loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Historia na juhudi za China katika maendeleo ya sayansi na teknolojia

KATIKA historia ya maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini China, hasa hadi kufi kia mwanzoni mwa enzi ya utawala wa kifalme ya Ming (1368 – 1644), China iliwahi kuwa nchi inayoongoza duniani.

Mavumbuzi manne makubwa yaliyofanyika nchini China karne nyingi kabla ya hapo, yaliweza kuleta mabadiliko makubwa duniani. Kwa wanaofuatilia maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani, wanaweza kukumbuka kuwa mavumbuzi manne ya China yaani utengenezaji wa karatasi, uchapaji, baruti na dira, ni mavumbuzi yaliyoleta mabadiliko makubwa duniani.

Teknolojia za mambo haya zinazotumika leo duniani, msingi wake unatokana na mavumbuzi hayo ya China. Hata hivyo kutokana na sababu mbalimbali, nguvu ya sayansi na teknolojia ya China ilikuwa imepotea kabisa hadi kufikia karne ya 14. Hii ni kutokana na kuwa katika kipindi hicho, mkazo kwenye elimu uliwekwa kwenye masomo ya fasihi na sanaa.

Masomo hayo yalionekana kuwa ni muhimu zaidi katika mtihani wa kifalme wa wakati ule, kwani kulikuwa na mahitaji ya maofisa wengi na kazi ya uofisa ilionekana kuleta hadhi katika jamii. Hisabati na masomo mengine yaliyohusu mambo ya uvumbuzi hayakupewa uzito mkubwa, na hayakupata uungaji mkono wa kutosha kutoka kwa serikali ya mfalme.

Hali hii ilifanya masomo ya sayansi yapoteze hadhi yake katika jamii ya China. Lakini kosa lililotokana na kupuuza sayansi na teknolojia lilileta pigo kubwa kwa China, hasa pale ilipovamiwa na kuonewa na Japan na baadhi ya nchi za Magharibi.

Udhaifu kwenye sayansi na teknolojia ulikuwa ni sababu kuu ya China kushindwa kujilinda. China ililazimika kutumia silaha na zana duni, na kufanikiwa kushinda uvamizi wa Japan baada ya mapambano ya kufa na kupona yaliyodumu kwa miaka 14.

Somo la kuvamiwa liliifanya China ianze kutafakari upya na kuamsha harakati za kuleta maendeleo ya sayansi, ikiwa ni njia ya kuimarisha nguvu ya nchi na kujilinda dhidi ya wavamizi. Baada ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949, serikali ya China iliamua kutoa kipaumbele kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hata hivyo mipango yake ya maendeleo ya sayansi na teknolojia haikupiga hatua sana.

Kwanza ni kutokana na mtindo usioendana na mazingira ya China, uliokuwa unaigwa kutoka kwenye mfumo wa Umoja wa Kisovieti (USSR). Watu wasiokuwa na ujuzi wa sayansi na teknolojia walisimamia idara za sayansi. Pili ni kutokana na changamoto zilizotokea katika kipindi cha miaka 10 kati ya mwaka 1966 -1976 wakati wa mapinduzi ya utamaduni, na kufanya juhudi zilizoanza kutekelezwa ziachwe.

Maendeleo ya sasa ya sayansi na teknolojia nchini China, msingi wake ulianza kujengwa upya mwaka 1976, wakati kiongozi wa wakati ule Deng Xiaoping, alipotaja kuleta mambo ya kisasa kwenye mambo manne, yaani kilimo, ulinzi wa taifa, viwanda na sayansi na teknolojia. Polepole mfumo uliokuwa unafanana na wa Urusi ulianza kubadilishwa.

Serikali ya China iliweka mkazo mkubwa katika kutenga fedha kwa ajili ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, kufanya sayansi na teknolojia kuwa na hadhi ya kipekee kwenye maendeleo ya uchumi na hata hadhi ya taifa. Katika kipindi cha kuanzia miaka ya 1990 hadi mwaka 2010, China ilikuwa inapiga hatua kwa kasi kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Mwaka 1995 Baraza la Serikali la China (sawa na Baraza la Mawaziri) lilitoa waraka wa “Uamuzi wa serikali kuhimiza maendeleo ya sayansi na teknolojia” ulioeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ya sayansi na teknolojia katika miongo iliyofuata.

Kuna njia mbili kuu ambazo zilifuatwa katika kujiendeleza kwenye mambo ya sayansi ya teknolojia. Kwanza ilikuwa ni kuweka mazingira mazuri ya ndani katika kuendeleza sayansi na teknolojia, na kuwaandaa wachina kwa sayansi na teknolojia. Pili ilikuwa ni kushirikiana kwa karibu na nchi na mashirika makubwa katika kuingiza teknolojia (Technology transfer).

Elimu ya sayansi imepewa kipaumbele katika ngazi mbalimbali za elimu. Tangu China ianze kampeni ya kuhimiza mwamko wa sayansi katika jamii, matokeo yanaonesha maendeleo mazuri. Mfano ni kuwa mwaka 2009 kwenye mpango wa kimataifa wa upimaji wa wanafunzi, wanafunzi wenye umri wa miaka 15 wa mji wa Shanghai, walionekana kuongoza kwenye masomo ya hisabati, sayansi na kusoma, na kuwaacha kwa mbali wanafunzi wa Marekani, Canada na nchi nyingine zinazoongoza kwenye sayansi na teknolojia.

Kwa sasa China pia imekuwa ni nchi yenye idadi kuwa zaidi ya wahandisi na wanasayansi. Hii ni kutokana na kuwa na vyuo vinavyotoa mafunzo ya michepuo ya sayansi, na kuwa na wahitimu wengi wa shahada za uzamili na uzamivu kwenye maswala ya sayansi. Mbali na wachina wanaosoma nchini, wachina waliosoma nje ya nchi pia wamekuwa wanahimizwa kurudi nyumbani.

Na kupitia idara maalum inayoshughulikia watu wenye asili ya China, serikali ya China imeweka mpango maalum wa kuwashirikisha watu hao kwenye kuleta biashara, uwekezaji na teknolojia za kisasa kutoka nje, iwe ni kwa njia ya ubia au biashara. China pia imekuwa ikiwavutia wachina walisoma nje ya nchi kurudi na kufanya kazi nyumbani.

Tangu mwaka 1978 hadi sasa zaidi ya wanafunzi milioni 3.13 wa China waliosoma nje ya China wamerudi nyumbani, na kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Motisha wa aina mbalimbali kama vile mikopo ya kuanzisha biashara zao, nyumba, mishahara mizuri au nafasi mbalimbali za upendeleo zimewekwa kwa ajili ya watu hao.

Kwa sasa hakuna mjadala kuwa China imepiga hatua kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia. Licha ya kuwa bado haijazifikia nchi za Magharibi zinazoongoza kwa sayansi na teknolojia duniani, kuna baadhi ya maeneo China imepiga hatua na kuwa nafasi ya mbele duniani.

Kwenye mpango wa 13 wa maendeleo ya miaka mitano, (2016 -2012) China imejihakikishia kupata maendeleo kwenye teknolojia za injini za ndege, kuwa na kituo chini ya bahari, kuwa na teknolojia za kisasa zaidi za kompyuta, sayansi za ubongo na utafiti wa ubongo. Baadhi ya maeneo ambayo China imekuwa na maendeleo ya wazi, ni pamoja na sekta ya kilimo.

Licha ya kuwa na eneo dogo linalofaa kwa kilimo, China imeweza kukidhi mahitaji yake ya chakula kwa kutumia sayansi na teknolojia. Maendeleo makubwa pia yameonekana kwenye sekta ya ufugaji wa samaki na uvuvi.

Kwenye sekta ya Tehama China imekuwa moja ya nchi zinazoongoza katika utengenezaji wa vifaa vya Tehama kama vile kompyuta na simu za mkononi, na ina makampuni makubwa ya Tehama kama vile Huawei, ambayo teknolojia yake ya mawasiliano ya 5G inaongoza duniani.

Maendeleo hayo pia yameonekana kwenye matumizi ya Intaneti, ambapo sasa kuna makampuni makubwa ya kutengeneza software kama Tencent, na tovuti maarufu za biashara ya mtandao wa internet kama vile Alibaba.com.

Kwenye vifaa vya kielektroniki, China inaongoza kwenye utengenezaji na uuzaji wa kompyuta, skrini za televisheni na vifaa vya mawasiliano kama simu za mkononi. China pia inafanya juhudi ili iweze kuongoza kwenye teknolojia ya akili bandia kabla ya mwaka 2030. Kwa sasa China imekuwa ni moja ya nchi ambazo imeweza kutengeneza roboti na ndege zisizo na rubani zikiwa na uwezo wa akili bandia. Kwa sasa China inadhibiti asilimia 80 ya soko za ndege zisizo na rubani duniani.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalum

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi