loader
Picha

Halmashauri ziwezeshwe kujenga maghala ya chakula

MBUNGE wa Nanyamba, Abdalah Chikota (CCM), ameiomba serikali iipe kipaumbele sekta ya kilimo na kuzitengea fedha halmashauri, ili zijenge maghala na kuepusha uhifadhi wa mazao kwenye maghala ya watu binafsi ambayo ni gharama. Alisema kufanya hivyo kutaokoa zaidi ya Sh bilioni moja kwa mwaka zinazotumika kulipia uhifadhi mazao kwenye maghala hayo binafsi.

Alitoa ombi hilo wakati akichangia mjadala wa mapendekezo ya mpango wa Serikali 2020/2021 bungeni na kusema kwa sasa kilo moja ya mazao inahifadhiwa kwa Sh 38 na kwamba tani 30,000 zinagharimu Sh bilioni moja kila mwaka. Chikota alisema ili kuokoa fedha hizo ni lazima serikali itenge bajeti itakayowezesha kujengwa maghala hususan kwa ajili ya kuhifadhi pamba na korosho.

“Tutenge fedha na kuzipa mamlaka za Serikali za Mitaa ili zijenge maghala. Hii itasaidia kuachana na gharama tunayoitumia kuhifadhi mazao katika maghala ya watu binafsi, badala yake tutaongeza mapato ya Serikali,” alisema Chikota.

Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM), aliishauri serikali ipanue bandari ya Mtwara sambamba na ujenzi wa reli na ili kufungua uchumi wa Kusini. Pia, aliishauri serikali kuwekeza kwenye lishe na kutilia mkazo siku 1000 za lishe kuhakikisha watoto wanakuwa na afya bora, hivyo kuweza kushiriki kuchangia maendeleo ya nchi.

Mbunge wa Igalula, Mussa Ntimizi (CCM) aliitaka serikali kuwekeza katika miundombinu ya umwagiliaji ili kuweza kuzalisha chakula cha kutosha, jambo litakalochangia usalama wa chakula na kupunguza umasikini.

Mbunge wa Manonga, Hashimu Gulamali (CCM) aliishauri serikali kuongeza fedha kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kwa kutenga asilimia 60 badala ya asilimia 30 ya sasa ili kukidhi mahitaji ya barabara za vijijini. Kwa sasa Tarura inapewa asilimia 30 na Tanroads asilimia 70, hivyo kuwafanya wabunge hao kusema kiasi hicho cha fedha ni kidogo ikilinganishwa na majukumu ya iliyonayo Tarura.

Alisema katika baadhi ya maeneo Tarura hafungui barabara, kujenga madaraja kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha. “Hali hii imewafanya wakulima kupata wakati mgumu kusafirisha mazao yao wakati wa kuuza, lakini pia inalikosesha taifa mapato.”

MAKUBALIANO ya mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi