loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM kuzindua kitabu cha maisha ya Mkapa

UZINDUZI wa kitabu cha Tawasifu ya Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alichokiandika mwenyewe, unafanywa leo Dar es Salaam na Rais John Magufuli huku marais wastaafu wote walio hai wa Tanzania wakitarajiwa kupamba uzinduzi huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais mstaafu huyo, uzinduzi wa kitabu hicho kiitwacho; “My Life, My Purpose: A Tanzanian President Remembers”, utahudhuriwa pia na viongozi wengine wa ngazi za juu, wafanyabiashara, wadau wa maendeleo, wasomi, taasisi za kiraia, vijana na waandishi wa vitabu.

Marais wanaotarajiwa kuhudhuria uzinduzi huo ni Rais mstaafu wa Awamu wa Pili, Ali Hassan Mwinyi pamoja na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete. Kitabu hicho kinazungumzia maisha yake ya utoto, ujana hadi kuwa kiongozi wa ngazi ya juu nchini na pia kinazungumzia maisha yake baada ya kustaafu katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Kitabu hicho kimechapishwa na wachapaji Mkuki na Nyota kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi. “Kuandika kitabu hiki nilihitaji kuangalia maisha yangu tangu utoto na kuandika safari yangu kuanzia hapo hadi leo, kina kumbukumbu zenye maumivu makali, ilibidi nivute hisia na kuzikumbuka vizuri ili niweze kuandika kitabu hiki, nyingine zilinitia nguvu na ujasiri ambao leo Watanzania tumefanikiwa,’’ alisema Mkapa kwenye taarifa hiyo.

Aliongeza; ‘’Tangu niondoke madarakani, dunia imebadilika na changamoto nyingi zimebaki zile zile ambazo leo viongozi wetu waliopo madarakani wanakumbana nazo,’’ alinukuliwa Mkapa kwenye taarifa hiyo. Mbali na kusema hayo, Mkapa pia aliwashukuru waliochangia kukua kwa maisha yake binafsi na ya ukombozi wa mataifa ya Afrika huku akimkumbuka Mwalimu Julius Nyerere kama mmoja wa viongozi waliofanikisha harakati za ukombozi wa bara hilo.

Kuhusu kitabu hicho, Mkapa alisema anaamini kitawavutia wengi kukisoma na hivyo kusaidia kuelezea historia ya Tanzania kwa kizazi kipya na kwa viongozi wa baadaye wa Afrika. Kitabu hicho baada ya uzinduzi wake kitakuwa kikiuzwa au kupatikana kwenye maduka ya vitabu na pia kupitia mauzo mtandaoni kama vile Amazon na kwingineko. Mkapa alikuwa Rais wa Tanzania katika Awamu ya Tatu iliyoanza mwaka 1995 hadi 2000. Pamoja na mambo mengine atakumbukwa kwa kuleta mageuzi ya kiuchumi.

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi