loader
Picha

NMB yatoa milioni 900/- kusaidia elimu, afya

KUTOKANA na umuhimu wa sekta ya elimu na afya, taasisi na mashirika mbalimbali yamekuwa yakijitolea kusaidia sekta hizo. Kwa kuzingatia hilo, Benki ya NMB imetoa zaidi ya Sh milioni 900 katika kipindi cha mwaka huu kwa ajili ya elimu na afya.

Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Straton Chilongola alisema benki ya NMB kwa mwaka 2019 imetenga Sh bilioni moja kwa jamii, kwa kuzilenga sekta hizo. Kwamba inafanya hivyo ili kuunga mkono juhudi za serikali.

Alisema kuwa fedha hizo hutumika kutoa misaada ya vifaa vya ujenzi, madawati, meza, viti na kompyuta. Kwamba NMB hutoa fedha hizo kupitia Kitengo cha Masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR). Chilongola alisema kuna mambo mengi NMB wamepanga kuifanyia jamii, lakini wameamua kuanza na elimu na afya kwa sababu ni mambo waliyoyapa kipaumbele cha kwanza kwani yanagusa jamii moja kwa moja.

Alisema kuwa hivi karibuni NMB ilitoa msaada wa madawati 100 kwa shule za msingi za Maduma na Uhambila Kata ya Maduma wilayani Mufindi.

“Kwa miaka kadhaa sasa Benki ya NMB tumekuwa mstari wa mbele kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi kwa lengo la kurejesha sehemu ya faida yetu kwa jamii na kwa zaidi ya miaka saba mfululizo tumechangia asilimia moja ya faida yetu kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayotuzunguka,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William akiwakilishwa na Katibu Tarafa wa Malangali, Andrew Chunga katika hafla hiyo, ambapo aliishukuru NMB kwa kusaidia sekta ya elimu. Alitoa mwito kwa benki hiyo kuendelea kutoa misaada mbalimbali katika sekta nyingine zinazokabiliwa na changamoto kubwa.

Alisema msaada huo umekuja kwa wakati muafaka kwani shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo barabara, maabara na dawa kwa ajili ya wanafunzi. Alitoa mwito kwa NMB kuendelea kuisaidia shule hiyo na nyingine katika wilaya ya Mafinga. Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameishukuru benki hiyo kwa msaada wa meza na viti vyenye thamani ya Sh milioni 10 kwa Shule ya Sekondari ya Mrisho Gambo katika Kata ya Mashono Vijijini.

Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Aikansia Muro alisema msaada huo ni sehemu ya mchango wao kwa jamii na kuunga mkono juhudi za serikali kuleta maendeleo. Kwamba NMB imejikita zaidi kwenye miradi ya elimu na afya na kusaidia majanga yanayoipata nchi yetu. Alisema benki hiyo ndiyo inayoongoza nchini kwa kuwa na matawi 229, ATM zaidi ya 800, NMB Wakala zaidi ya 6,000 na wateja zaidi ya milioni tatu, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na benki nyingine nchini.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Simon Chacha amepokea msaada wa madawati 125 kwa ajili ya shule za msingi Minigo na Ryaghati wilayani Rorya. Chacha alisema kuwa NMB imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo wilayani humo na aliahidi kuendeleza ushirikiano na uhusiano huo.

Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Amos Mubusi alisema benki hiyo ilipokea maombi ya msaada kwa shule hizo na kuyafanyia kazi kwa haraka.

“Vitu vyote hivi tunavyokabidhi leo kwa shule hizi vina thamani ya Sh milioni 15 na ni sehemu ya misaada ambayo benki tunatoa kwa ajili ya maendeleo ya jamii,” alisema Mubusi.

TANZANIA imeitaka Dunia na Jumuiya za Kimataifa kutambua kuwa kauli ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi