loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mkapa- Baba alipenda niwe padre au daktari

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa (81) amesema baba yake mzazi hakuwahi kuota kuwa angekuwa Rais wa Tanzania na hakumuona wakati akiwa kwenye madaraka hayo kwa miaka 10.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuzindua kitabu chenye kurasa 319 kuhusu maisha yake.

“Ningelipendelea uwe mmoja kati ya hawa baadaye utakapomaliza masomo, kwanza uwe padre, ikikushinda hivyo kama haitawezekana natumaini utakuja kuwa daktari, kama hayo mawili hayatawezekana basi angalau uwe mwalimu” amesema mzee Mkapa akinukuu maneno ya baba yake mzazi.

“…kama mnavyojua badala yake nimekuwa Rais wa Tanzania kwa miaka 10 kitu ambacho baba yangu hakuwahi hata kuota na hata hatimae kuona…maisha ya binadamu ni fumbo kubwa sana, pamoja na kuwa tunapozaliwa wazazi hufanya maandalizi mbalimbali ya kuwawezesha watoto wao kumudu maisha yao ya baadaye ni vigumu sana kwa mzazi kujenga tamaa ya mwanawe kuwa kiongozi au Rais wa nchi, kauli ya baba yangu ni kielelezo cha hilo…”amesema.

Amewashukuru Rais Mstaafu Olusegun Obasanjo wa Nigeria na Rais Mstaafu Joachim Chisano wa Msumbiji kwa kumshauri na kumhimiza aandike kitabu hicho chenye sura 16.

Amesema haikuwa kazi rahisi kuandika kitabu hicho baada ya Taasisi ya Uongozi kumshawishi kwa kuwa hakuwahi kufikiria kuwa kuna mengi ya kujifunza kupitia safari ya maisha yake hadi kufikia alipo.

Rais John Magufuli amekizindua kitabu hicho na ameiagiza Taasisi ya Uongozi ione uwezekano wa kukitafsiri kwa lugha ya Kiswahili.

Dk Magufuli amesema, mzee Mkapa alipewa nafasi mbalimbali za uongozi kwa sababu ya juhudi, nidhamu na uadilifu wake vilivyosababisha aaminike.

“Nilicheka kidogo pale nilipogundua kuwa mzee Mkapa kama ilivyokuwa kwangu nae wazazi wake walitaka awe padre upadre ukamshinda na hii ni kwa sababu wanaoitwa ni wengi lakini wanaochaguliwa ni wachache”amesema Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa Magufuli, Rais Mstaafu Mkapa ni mcha Mungu na anamtanguliza Mungu kwenye mambo yake mengi.

"Ni mtu mwenye kujiamini, ana msimamo anayejua mwelekeo anaoutaka, ana upendo wa kweli na sio mnafiki, mtulivu kwa mambo ya kitaifa, mzalendo, mwanafunzi mwadilifu wa sera na falsafa za Baba wa Taifa Mwl Nyerere na pia ni mwanadiplomasia mzuri" amesema.

foto
Mwandishi: Basil Msongo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi