loader
Picha

CCM yatoa onyo, Chadema yajitoa

CHAMA cha Mapinduzi(CCM) kimetoa onyo kwa serikali kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa, kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi, kwa kufuatilia mchakato wa ndani wa uchaguzi kwa vyama vya siasa.

Wakati CCM inatoa onyo hilo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kimetangaza kujitoa kwa asilimia 100 katika ushiriki wa uchaguzi wa serikali za mitaa, utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu.

Pia, Chadema kimewataka wagombea wa chama hicho ambao wamepitishwa, kutoshiriki uchaguzi huo na kwa wale waliokata rufaa, waachane na rufaa hizo. Kujitoa kwa Chadema, kunatokana na maazimio yaliyofikiwa kwenye kikao cha wabunge wa chama chicho na Kamati Kuu ya chama hicho, jana mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe ambapo walijadili washiriki uchaguzi huo au la.

Onyo la CCM limetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole jana wakati akizungumza na waandishi wa habari. Polepole alisema kuwa vyama vya upinzani, vingi havikufuata sheria na kanuni za uchaguzi, kama inavyoelekeza.

Polepole alisema “Uchaguzi huu unaongozwa kwa sheria na kanuni, wenzetu walijua uchaguzi ni shamrashamra, hawakuwekeza, ipo kanuni hapa ya uchaguzi ina kurasa 194 unatakiwa kusoma na kuzingatia, mle kuna viapo na fomu zenyewe, kama hukujiandikisha unapoteza sifa ya kuwa mgombea. Na wengine hawakuwa na mchakato kabisa, walikaa kimya, mfano mkoa wa Arusha ambao mimi ninaulea, wengi ni watu wa nongwa, wanasubiri kama fisi mkono urudi nyuma udondoka chini halafu wao waudake wapate wagombea. Hivi unawezaje kuwa na chama ambacho kinasubiri wagombea wabovu wa CCM waenguliwe ndio wawape dhamana?” alihoji.

Aliongeza:”Tunayasema haya ili wajue kwa nini hawakuwa na mchakato wa ndani. Tunaitaka serikali kupitia kwa msajili wa vyama vya siasa, sheria inamtaka ajiridhishe na mchakato wa kila chama, wa ndani wa kupata wagombea wa uchaguzi huu. Polepole alisema vyama vya upinzani vinawakosea Watanzania, kwani vinahitaji kuwekeza na kuwa taasisi imara na kutoa aina ya watu ambao wataweza kutoa viongozi katika nchi. Alikosoa ujazaji fomu wa baadhi ya wagombea wa upinzani, ambao asilimia kubwa wameenguliwa, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukosa sifa. Akifafanua, Polepole alisema kuna vyama vimepeleka fomu vijijini zina majina yake kwa mujibu wa sheria na yameandikwa kwenye matangazo ya serikali. Lakini, mgombea anaulizwa anataka kugombea kijiji gani anaandika kijiji anachokijua yeye, mfano “mtaa ni ‘Sinza A’ sasa kwa kuandika kwa presha zake anaandika ‘Sinzaa’ pale anakuwa amekosa sifa,”alisema.

“Serikali chonde chonde tutaonana wabaya, kila chama tulikubaliana kiseme ni ngazi ipi itadhamini mgombea, sisi tulisema ngazi ya tawi ndio itakayodhamini mgombea na kuna muhuri, lakini wenzetu watani wa jadi kule chini hawapo, si mkubali ngoma imeshaisha tukutane kwenye ubunge na udiwani, Kuna chama (Chadema) tumesikia mnaomba huruma, muhuri wa taifa utumike kwenye matawi, serikali chondechonde, sheria ni msumeno, anayekwenda kinyume sababu ya ujinga wake hakuwekeza kwenye elimu, tusiwaruhusu” alisema.

Alisema vyama vya siasa vimeshindwa kuwekeza kwenye vyama vyao na kutoa elimu kwa Watanzania, ndio maana kuna baadhi ya maeneo watu wanashindwa hata kuandika majina yao matatu, halafu bado vyama vyao vinataka waonewe huruma.

“Chama cha ndugu Mbowe ni mtindo wenu, hata madiwani wa Momba walipohama walikatiwa pia mahindi yao, sehemu nyingine walivunjiwa samani zao za ofisi, makosa wafanye wao, mahindi mkawakatie wengine, hilo halikubaliki, ujinga wako kisheria unaenda kutolea hasira kwa mtu mwingine, tunaendelea kukusanya ushahidi,”alisema .

CCM iliwekeza kwa wanachama wake, kwa kutoa elimu kwa wagombea, ambapo kilituma wanasheria na mawakili 1,250 nchi nzima na kuwagawanya katika kila kata na wilaya kutoa msaada wa kisheria, namna ya kujaza fomu hizo na kwamba hawakuruhusu mtu kujaza fomu nyumbani. Alisema CCM imejipanga kwenda kuomba dhamana kwa Watanzania na imeonyesha kiwango cha juu zaidi cha umakini wa chama chao.

“Chama cha ndugu Mbowe (Freeman) wengi wameingia chaka, wamejaa upepo unaitwa nani unasema CDM au kile cha ndugu Kabwe (Zitto) kimeandikwa ACT Wazalendo, matokeo yake wanachama wao buku mbili wameenguliwa, mnabaki CCM...CCM.. acheni nongwa” alisema.

Alisema CCM ilianza kuwekeza kwenye uchaguzi tangu mwaka 2017. Alitoa takwimu kuwa ina matawi yenye wanachama kuanzia watu 100 mpaka 150 na mashina 232. Wanachama hao wanafika milioni 15 nchini wenye kadi za kitabu na sasa wanawasajili kwa kadi za kielektroniki.

“Uchaguzi huu sisi hatujashtukizwa, tumejipanga tangu mwaka 2017 na unasimamiwa na matawi yetu 232, hakuna chama chochote ambacho kinafikia matawi haya hata robo,”alisema.

Waliojitokeza kuomba dhamana ya uongozi wa mwenyekiti serikali za mitaa ni 16,836, walioomba uenyekiti serikali ya kijiji kwa vijiji 12,000 ni wana CCM 49,348,000.

“Idadi hiyo ni zaidi ya mara nne ya nafasi ambazo chama kikatiba na kikanuni tunaweza kupeleka kwenye uchaguzi” alisema.

Kwamba kuna vitongoji 64,000 na walioomba kuwania uenyekiti ni wana CCM 28,42 ,000. Kwa wajumbe wa serikali za mitaa nchi nzima, walioomba ni 40,000 katika kata 4,000. Upande wa wajumbe wa serikali za vijiji, 696,201 waliomba kuwania nafasi hiyo. Mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho, ulianza kwa mtu kuweka nia kuchukua fomu. Ilikuwa ni marufuku kufanya kampeni za wazi za kuvurugana. Jumla ya fomu 930,000 zilichukuliwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Chadema yajitoa Akizungumzia kujitoa kwa Chadema kwenye uchaguzi huo, Mwenyekiti wake, Mbowe alisema kujitoa kwa chama hicho, kunatokana na maazimio yaliyofikiwa kwenye kikao cha wabunge wa chama chicho.

“Ni busara kwa chama chetu kutobariki uchaguzi, sisi kuendelea kushiriki kwa njia yoyote uchaguzi wa aina hii ni kuhalalisha ubatili, tumeamua hatutashiriki, ninatoa maelekezo kwa viongozi na wagombea wote nchini nzima wasitishe kushiriki, waachane na kukata rufaa, waachane na kuweka mapingamizi, hatupo tayari kubariki ubatili huu,”alisema.

Alisema chama chake kimeachiwa wagombea asilimia tatu tu kwenye maeneo ya miji ya makao makuu ya mikoa. Wana mitaa 4,263, chama kimesimamisha wagombea kwa asilimia 64 kwenye mitaa ya nchi sawa na mitaa 40,007. Upande wa vijiji wana 12,319 na chama kilisimamisha wagombea asilimia 85 ya vijiji nchi nzima sawa na wagombea 10,471. Kwa upande wa vitongoji, walisimamishwa asilimia 78 ya vitongoji vyote 64,383 sawa na vitongoji 50,218 na wengine maelfu wamesimamishwa.

“Waliofanikiwa kuchukua na kurudisha fomu ni asilimia 60 tu na asilimia 25 walinyimwa fomu na wengine wakatekwa na kushtakiwa wakati wa mchakato huo” alisema.

Wakati vumbi la uchaguzi wa serikali za mitaa likiendelea kutimka, wilayani Tarime mkoani Mara wagombea wanne wa Chadema na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Tarime, wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuwajeruhi maofisa wasimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za mitaa. Kauli ya Jafo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema kutokana na ukweli huo serikali haiwezi kupuuza asilimia 1.8 ya kasoro zilizojitokeza.

Aliagiza pingamizi zote za wagombea, zishughulikiwe kikamilifu ili haki itendeke. Jafo alitoa kauli hiyo juzi baada ya kufika ghafla kwenye mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge, uliokuwa ukifanyika katika Kijiji cha Bukulu Kata ya Sowela Tarafa ya Kolo wilayani Kondoa.

“Nilikuwa nikitoka mkoani Manyara, sasa njiani nimekutana na kibao kimeandika Bukulu, nikajua hapa ndio Bukulu makao makuu ya wilaya ya Kondoa, nikamwambia dereva wangu geuza gari tutafute ofisi za halmashauri, tulipofika karibu nikaona kuna magari mengine yamepaki hapa,” alisema Jafo huku akishangiliwa na wananchi.

“Lengo langu lilikuwa kwenda kuangalia ofisi za halmashauri na wala sikufahamu kuwa kuna mkutano wa mkuu wa mkoa,” alisema.

Alisema alikuwa akitokea mikoa ya Singida na Manyara kwa ajili ya kukagua mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa na kusisitiza kuwa maeneo mengi aliyopita mchakato huo umekwenda vizuri kwa asilimia 98.2, lakini serikali haiwezi kubeza asilimia 1.8 iliyobaki. Jafo alisema baada ya kutoka Manyara, atakwenda mikoa ya Iringa, Njombe, Morogoro na Tanga, na lengo ni kuona uhalisia wa hali ikoje.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala wa Serikali za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mwita Waitara, aliwaambia wabunge kuwa wao sio waliojaza fomu za kugombea nafasi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na kwamba walioenguliwa wanapaswa kufuata taratibu ikiwamo kwenda mahakamani kama hawajaridhika. Alisema baadhi ya maeneo ambako wabunge wamepiga kelele za kuwapo kwa ukiukwaji wa kanuni, imegundulika hali sivyo ilivyo kama inavyolalamikiwa na wabunge, hasa wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Waitara alisema hayo bungeni jana akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF). Katika swali lake, Salim alihoji kuenguliwa wagombea wa upinzani maeneo mbalimbali na kuwa licha ya agizo la Jafo la kuwarejesha wale watakaonekana hawana matatizo, halijatekelezwa. Waitara alisema wabunge wanalalamika, lakini wao sio waliojaza fomu za kugombea, na kwamba muda bado upo wa kukata rufani kwa mujibu wa kanuni.

Alifafanua kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi, juzi na jana ilikuwa muda wa kukata rufaa na kuzipeleka kwa Msimamizi Msaidizi. Alisema kuwa fursa hiyo ipo hadi kufikia Novemba 9, mwaka huu, kushughulikia Imeandikwa na Vicky Kimaro, Dar, Anastazia Anyimike, Dodoma, Sifa Lubasi na Mgaya Kingoba, Dodoma.

WAKURUGENZI wawili wa Kampuni ya Tanzanite One Mining Ltd ya ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi