loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Rita kusajili vyeti kwa njia ya mtandao

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) unatarajia kuanzisha huduma ya usajili kwa njia ya mtandao ili wananchi wengi wapate urahisi wa kufanya maombi ya cheti cha kuzaliwa.

Hayo yalielezwa bungeni jana na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Fatma Toufiq (CCM). Mbunge huyo alitaka kujua serikali imejipangaje kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa Watanzania wenye zaidi ya miaka mitano na kuendelea baada ya kufanyika kampeni kwa watoto chini ya miaka mitano.

Akijibu swali hilo, Dk Mahiga alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa njia hiyo ya mtandao ni kuwezesha kuwafikia wananchi wengi kwa urahisi ambapo wataweza kufanya maombi ya cheti cha kuzaliwa kupitia mtandao na baadaye kufika ofisi ya Rita iliyo karibu kwa ajili ya kukamilisha taratibu za usajili. Alisema Rita imejiwekea malengo ya kusajili na kutoa vyeti kwa wananchi milioni 15.917 ifikapo mwaka 2025.

“Hatua hiyo itasaidia kufanya idadi ya wasio na vyeti kupungua hadi kufikia milioni 21.5 ambao ni chini ya asilimia 50 ya wote wenye umri zaidi ya miaka mitano,” alisema.

Aidha, Mahiga alitoa mwito kwa wananchi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa kufika kwenye ofisi za Rita kwa ajili ya kusajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa ikiwa ni haki yao muhimu ya kutambuliwa.

“Aidha, niwaombe wabunge wote kuendelea kushirikiana na serikali kwa kuwaelimisha wananchi katika majimbo yenu juu ya umuhimu wa kusajili matukio muhimu ya binadamu, ikiwa ni pamoja na kujisajili na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa,” alisisitiza.

Alisema kuwa serikali kupitia Rita imekuwa ikitekeleza mkakati wa usajili wa matukio hayo muhimu na takwimu ili kuboresha hali ya usajili nchini. Mahiga alisema mkakati huo una mipango ambayo imekuwa ikitekelezwa na serikali, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa watanzania wote wenye umri wa zaidi ya miaka mitano wanasajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.

Alisema mojawapo ya mipango hiyo ni kusajili na kutoa vyeti ya kuzaliwa kwa watoto wote waliopo kwenye mfumo rasmi na kufanya kampeni za uhamasishaji kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao ya makazi.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi