loader
Picha

Uhusiano wa kidiplomasia unavyoimarika

HISTORIA ya Tanzania imesheheni matukio yanayoifanya iwe kati ya nchi zilizokuwa na ushawishi mkubwa kimataifa tangu uhuru ukilinganisha na nafasi yake kiuchumi na hata kijiografia.

Ukweli huu ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyeuambia ulimwengu baada ya uhuru kwamba uhuru wa wetu hautakuwa na maana kama nchi nyingine katika bara letu zitakuwa bado zinatawaliwa.

Tamko hilo liliiweka nchi yetu katika nafasi imara ya kidiplomasia, kwani lilikuwa nguzo muhimu ya kuimarisha uhusiano na mataifa mengine ya kikanda na kimataifa. Wapinga ukoloni wote na waliokuwa katika harakati za kudai uhuru, walijikuta wakiwa wadau katika wazo hilo la Mwalimu Nyerere.

Siyo hilo tu bali na mengine mengi kama vile Tanzania ilivyouambia Umoja wa Mataifa kuwa Jamhuri ya Watu wa China ilistahili kuwamo, hali iliyolifanya taifa kubwa kama China kuvutiwa na kunufaika na ushawishi wa Tanzania kwa mataifa mengine. Lakini pia watu wa mataifa mengine walivutiwa na jinsi Mwalimu Nyerere alivyoijenga Tanzania katika misingi ya umoja na amani, Watanzania wote wakiwa wamoja bila kujali tofauti za itikadi zao za kisiasa, kikabila na kidini.

Aidha, misingi hii imeijengea heshima Tanzania mpaka ikaitwa “kisiwa cha amani” huku ikiwa mstari wa mbele katika kulaani ubabe, uonevu na ukandamizaji popote pale ulipotokea duniani bila kuogopa.

Pamoja na mambo mengine, Tanzania, ikiwa imejizatiti katika misingi ya kidiplomasia, kwa nyakati tofauti ilijitolea katika ukombozi wa nchi zilizokuwa chini ya tawala za kikoloni, hasa zile za kusini mwa bara la Afrika. Kielelezo kizuri cha mchango wa Tanzania katika jumuiya ya kimataifa ni nishani ya heshima ya juu aliyopewa Dk Salim Ahmed Salim na nchi ya China kwa kutambua mchango wake katika kuitetea ili irudishiwe kiti chake Umoja wa Mataifa katika miaka ya 1970.

Aidha, mchango wa Dk Salim katika kuimarisha uhusiano kati ya China na Tanzania wakati aliposhikilia nyadhifa mbalimbali ulitajwa kama sababu ya kutunukiwa nishani hiyo. Vilevile, mchango wa Dk Salim katika kujenga uhusiano mzuri kati ya China na Afrika, akiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), umetajwa pia kuwa sababu nyingine ya kutunukiwa nishani.

Chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, Tanzania imeendelea kuwa mshirika mzuri katika jumuiya mbalimbali za kimataifa, katika Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kupitia ushiriki wake Tanzania imeendeleza misingi ya Baba wa Taifa ya kupinga dhuluma, kuhimiza maendeleo barani Afrika, kulinda amani, umoja na mshikamano. Kwa sasa, Tanzania ikiwa ndiye mwenyekiti wa SADC, inaendelea kutumia diplomasia katika kukuza uhusiano na ustawi katika nchi wanachama wa SADC, kwa kuitaka jumuiya ya kimataifa kuiondolea nchi ya Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alipokuwa akifungua kongamano la kumbukizi ya Mwalimu Nyerere hivi karibuni, alisema Tanzania haiko katika dunia yake yenyewe na kwamba, katika kujiletea maendeleo, huona fahari katika kushirikiana na nchi nyingine.

“Ni msimamo wetu kuwa nchi za SADC haziwezi kujiletea maendeleo katika nchi wanachama kama wenzetu wanakabiliwa na vikwazo. Nimefurahi kusikia kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mko katika maandalizi ya kongamano ambalo, pamoja na mambo mengine, litajadili mustakabali wa vikwazo kwa maendeleo ya Zimbabwe na Afrika kwa ujumla,” alisema.

Sera ya mambo ya nje pia inaitaka Tanzania kuimarisha utendaji wa mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali ambayo yanafanya kazi nchini ili kuhakikisha huduma mbalimbali zinazotolewa na mashirika hayo zinaendana na sheria za nchi, ambapo kwa Tanzania pia tumeshuhudia asasi mbalimbali zikifanya kazi zake hapa nchini.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekabidhiwa usimamizi na mapitio ya sera, ambapo pamoja na mambo mengine, imepewa jukumu la kuratibu shughuli zote kimataifa na kuimarisha shughuli zote kidiplomasia zinazoiunganisha Tanzania na mataifa mengine duniani. Ili kufanikisha malengo hayo, Tanzania inatumia mikakati mbalimbali ili kuendana na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi, kwa kuzingatia misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa letu.

Mikakati hiyo imejikita katika kutengeneza mazingira mazuri ya ndani na nje ya utekelezaji wa sera hiyo ili kuimarisha diplomasia. Malengo ya sera hiyo ni pamoja na kuanzisha, kuhimiza na kulinda maslahi ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiuchumi ya Tanzania kupitia diplomasia endelevu ya kiuchumi. Malengo mengine ya sera pia ni kuhakikisha mahusiano ya Tanzania na nchi nyingine au mashirika ya kimataifa yanachochewa ili kukuza maslahi mapana ya kiuchumi.

Kujenga uchumi wa kujitegemea, kuimarisha amani na usalama wa taifa na kusaidia juhudi za kikanda na kimataifa ili dunia iwe na amani ni malengo mengine ya sera hiyo. Ukuaji wa uchumi wa kidiplomasia Moja kati ya mambo yanayotiliwa mkazo na serikali ni kuimarisha na kukuza uhusiano wa kimataifa pamoja na diplomasia ya uchumi, ambapo mabalozi wa nchi yetu wamekuwa tegemeo kubwa katika kuhamasisha malengo hayo.

Diplomasia ya uchumi ni dhana pana lakini kwa lugha nyepesi ni uwakilishi wa nchi nje ya nchi na mara nyingi hujikita katika mambo ya kiuchumi, ambayo ni pamoja na kuvutia wawekezaji, kuvuta watalii na kuhamasisha fursa za biashara. Kupitia wawakilishi wetu katika muktadha huo wa kukuza diplomasia ya uchumi Mwezi Aprili 2019, Serikali ilipokea watalii 1,000 kutoka Israel.

Aidha, mwezi Mei, 2019 serikali pia ilipokea watalii 330 wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji kutoka China. Watalii hao walikuwa ni kundi la kwanza miongoni mwa watalii 10,000 ambao wanatarajiwa kutembelea Tanzania mwaka huu. Mazao 10 ya Tanzania yapata soko China Katika mkutano wa 15 wa kimataifa baina ya China na nchi jirani na nchi marafiki, uliofanyika mwaka 2018 nchini humo, mazao 10 kutoka Tanzania yalipata wanunuzi katika masoko ya China.

Mazao yanayohitajiwa kwa wingi katika soko la China ni korosho, kahawa, mbaazi, choroko, dengu, chai, tangawizi, asali na muhogo. Sekta ya Elimu Katika kuhakikisha kuwa uhusiano kati ya China na Tanzania unazidi kukua katika sekta ya elimu, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa miaka 55, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilisaini makubaliano ya ushirikiano na chuo kikuu cha Beijing katika masuala ya sheria.

Makubaliano hayo yalifanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Juni 2019 wakati wa uzinduzi wa kituo cha mafunzo ya sheria kwa nchi za Afrika. Haya yote yanaonesha namna diplomasia yetu ya uchumi inavyoimarika katika taifa hilo linaloibuka kwa ukubwa duniani hususani katika miaka hii minne ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/2020 utarejea tena Juni ...

foto
Mwandishi: Nelson Kessy

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi