loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mnyama akiwa na njaa, kiu, maumivu unalipa mil 1/-

BUNGE limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 7 wa 2019, ambao utaruhusu watu kujipima Virusi Vya Ukimwi na viongozi wa kitaifa kuwa huru kuchagua pa kuzikwa.

Pia, itakuwa ni kosa mtu asipohakikisha wanyama walio chini ya uangalizi wake, wanaishi bila njaa, kiu, woga, maumivu au majeraha.

Muswada huo umerekebisha sheria 11 ambazo ni Sheria ya Magonjwa Sura ya 156, Sheria ya Ustawi wa Wanyama Sura ya 154, Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania Sura ya 197, Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada Sura ya 134 na Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa VVU na UKIMWI Sura ya 431.

Nyingine ni Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Sura ya 182, Sheria ya Madini Sura ya 123, Sheria ya Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa Sura ya 419, Sheria ya Bandari Sura ya 166, Sheria ya Kuzuia Ugaidi Sura ya 19, Sheria ya Usajili na Utambuzi wa Watu Sura ya 36.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi alisema lengo la marekebisho hayo ni kurahisisha utekelezaji wa sheria hizo kwa kuondoa upungufu, uliojitokeza wakati wa kutumia masharti ya sheria hizo na pia kuoanisha masharti ya sheria zinazorekebishwa na masharti yaliyoko katika sheria nyingine zilizopo.

Alisema katika Sheria ya Magonjwa ya Wanyama, inapendekezwa kurekebishwa kwa madhumuni ya kuhuisha upya adhabu na makosa mbalimbali.

Aidha, kinaongezwa kifungu ili kuweka mfumo wa kufililisha makosa, jambo ambalo litaepusha mchakato mrefu wa mashtaka na hivyo kuokoa gharama na muda na kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani kwa makosa madogo ambayo yanaweza kufililishwa.

Katika Sheria ya Ustawi wa Wanyama, imerekebishwa kwa lengo la kuongeza idadi ya vitendo ambavyo ni makosa chini ya sheria hiyo ili kujumuisha vitendo ambavyo ni kinyume na haki za wanyama zinazotambulika kimataifa.

“Kwa mujibu wa marekebisho haya, itakuwa ni kosa mtu asipohakikisha kuwa wanyama walio chini ya uangalizi wake wanaishi bila njaa, kiu, woga, maumivu au majeraha,” ilieleza sehemu ya muswada huo.

Kwa mujibu wa marekebisho hayo itakuwa ni kosa kumsababisha mnyama njaa, kutompa chakula cha kutosha au kumnyima chakula au maji.

Adhabu iliyopendekezwa ni Sh 100,000 hadi Sh milioni moja, kiwango ambacho Kambi ya Upinzani ilisema ni kikubwa na kupendekeza kiwe kati ya Sh 50,000 hadi 500,000.

Katika Sheria ya Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa, endapo marekebisho hayo yatapata baraka za Rais John Magufuli, yatawawezesha viongozi au familia zao kuwa huru, kuchagua mahali pa kuzikwa kwa kuheshimu tamaduni, mila na dini zao.

Aidha, yataondoa masharti yanayohusu uanzishwaji wa Makaburi ya Kitaifa na usimamizi wake. “Lengo ni kuboresha ushirikiano kwa pamoja katika maandalizi na taratibu za mazishi ya viongozi wa kitaifa,” yamebainisha marekebisho hayo.

“Lengo la marekebisho haya ni kuruhusu kiongozi wa kitaifa kuzikwa katika eneo ambalo familia yake itaamua azikwe au kwa kuzingatia wosia wake,” imefafanuliwa.

Katika Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa VVU na UKIMWI, sasa sheria imejumuisha masharti ya kujipima VVU, kwa kuainisha wajibu kwa mtu anayejipima VVU na mtu anayetoa au kusambaza vifaa vya kujipima VVU.

Aidha, marekebisho hayo yameweka bayana umri wa mtoto katika masuala ya upimaji wa Virusi Vya UKIMWI (VVU) na kueleza maana ya dhana ya kujipima VVU.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtoto mwenye umri wa miaka 15 ataruhusiwa kupimwa VVU, majibu ya vipimo ya mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18 yatatolewa pia kwa mzazi, mlezi au mtu mwingine ambaye mwenye vipimo anamuamini.

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umeanza rasmi ...

foto
Mwandishi: Mgaya Kingoba, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi