loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkandarasi umeme Mwanza abanwe

SERIKALI imejitahidi kusambaza umeme mijini na vijijini. Juhudi hizo zimeifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazoongoza barani Afrika kwa kusambaza nishati hiyo kwa sasa.

Kwa mujibu wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kasi ya kuunganisha umeme nchini, imeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Rais John Magufuli.

Kwa mfano, vijiji vilivyounganishwa umeme, vimeongezeka kutoka vijiji 2,018 mwaka 2015 hadi vijiji 8,012 mwezi Oktoba mwaka 2019. Hilo ni ongezeko la vijiji 6,084 ikiwa ni sawa na asilimia 301.

Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo kubwa za serikali, bado kuna makandarasi waliopewa kazi ya kusambaza umeme, wanaosuasua kukamilisha miradi.

Moja ya mikoa yenye changamoto hiyo ni Mwanza, ambako hivi karibuni wakuu wa wilaya walieleza wazi wazi kuwa hawaridhishwi na utendaji kazi wa mkandarasi anayetekeleza miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Kwamba mkandarasi huyo ameshindwa kutekeleza miradi kwa wakati katika baadhi ya maeneo ya vijijini katika wilaya zao. Kwamba wana wasiwasi hatatekeleza pia agizo kukamilisha miradi hiyo ndani mwezi mmoja hadi Desemba.

Alipewa agizo hilo na bodi ya wakurugenzi wa REA. Wakuu hao wa wilaya wanasema wamechoka na maneno ya mkandarasi huyo, ambaye awali aliwahakikishia kuwa miradi ingekamilika kwa wakati.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipore, mkandarasi huyo ametumia muda wa miaka miwili kuweka nguzo 46 tu na kuunganisha nyumba 350 tu wilayani humo.

Kwamba baadhi ya vibarua wanaofanya kazi kwa mkandarasi huyo, wamekuwa wakienda ofisini kwake mara kwa mara kumlalamikia kwa kushindwa kuwalipa fedha zao.

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda anasema anamshangaa mkandarasi huyo, kwa kushindwa kutekeleza mradi huo katika wilaya yake.

Kwamba ameweka nguzo kwa muda mrefu kwenye kata tatu, huku kata hizo zikiwa hazina umeme.

Hali ipo hivyo hivyo pia wilayani Magu, ambako Mkuu wa Wilaya, Dk. Philemon Sengati anasema anashangaa jinsi mkandarasi huyo anavyotekeleza mradi huo wa REA.

Anasema mwaka 2017 Wizara ya Nishati iliwahakikishia viongozi wa wilaya na wananchi, kuwa kila mwananchi angepata huduma ya umeme huo wa REA, lakini hali ni tofauti.

Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Ngaga anasema mkandarasi huyo, anampa wakati ngumu, kwa madai kuwa alichokifanya ni kupeleka nguzo tu na katika baadhi ya maeneo, nguzo hizo ziko chini bila kuwepo dalili ya kuwaka umeme.

Hivyo, kutokana na hali hiyo, tuna imani menejimenti ya REA, bodi ya wakurugenzi wa REA na Wizara ya Nishati, watayafanyia kazi malalamiko ya wakuu hao wa wilaya za mkoa wa Mwanza.

Wananchi wa wilaya hizo za mkoa wa Mwanza, wanachohitaji ni kuona umeme unawaka na sio nguzo wala nyaya zilizorundikwa chini.

Maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi