loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ewura yaja kivingine biashara ya mafuta vijijini

UNAISHIWA na mafuta kwenye gari yako katika moja ya vitongoji nchini na unapouliza mahala unapoweza kuongeza mafuta unaambiwa hakuna kituo cha mafuta kilicho karibu.

“Lakini nenda pale utapata mafuta,” unaelekezwa na dereva wa bodaboda unayemuuliza mahala unapoweza kupata mafuta.

Unapofika mahala ulikoelekezwa unakuta kuna meza ambako vimepangwa vidumu na chupa za plastiki zikiwa na petroli ambazo wala hujui kabla ya kuwekwa mafuta zilikuwa na kitu gani ndani.

Unalazimika kununua vidumu viwili ukiwa hujui ubora wa mafuta hayo wala mchanganyiko wake kutokana na chombo ambacho mafuta yamewekwa. Ni kutokana na kadhia hiyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imekuja na mikakati miwili ya kusogeza huduma za vituo vya mafuta karibu na wananchi, ikiwemo maeneo kama hayo ambayo wawekezaji wanaona ugumu kuweka vituo vya kisasa. Mkakati huo unalenga kupunguza madhara yatokanayo na mafuta kwenye vidumu, machupa ya plastiki na vifaa vingine ambavyo havikutengenezwa kwa madhumuni hayo kwa kuwa ni hatari pia katika usalama endapo kutatokea moto.

UJENZI WA VITUO RAHISI

Akitoa mada kwenye mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyofanyika Dodoma kuhusu utendaji wa Ewura, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka hiyo, Nzinyangwa Mchany, anasema mkakati wa kwanza ni kuhakikisha kwamba huduma ya mafuta inakuwa karibu na wananchi. Anasema wanatarajia kuanzisha utaratibu mpya wa kuhamasisha wawekezaji wa biashara ya mafuta katika maeneo ya vijijini na vitongojini kuweka vituo vingi kwa gharama nafuu.

Anasema katika mkakati wao watarahisisha upatikanaji wa leseni, kwa wawekezaji hao na kuondoa baadhi ya vigezo ambavyo si vya lazima katika kuwekeza kwenye sekta ndogo ya mafuta. Anasema wawekezaji watakaokuwa tayari kujenga vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini wataruhusiwa kujenga vituo rahisi vidogo ambavyo vina pampu moja au mbili bila kuwa na vitu vingi kama vya mjini.

“Lakini pia bei ya ujenzi wa vituo hivyo ni ndogo, kutoka Sh bilioni moja hadi Sh milioni 50, hatua ambayo inahamasisha wawekezaji wenye mitaji kuchangamkia fursa hii,” anasema Mchany.

VITUO VINAVYOTEMBEA

Kaimu Mkurugenzi huyo anasema wanajipanga pia katika kuhakikisha wanakuja na vituo vinavyohamishika kutoka eneo moja hadi lingine ili kutoa huduma hiyo kwa kutumia magari madogo au maguta yenye magurudumu matatu. Lengo la mpango huo anasema ni kuhakikisha kwamba huduma ya uuzaji wa mafuta inafika katika maneo ya vijijini ikiwa salama zaidi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu katika maeneo yao. Mkakati huo anasema mkakati unalenga pia kupunguza athari zinazotokana na wasafirishaji wa mafuta kutoka eneo moja hadi jingine kwa kutumia madumu na makopo ya plasitiki ambayo ni hatari kwa maisha yao.

HATARI MAFUTA KWENYE PLASTIKI

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo, anatoa ufafanuzi kuhusu usafirishaji, ubebaji na uuzaji mafuta kwenye makopo, vidumu na madebe ya plastiki akisema ni hatari kwa usalama na wao hawaungi mkono suala hilo.

“Ili kupunguza tatizo la mafuta vijijini, tunakusudia kuanzisha huduma za mafuta zinazotembea (mobile) ili kuwafikishia wananchi huduma za mafuta kwa kutumia magari ya pickup au bajaji za miguu mitatu,” anasema.

Kaguo anasema kazi hiyo wamewaachiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa ajili ya kufanya utafiti ni namna gani wawekezaji wanaweza kuanzisha utoaji wa huduma ya mafuta kupitia vituo vinavyotembea. Kaguo anasema mkakati huo wa kuweka vituo vinavyohamishika kutoka kijiji kimoja hadi kingine, utaanza karibuni mara utafiti utakapokamilika na kwamba unatarajia kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa mafuta vijijini na maeneo yasiyo na vituo vya mafuta.

Anasema licha ya kutoa leseni kwa ajili ya ujenzi wa vituo 1,500 vya mafuta nchini katika miaka ya karibuni bado mahitaji ni makubwa katika maeneo ya vijijini tofauti na mjini ambako vituo ni vingi. Anasema wao kama wadhibiti, hawawezi kuruhusu kubeba mafuta kwenye plastiki kutokana na ukweli kwamba hayakutengenezwa kwa nia hiyo na wakati mwingine mafuta yanaweza kuyeyusha makopo, madebe au vidumu hivyo.

Ewura inasisitiza kwamba ni marufuku kuuza petroli barabarani, kwenye nyumba au kubeba kwenye madebe na madumu ya plastiki kwani kufanya hivyo ni hatari kwa usalama.

Msisitizo huo wa EWURA unaenda sambamba na ule alioutoa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Mluto ambaye Septemba 19 mwaka huu, alifanya msako jijini humo na kukamata zaidi ya lita 4,000 za petroli iliyokuwa ikiuzwa mitaani, kando ya barabara kwenye madebe na vidumu. Mkakati huo wa Ewura umekuja ili kuhakikisha kwamba ufanisi wa kazi zake ndani ya miaka 13 ya uhai wake tangu 2006, unakuwa wenye ufanisi mkubwa.

UCHAKACHUAJI WADHIBITIWA

Kuhusu ubora wa mafuta, Kaguo anasema tayari mamlaka hiyo imejitahidi kuondoa uchakachuaji kutoka asilimia 78 mwaka 2006 hadi asilimia nne mwaka huu na kwamba kiujumla hakuna uchakachuaji isipokuwa umebaki wa kuchanganya mafuta yaliyolipiwa na yasiyolipiwa ambayo ni kidogo. Mamlaka hiyo pia imedhibiti upandishaji holela wa bei ya mafuta kwa waagizaji baada ya kuingiza mfumo wa kuagiza pamoja (BPS) ambapo katika kipindi cha mwaka 2012 na 13, imeokoa zaidi ya Sh bilioni 212.6 ambazo zilikuwa ni gharama za uagizaji.

EWURA KUJITANUA ZAIDI

Katika kuboresha zaidi huduma zake, Ewura pia inajipanua kwa kujenga ofisi katika kanda mbalimbali ikiwemo ya Ziwa, Kaskazini, Mashariki, Nyanda za Juu Kusini na Kati. Ewura pia imeshatoa leseni za biashara ya mafuta 1,561 zikiwemo za jumla 66, rejareja 1,397 na za gesi za kupikia 19 na vituo vya kuuza vilainishi mitaani 59.

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi