti Profesa Mussa Assad amewaomba radhi wote aliowakwaza katika kipindi chote cha utendaji wake wa kazi na kusema hakuwahi kufikiri kama angeweza kutengeneza adui wakati wa utekelezaji wa kazi yake. Sambamba na kauli hiyo ya CAG, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Profesa Adelardus Kilangi ametoa ufafanuzi juu ya mjadala unaoendelea nchini kuhusu uteuzi wa CAG Kichere na kusema unapotoshwa na kubainisha kuwa hakuna sheria wala Katiba iliyovunjwa kutokana na uteuzi huo.

Kichere alisema anajua ugumu wa kukusanya mapato kwani alishakuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) na akayaona, hivyo hatakuwa na simile kwa watakaovurunda kwa kufanya madudu ya fedha kwa mashirika, idara na taasisi za serikali.

“Nitahakikisha nalinda kihenge, nimefanya kazi TRA najua ugumu wa ukusanyaji mapato, nitakuwa na wivu mkubwa na kulinda mapato ya nchi, sitakuwa na simile kwa watu ambao wanatumia mapato ya serikali vibaya, nitawaripoti ili hatua stahiki zichukuliwe,” alisema Kichere.

Alisema pia atahakikisha anafanya kazi yake kwa weledi na kutoa mawazo chanya yatakayoimarisha mifumo, ili mambo yaende vizuri. Kichere aliyasema hayo jana baada ya kuripoti kwenye ofisi yake mpya iliyopo Samora na kukabidhiwa rasmi ofisi na CAG wa zamani, Profesa Assad. Kichere alimshukuru Profesa Assad kwa mapokezi aliyompa na kumuahidi kujenga taasisi imara.

“Profesa Assad ni mwalimu wangu, nilimfahamu kwa mara ya kwanza mwaka 1994 nilipojiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka wa kwanza akiwa miongoni mwa walimu waliotupokea na kutufundisha. Najiunga na ofisi hii kufanya kazi za wananchi wa Tanzania kuangalia mapato ya nchi yanatumikaje kwa lengo la kuleta maendeleo,”alisema.

Alisema kazi kubwa iliyopo mbele yake ni kuhakikisha anadhibiti na kukagua hesabu za serikali, kuhakikisha mapato ya nchi yanatumika vizuri kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Aliahidi kuendelea kuifanya kazi aliyofanya Profesa Assad na timu yake kwa weledi na kuahidi ushirikiano mzuri kwa wafanyakazi wote.

Alimweleza Profesa Asaad kuwa atakapobisha hodi kuhitaji msaada wake asisite kumfungulia mlango. Mgogoro ofisi ya CAG na Bunge: Akizungumzia kulegalega kwa mahusiano kati ya ofisi ya CAG na Bunge, Kichere alisema mkakati mmojawapo alionao ni kuimarisha mahusiano ya ofisi yake na bunge ili waweze kufaya kazi vizuri.

“Kama kulikuwa na kulegalega basi nitakwenda kuimarisha kwa sababu huwezi kufanya kazi ya udhibiti bila kuwa sawa na bunge lenye kazi ya kuishauri na kusimamia serikali. CAG anapeleka ripoti bunge liifanyie kazi. Ni lazima tuwe na mahusiano mazuri na ushirikiano ili mambo yaende sawa,”alisema.

Aprili 2, mwaka huu Bunge la Tanzania liliazimia kutofanya kazi na Mkaguzi na aliyekuwa CAG, Prof Assad baada ya kudai amekidharau chombo hicho. Wakati akikabidhi ofisi hiyo, Profesa Assad alisema makabidhiano hayo ni ya mfano na kwamba rasmi yatafanyika Dodoma kimaandishi ambako ndipo makao makuu ya ofisi hiyo yapo. Amewaomba radhi wote aliowakwaza katika kipindi chote cha utendaji wake wa kazi.

Alisema hafahamu na hakuwahi kufikiri kama angeweza kutengeneza adui wakati wa utekelezaji wa kazi yake, hivyo anaona ni vizuri kusameheana kama kuna yeyote alimkosea kwenye utendaji wake wa kazi. Aidha, alimtahadharisha Kichere kuhusu kubadili watumishi na kusema inamdidi awe muangalifu sana kuepuka kusababisha uharibifu utakaoigharimu taasisi kwa sababu hadi kufikia kuwa msaidizi wa CAG maana yake mtumishi anakuwa amejifunza kwa miaka mingi sana.

“Mimi si muumini wa kuingia mahali na kutoa watu wote niliowakuta na kutengeneza timu mpya, kufanya hivyo uharibifu mkubwa unaweza kutokea na itagharimu kwa taasisi kama hii ambayo mtu anajifunza kwa miaka mingi sana kufikia kiwango cha DAG (wasaidiazi wa CAG), Mtu amekaa kwa miaka 10 hadi 15 ndio anapata nafasi hiyo, huwezi tu kumteua mtu na kumweka, uwezo wake ni muhimu sana kuuhamisha kwa mwingine, ukifanya mabadiliko ya haraka utapoteza kumbukumbu ya taasisi na itakuwia vigumu kufanya kazi,”alimwambia Kichere na kuongeza: “Taasisi ina mifumo yake na sheria zake, sera zake na namna zake za kuiendesha, namna zote inasimamiwa na watu na watu hawa ndio walionisaidia kufanya kazi, sifa kubwa zitakuja lakini watu wa chini ndio watendaji wakuu wa kazi za kila siku, ni lazima uwatizame vizuri”.

Alisema ukitazama taasisi za ukaguzi zote wanazofanya ni kujengea watu uwezo na taasisi hiyo pia ina mfumo wake wa kuwachukua vijana vyuo vikuu na kuwajengea uwezo na kuwa bora zaidi. Alisema mfumo wa taasisi hiyo hakuna inayoweza kushindana nayo na kwamba wanashirikiana na taasisi za nje hususani Afrika Kusini na wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wafanyakazi kila baada ya miezi miwili ili kuwajengea uwezo zaidi. Kwa miaka mitano aliyokuwa CAG alifanya kazi ya kujenga mahusiano ambayo hayafutiki na iwapo watahitajiana basi milango yake ipo wazi.

Nitakuwa mkulima wa bamia Mara baada ya kukabidhi nyaraka mbalimbali ikiwemo Sheria ya Ukaguzi, ripoti ya Sera ya Rasilimaliwatu na ripoti moja ya ukaguzi, alisema kichwani kwake kwa sasa anafikiria kuwa mkulima mdogo.

“Kwa muda mrefu mimi kichwani kwangu nafikiria kuwa mkulima mdogo, miaka yote napenda nipande bamia, nilisimamie liote, nivune bamia langu liingie jikoni nile,”alisema.

Alisema miezi miwili iliyopita alishaanza kuwekeza kwenye kilimo na kwamba anakwenda kuishi shamba na iwapo watu wa mjini wakimuhitaji atakuja. Alisema alikutana na changamoto nyingi.

Rais Magufuli juzi alimteua aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Charles Kichere kuwa CAG mpya na kumuapisha rasmi jana akishika nafasi ya CAG wa saba tangu Tanzania kupata Uhuru akichukua nafasi ya Profesa Assad aliyemaliza kipindi chake cha miaka mitano jana.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 utarejea tena Juni ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi