loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wizara yamtaka mfanyabiashara ateme bil 4.5/-

WIZARA ya Kilimo imemtaka mfanyabiashara anayemiliki Kampuni ya Bajuta kurejesha Sh bilioni 4.5 za kuagiza viuatilifu aina ya sulphur, huku ikionya mtumishi wake atakayefanya ubadhirifu hatavumiliwa.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema hayo akijibu swali la Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM) aliyehoji kukwama bandarini sulphur iliyoagizwa kwa ajili ya wakulima wa korosho.

“Kuna mfanyabiashara tumemuamuru kurejesha shilingi bilioni 4.5 kutokana na kukwama kwa dawa hiyo...mfanyabiashara huyo wa Bajuta arejeshe fedha hizo mara moja. Na pia katika hatua nyingine tumemsimamisha mtendaji wa TFC,” alisema Bashe.

Aliongeza kuwa mbali ya hatua hizo, pia wanazungumza na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) pamoja na Kampuni ya Azam ili kuzitoa dawa hizo bila gharama na pia kupunguziwa gharama za utunzaji, ili zisiharibike na ziende kwa wakulima kwa ajili ya msimu unaoanza.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Rungwe, Saul Amon (CCM) alihoji serikali ina mpango gani kuanzisha vitalu vya maparachichi ili wananchi wapate miche kwa bei nafuu kwani bei ya sasa ya Sh 3,000 tatu kwa mche kwa mkulima wa kawaida ni ghali. Pia alihoji serikali ina mpango gani wa kusambaza wataalamu wa kilimo katika Jimbo la Rungwe.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Bashe alisema kilimo cha parachichi ni muhimu katika kuongeza kipato na lishe kwa wakulima na jamii na kuliingizia Taifa fedha za kigeni kutokana na mauzo nje ya nchi. Kutokana umuhimu huo, alisema serikali imekuwa ikihamasisha wakulima na wadau wengine kuongeza uzalishaji wa zao la parachichi hususan aina ya HASS ambayo imekuwa na soko la uhakika.

“Serikali pia inaainisha maeneo yote yanayofaa kwa kilimo cha parachichi nchini kuongeza uzalishaji wa miche ya miparachichi aina ya HASS na kuilinda ili isiharibiwe na aina nyingine za miparachichi kupitia “cross breeding,” alisema Bashe.

Alieleza kutokana uhamasishaji wa serikali, wadau mbalimbali wakiwemo wakulima na makampuni binafsi wameanza kuzalisha miche bora ya parachichi ambapo jumla ya vitalu 233 vikiwemo vitalu 230 vya wakulima wadogo wadogo na vitalu vitatu vya kampuni binafsi vimeanzishwa wilayani Rungwe. Aidha, vitalu hivyo vimezalisha miche 345,473 ambapo miche 265,473 imezalishwa na wakulima wadogo na miche 80,000 imezalishwa na kampuni binafsi.

“Katika kuhakikisha upatikanaji wa miche bora ya miparachichi, mkakati wa serikali ni kukiboresha Kituo cha utafiti cha Uyole na Kituo cha Utafiti Horti Tengeru ili kuwa vituo mahiri katika uzalishaji wa miche bora ya miparachichi aina ya HASS nchini,” alisema.

CHAMA cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimekubaliwa ...

foto
Mwandishi: Mgaya Kingoba, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi