loader
Picha

‘Wapeni elimu ya mikopo walemavu’

WAKURUGENZI Watendaji wa Halmashauri na Maofi sa Maendeleo ya Jamii wametakiwa kuwapa elimu ya ujasiriamali watu wenye ulemavu ili wafaidi mikopo ya asilimia mbili wanazowatengea.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Nyamhanga alitoa agizo hilo juzi jijini hapa wakati akizungumza kwenye Kongamano la Asasi za Kiraia (AZAKI) ambalo linafanyika jijini hapa kwa kuzikutanisha zaidi ya asasi za kiraia 500 kutoka nchi nzima.

Nyamhanga alisema kuna changamoto kwa watu wenye ulemavu kutotumia fursa ya mikopo hiyo kutokana na kutokuwa na elimu ya ujasiriamali hivyo kuwafanya wengi kuwa ombaomba mitaani.

“Najua watu wenye ulemavu hawawezi kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha zikiwemo benki kutokana na hali yao, ndiyo maana serikali iliamua kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zote nchini kwa ajili ya kutoa mikopo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

“Lakini katika hali ya kusikitisha watu wengi wenye ulemavu hawajajitokeza vya kutosha kutumia fursa hii ya mikopo kujiimarisha kiuchumi ndiyo maana nawaagiza wakurugenzi watendaji wa halmashauri kupitia maofisa maendeleo ya jamii kutoa elimu ya ujasiriamali ili wajiunge katika vikundi, kujisajili ili kupata mikopo inayotolewa na halmashauri bila masharti magumu,” alisema.

Alisema mikopo inayotolewa na halmashauri ya asilimia 10 ya mapato yake ya ndani ni kwa mujibu wa sheria, hivyo kila moja ni lazima itenge fedha hizo kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kila halmashauri ambayo haitafanya hivyo, viongozi watatakiwa kujieleza.

Nyamhanga alisema kutokana na agizo hilo, katika mwaka 2018/2019, halmashauri mbalimbali nchini zilitenga Sh bilioni 54.08 kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, lakini hadi kufikia Juni 30, mwaka huu kiasi cha fedha kilichotolewa ni Sh bilioni 42.06.

“Kati ya fedha hizo, zilizoenda kwa vikundi vya watu wenye ulemavu ni Sh bilioni 3.87 ambazo ni kidogo kulinganisha na wanawake waliopata Sh bilioni 23.18 na vijana Sh bilioni 15.01,” alisema.

Alisema mwaka 2019/2020, serikali imetenga Sh bilioni 62.22 ambapo vikundi vya wanawake na vijana vimetengewa Sh bilioni 24.9 na watu wenye ulemavu wametengewa Sh bilioni 12.4 lakini ni vikundi vichache vimejitokeza kutumia fedha hizo kutokana na kutokuwa na elimu ya ujasiriamali.

SERIKALI imetoa ripoti ya uchunguzi wa Maabara ya Taifa ya ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi