loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

DPP aomba kutaifisha nyumba 7

BAADA ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutangaza kumsaka kwa miezi tisa bila ya mafanikio mtuhumiwa wa kesi ya kutakatisha fedha haramu, Magreth Gonzaga, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), amewasilisha maombi Mahakama Kuu ya Tanzania kuomba kutaifi sha mali zake zikiwemo nyumba saba.

Maombi hayo namba 1/2019 yamewasilishwa katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi na yataanza kusikilizwa Novemba 26, mwaka huu mbele ya Jaji Sirilius Matupa.

Maombi hayo yamewasilishwa chini ya kifungu namba 4(1) (c), 9 (1) na 14(1) na (2) cha mwenendo wa mashauri ya jinai namba 256 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002. DPP anaomba kutaifisha nyumba namba 199 iliyopo kitalu namba D yenye hati namba 121302 iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam na nyumba namba 200 iliyopo kitalu D yenye hati namba 39021 iliyopo Tegeta.

Pia anaomba kutaifisha nyumba namba 1378, Block E Tegeta ikiwa namba za hati 41275 na nyumba namba 176 Block B iliyopo Aman Gomvu ikiwa na hati namba 138598. Nyingine ni nyumba namba 191, Block B iliyopo Aman Gomvu ikiwa na hati namba namba 132797 na nyumba namba 174 Block B iliyopo Aman Gomvu ikiwa na hati namba 138597.

Machi 26, mwaka huu Takukuru ilitangaza kumsaka Margreth ikidai anamiliki nyumba tatu za kifahari jijini Dar es Salaam, huku akidaiwa kutakatisha fedha haramu kinyume cha kifungu namba 12(d) na 13(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha Haramu namba 12 ya Mwaka 2006.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati huo, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Diwani Athumani, alisema wanamsaka Margreth kupitia tangazo lililotolewa kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayosikiliza shauri la jinai namba 28 la mwaka 2019.

Alisema Margreth amekimbilia nje ya nchi hivyo anatafutwa na Takukuru kwa tuhuma za kutakatisha fedha haramu na kujipatia mali kupitia kampuni ya Superior Financing Solution Limited (SFS) inayodaiwa kufanya biashara bila kulipa kodi ya serikali.

Alisema kutokana na mtuhumiwa huyo kutoroka wakati uchunguzi unaendelea, Takukuru inapaswa kutangaza kutafutwa kwake kabla ya kutaifisha mali alizojipatia kwa njia ya rushwa.

Hata hivyo, mume wa Margreth, Aloycious Gonzaga na mwenzake Isaack Kasanga bado wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 5/2019 katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ambayo iko katika hatua ya usikilizwaji. Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 45, ikiwamo moja la kula njama kutenda kosa, kughushi 12, kuwasilisha nyaraka za uongo tisa, kushindwa kulipa kodi na utakatishaji fedha mashitaka 30.

IKIWA fomu moja ya kuomba ridhaa ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi