loader
Picha

Labda tunahitaji lugha za malaika kumwelewa JPM

NIMEKUWA nikisoma baadhi ya magazeti na mitandao ya kijamii ambayo ina mambo mengi yanayohusu serikali ya Dk John Magufuli, magazeti mengi na baadhi ya mitandao ya jamii imekuwa ikijaribu kueleza mafanikio ya serikali ya awamu ya tano ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais John Magufuli.

Hata hivyo, baadhi ya magazeti na mitandao ya kijamii imekuwa na tabia au kasumba ya kuchafua mafanikio ya serikali ya awamu ya tano yaliyopatikana na yanayoendelea kupatikana. Kutokana na changamoto hiyo nimeamua kujadili baadhi ya mafanikio ya serikali ya awamu ya tano ambayo yametokana na uongozi makini wa Dk John Magufuli.

KUMWELEWA MAGUFULI

Lengo la makala haya si kusifia yaliyofanywa na serikali ila kuwafahamisha watanzania wenzangu umuhimu wa kumwelewa Rais kwa juhudi zake za kujitolea katika kuijenga nchi hii kimaadili, kiuchumi, kisiasa, kifkra na kijamii.

Nafahamu kuwa haiwezekani wote tuwe na fikra zinazofanana isipokuwa tuwe na hoja kila tunapotaka kupinga na kuchafua serikali ya awamu ya tano. Nitataja mambo machache ambayo serikali hii imeyafanya na inayatekeleza hivi sasa ambayo yalishindikana huko nyuma. Haya nitakayoyajadili yamewezekana kwa sababu ya uwepo wa Dk Magufuli katika ikulu yetu.

SEKTA YA MADINI

Mosi, kwa takribani miaka 20 iliyopita (1995- 2015) sekta muhimu ya madini ilikuwa haichangii vya kutosha katika pato la taifa. Kila wakati makampuni haya ya kibeberu yalikuwa yanadai kupata hasara na hivyo yalikuwa hayalipi kodi. Wachimbaji wadogo nao walikuwa hawachangii cha maana katika mapato ya serikali.

Hata hivyo, tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini katika wilaya na mikoa mbalimbali mchango wa pato la madini unaonekana katika pato la Taifa. Makampuni yaliyowekeza leo hii yanalipa kodi na ‘hayazalishi hasara’ tena kama walivyotuaminisha hapo zamani. Hivi karibuni kampuni kubwa ya madini duniani ya Barick Gold Mine wameweza kuigawia serikali ya Tanzania hisa ambapo zamani isingewezekana.

Kwa hili Rais Magufuli tunakupongeza kwa kuonesha dunia kuwa rasilimali za Tanzania ni ya watanzania na Tanzania ni tajiri. Hata kama amekugusa na ulikuwa unafaidika na mapato ya madini wewe na familia yako kwa kutolipa kodi, nyamaza sindano iingie.

UFISADI DHIDI YA RASILIMALI ZA UMMA

Pili, eneo ambalo lilikuwa linasumbua serikali huko nyuma ni kashfa mbalimbali za matumizi mabaya ya fedha za Umma. Kashafa hizi enzi hizo zilikuwa zinaitwa UFISADI. Mfano ni kashfa ya EPA, kashfa ya Esrow, kashfa ya Richmond, IPTL TICS na kadhalika. Tangu serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Dk John Magufuli ianze kazi, kashfa hizi hatuoni zikiibuka na hizo alizozirithi, hatua zinachkuliwa pale panapostahili huku wale ambao walionekana ni mwiba kuwagusa, wakishughulikiwa pia.

Waliohujumu uchumi wamerudisha fedha za umma. Tumesahau lini kuwa baadhi ya majina ya watuhumiwa wa uhujumu uchumi walikuwa wanaogopwa hata na serikali? Tangu Dk Magufuli aingie madarakani hakuna tajiri wala maskini mbele ya sheria, watu wote wamekuwa watii wa sheria na wananchi wanyonge wameendelea kupata haki zao. Mnyonge mnyongeni lakini Dk Magufuli tumpe haki yake na tumwombee mazuri kwani amerudisha nchi kwenye reli salama.

Mimi niliporipoti kwa mara ya kwanza kama mkuu wa wilaya, kuna tajiri nilimwita, nikamwambia arudishe maeneo ya wananchi aliyopora. Akaniambia kuwa hawezi kurudisha na sina la kumfanya. Lakini nilipomtupa rumande alianza kulia na akarudisha maeneo ya wananchi.

Haya yalikuwa hayawezekani huko nyuma kwa sababu wanakushitaki huko wanakojua wao. Leo hata viongozi wa chini tunafanya uamuzi kwa sababu Rais Magufuli ameondoa kabisa ule mfumo wa kuwa na miungu watu kutokana na utajiri wao, vyeo au sifa zao katika jamii. Sambamba na hayo, rushwa serikalini na taasisi zake imepungua sana.

Watoaji na wapokeaji wanajitafakari sana kwa suala la rushwa kinyume na hapo nyuma ambapo rushwa ilikuwa inaombwa waziwazi na kuwa kama sehemu ya maisha. Nchi mbalimbali sasa zinatoa mfano wa Tanzania zinapozungumzia mapambano dhdi ya rushwa. Katika kumaliza saratani hii, Dk Magufuli ametusaidia sana kama taifa na sasa wananchi wanyonge wanasikilizwa na kuhudumiwa bila kulazimika kutafuta hongo.

KUMALIZA MGAWO WA UMEME

Tatu, kitu kingine ambacho JPM amefanya uamuzi mgumu ni kutatua tatizo la mgawo wa umeme na ununuzi wa mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme. Hiki kilikuwa kichaka kikubwa cha ufisadi nchini. Kulifanyika hujuma katika mfumo wa usambazaji umeme kwa kukatwa kwa makusudi ili watu wanufaike na mafuta. Halikadhalika mabwawa ya kuzalisha umeme yalitapishwa maji kwa makusudi ili ionekane maji hayatoshi na mgawo wa umeme kuanzishwa mapema.

Tangu Dk John Magufuli aingie madarakani mgawo wa umeme umeisha na hakuna mjadala kuhusu suala la upatikanaji wa umeme. Tukumbuke wakati huo kulikuwa na siasa ya uchumi wa gesi ili kuzalishwa umeme kupitia miradi kama ule wa Symbion Power ambao mtu hupewa tenda ya kuzalisha umeme wa dharura na kama hajazalisha analipwa kitu kinachoitwa ‘capacity charges’. Haya yanaendelea kubaki historia.

Enzi hizo magazeti kila siku yalikuwa na habari kuhusu sekta ya umeme hasa ubadhirifu uliokuwa unatendeka lakini hakuna aliyekuwa anashituka. Siku hizi serikali ya awamu ya tano imeondoa tatizo la mgao wa umeme na wigo wa upatikanaji wa nishati ya umeme umeongezeka. Tatizo litaisha kabisa ifikapo mwaka 2022 baada ya kukamilika kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere katika mto Rufiji.

Bwawa hili la kwanza kwa ukubwa Tanzania, la nne kwa ukubwa barani Afrika na la tisa kwa ukubwa duniani linajengwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania. Kwa hili pia bado tunaendelea kutoisemea vizuri serikali ya Magufuli? Kama mnashindwa kuelewa hili pia kiasi cha kusikia watu kama Zitto Kabwe wakipinga basi wanahitaji lugha za malaika kumwelewa Magufuli. Hongera Dk John Magufuli kwa kufanya mambo sahihi.

KUHAMIA DODOMA

Nne, ni kuhamisha Makao Makuu ya serikali kwenda Dodoma. Wazo la kuhamia Dodoma liliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere miaka 1970 na kupitishwa na Kamati Kuu ya Chama cha TANU wakati huo. Mwaka 2012 nilisoma makala ya mwandishi nguli nchini, Jenerali Ulimwengu, aliyoipa kichwa cha habari ‘Tukifanya upuuzi juu ya Katiba, tutakuwa tunarudia upuuzi juu ya kuhamia Dodoma,” akizungumzia suala hilo.

Katika makala yake alijadili mambo mengi kuhusu serikali kukosa uamuzi katika mambo mbalimbali lakini akatolea mfano wa kuhamia Dodoma kuonesha kuwa Serikai ilikuwa inasema itafanya jambo A lakini inatekeleza jambo B.

Ulimwengu alisema, ninanukuu: “Mfano mmoja ni riwaya kuwa Makao Makuu ya nchi kuwa Dodoma, baada ya uamuzi uliofanyika miaka takribani 40 iliyopita. Hadi leo baada ya miaka 40 hii imebaki ni riwaya. Makao makuu hayako Dodoma wala wakuu hawakai Dar es Salaam. Wamo safarini siku zote kati ya Dodoma na Dar es Salaam,” mwisho wa kunukuu.

Nimeamua kurejea hoja hii ya mwaka 2012 kudhihirisha ujasiri, uzalendo na uwezo wa Rais Magufuli katika kufanya maamuzi ambayo kwa miaka 40 yalishindikana kufanywa. Wale ambao bado mnadhihaki Serikali ya Dk Magufuli mnapaswa kuelewa hili kwamba vitu vinatokea kwa sababu Magufuli ni jemedari wa kufanya maamuzi na uthubutu wa hali ya juu. Tunahitaji kumwombea na kumtia moyo aendeleze kasi hiyo hiyo.

UJENZI RELI YA KISASA

Tano, Dk Magufuli ameamua kujenga reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi mpakani mwa Rwanda kwa fedha za ndani. Uamuzi huu ni uamuzi mgumu katika kujifunga mkanda ili kuutekeleza. Hapo awali shirika la reli lilikosa mwelekeo na lilibaki kama sehemu ya kuzalisha migogoro kama ule wa wafanyakazi wake kudai maslahi yao. Leo hii shirika limefufuka na linaendelea kuzalisha.

Uwezo wa kuamua jambo na kulifanyia kazi hata kama kuna vikwazo ni uamuzi wa kijasiri wa Dk Magufuli. Katika ujasiri wake ameionesha dunia kuwa watanzania wanaweza kujiletea maendeleo yao wenyewe.

Kutokana na kuwa kiongozi wa uamuzi mgumu na yenye busara hivi sasa wale waliofikiri haiwezekani wanamtembelea Ikulu na wanaleta misaada wenyewe badala hapo zamani tulikuwa tunaifuata Washington, Geneva, Paris, London n.k. Mheshimiwa Rais wetu, piga kazi, wale wenye husuda wa ndani na nje ya nchi watapanda SGR iliyojengwa kwa fedha za watanzania na wataandika vitabu kuifunza dunia maono yako.

KUFUFUA SHIRIKA LA NDEGE

Sita, ununuzi wa ndege kwa ajili ya kufufua shirika letu la ndege, ATCL. Uamuzi huu uliodhihakiwa na wanasiasa na baadhi ya wananchi wasioitakia mema na mafanikio ya serikali ya awamu ya tano sasa wamebaki vinywa wazi. Ununuzi wa ndege za ATCL ni uamuzi mgumu ambao kama nchi ingeendelea kuongezwa na mtu asiyekuwa na uamuzi isingewezekana.

Nilikuwa nikifuatilia mijadala kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii wakati Bombardier zilipowasili baadhi ya watu walikuwa wanaziponda zinapopata changamoto. Mfano, hata ikichelewa kuondoka au kufika habari kuu katika mitandao ya kijamii ni kushambulia ndege hizi za shirika letu la umma.

Madalali hawa wa kuchafua Serikali wakawa wamesahau kuwa huko nyuma unaweza kufika uwanja wa ndege ukakuta ndege imeahirisha safari au imechelewa na mengine kama hayo kwani ni mambo ya kawaida tu. Maneno haya ya kutafuta ‘vijimakosa’ ili kuishambulia ATCL yakawa yananikumbusha msemo wa wahenga kuwa shukrani ya punda ni mateke. Nampongeza sana Rais wetu kwa msimamo wake wa kuendelea kutekeleza yale anayoyaamini. Kuhuishwa kwa shirila letu la ATCL imetupa heshima kubwa Barani Afrika na duniani. Chapa yetu ya Twiga inapasua anga. Hili limewezekana kwa sababu ya Dk John Magufuli.

UNUNUZI WA KOROSHO

aSaba, ununuzi wa korosho za wakulima. Wakati wa sakata la bei ya korosho madalali na mawakala wao walipiga kelele na kuilaumu serikali kuingilia mchakato wa ununuzi wa korosho. Wakulima walikosa mtetezi mpaka pale Rais Magufuli alipoingilia na kuagiza korosho zinunuliwe kwa kutumia fedha za Serikali zaidi ya bilioni 600 ambazo zilisimamiwa na Benki ya Kilimo Tanzania. Mabeberu mamboleo na mawakala wao waliamini kuwa serikali itashindwa kuwasaidia wakulima ili kuhakikisha mipango ya kuwahujumu wakulima inafanikiwa, walipenyeza hila zao mpaka kwenye vyombo vya kutunga sheria. Naamini kama sio uamuzi jasiri wa Dk Magufuli leo hii wakulima wa korosho wasingekuwa na uwezo wa kulihudumia zao la korosho tena. Kila jambo lina mazuri yake, sakata la korosho limesaidia kufufua viwanda vyetu vilivyohujumiwa huko nyuma na sasa vinafanya kazi na ajira zimeongezeka. UJANGILI Nane, tatizo la ujangili lilisumbua sana serikali za awamu zilizopita na kuanza kuonekana kama sugu lakini limeshughulikiwa vyema zaidi katika Serikali hii ya awamu ya tano. Serikali imeweza kuwa safi kwa sababu kiongozi wake ni msafi, mfuatiliaji na mwadilifu. Mfano, ujangili katika mbuga za wanyama hasa hifadhi za Taifa hapo zamani tembo na faru walikuwa mbioni kupotea kutokana na majangili kutokuchukuliwa hatua stahili. Siku hizi tembo wanafanya utalii katika maeneo ya wananchi badala ya kuwakimbia majangili! Majangili wakifika mahakamani wanakula mvua ya jela, jambo ambalo huku nyuma ilikuwa kiini macho. MABORESHO HUDUMA ZA AFYA Tisa, Rais amefanya uamuzi mgumu na ya busara katika kuboresha sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na suala la matibabu ya nje ya nchi kwa watumishi wa umma. Huko nyuma kila siku watu walikuwa wanakwenda India, Ulaya, Afrika Kusini kupima malaria na kuchunguza chunusi kwa fedha za serikali. Dk Magufuli baada ya kuona hilo ameimarisha ubora wa hospitali za serikali hasa Muhimbili kwa kuhakikisha huduma bora zinapatikana. Mtakumbuka ziara yake ya pili ya kushitukiza mara tu baada ya kuapishwa ilikuwa ni Muhimbili. Ambako alifumua uongozi na kusababisha mabadiliko makubwa ya kiutendaji huku akiagiza mashine ambazo zilikuwa zikihujumiwa kama computerized tomography (CT) scan kutengenezwa. Kwa sasa hospitali zote kubwa mbali na Muhimbili kama vile Benjamin Mkapa Dodoma, Bugando, Mwanza na KCMC, Moshi zimejizatiti kila uchwapo kwa kutoa matibabu ya kibingwa ambayo huko nyuma Watanzania walilazimika kuyafuata nje ya nchi. Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili imeimarisha sana taasisi zake za kitabibu kama ile ya moyo ya JKCI, taasisi ya mifupa (MOI) n.k. Leo hii upasuaji wa moyo unafanyika Tanzania jambo ambalo zamani lazima uende India au Ulaya, kupandikiza figo na matibabu mengine ya kibingwa ya mifupa. Tujitafakari, hivi profesa wa Tanzania wa fani ya utabibu wa Muhimbili ana tofauti gani na profesa wa fani hiyo hiyo wa hospitali ya Apolo ya India? Daktari wa Tanzania na India tofauti yao nini? Hivi kuna tofauti ya mtaala wa udaktari kati ya Tanzania na India? Mimi naamini hakuna tofauti ila sisi tulishindwa kuwekeza katika sekta hiyo ambayo serikali ya awamu ya tano sasa inawekeza. Nafahamu changamoto ya vifaa tiba ambavyo Serikali imeendelea kuwekeza kwa hospitali zote za rufaa za mikoa na kanda sambamba na kuongeza maradufu bajeti ya dawa na vifaa tiba. Pia usimamizi mbaya wa matumizi ya mapato ya Serikali katika sekta ya afya umepungua. Tukifanya tafakuri hii ndiyo maana leo hii huduma imeendelea kuboreshwa katika hospitali za umma. Maendeleo yoyote duniani yanaanzishwa au yanaasisiwa na mtu ambaye ni kiongozi au mvumbuzi. Dk John Magufuli ni kiongozi aliyejaaliwa kuasisi fikra za kimaendeleo kwa ajili ya jamii. Napenda kuwafahamisha wasomaji kuwa lengo la kuandika makala haya si kusifia kazi za serikali ya JPM, ila kuelezea ukweli kuhusu serikali hii chini ya jemedari wetu huyu. Ukweli huu nauelezea ili watanzania na dunia wafahamu kuwa uongozi wa serikali ya Tanzania ni uongozi wa kufanya uamuzi wa kimaendeleo. Kimsimgi, kuyaandika yote yaliyofanywa na awamu ya tano katika kipindi kifupi tunaweza kujaza gazeti zima. Nimeacha kuyasemea mengi tu kama vile maendeleo katika sekta ya barabara, maji, kilimo, mifugo, uvuvi, elimu pasipo malipo, amani na utulivu, ukasanyaji wa mapato. Nimeamua kujadili haya machache ambayo yalikuwa yameshindikana huko zamani. Watanzania wenzangu, Dk Magufuli ni Rais wa maamuzi. Ambao hawataki kumwelewa basi hata kwa lugha za malaika hawatamwelewa. Mimi naamimi kuwa inawezekana wanazikubali kazi zake ila roho zao zimejaa husuda dhidi ya Rais na Chama Cha Mapinduzi au walikuwa wakinufaika na mfumo wa hovyo uliokuwepo huko nyuma. Hivi sasa wamebaki kuvumisha uongo dhidi ya Rais na pia kuvuzia vijimakosa vya kibinadamu na kupayuka navyo. Pia naamini bila uongozi makini wa Dk Magufuli watanzania tutabaki maskini na tutaendelea kunyonywa na mabeberu huku tukiwalamba miguu.

MAFUNZO ya uongozi na usimamizi wa elimu ni ...

foto
Mwandishi: Vicent Anney

Weka maoni yako

1 Comments

  • avatar
    Majura Songo
    07/11/2019

    Mh. Naomba ushughulikie mgogoro wa ardhi kwenye shamba letu ambapo Ndugu Mashauri amejimilikisha shamba la ekari 42 bila ridhaa yetu. Huu ni uonevu wa wanyonge na swala hili lilushafikishwa mezani kwako na hakuna hatua zilizochukuliwa. Jesus hapo kuna haki kwa mnyonge. Tunaomba uchukue hatua.

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi