loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Nilikuwa nachoka, kukosa nguvu kumbe tatizo la moyo’

“NILIKUWA kila nikienda shuleni mwili unachoka sana, nakosa nguvu na kichwa kuniuma hadi nashindwa kuendelea kusoma na kusababisha walimu kunirudisha nyumbani ili niweze kupata huduma za matibabu. Wakati mwingine, walimu walikuwa wakimpigia mama yangu simu aje anichukue kutokana na kushindwa kuendelea na majukumu yangu vyema.”

Ndivyo anavyoanza kusimulia mkasa wake mvulana mdogo mwenye umri wa miaka 14, Eric Zacharia ambaye anaendelea na matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) baada ya kubainika kuwa tatizo lililomsumbua tangu utoto wake ni ugonjwa wa moyo.

Eric, mkazi Arusha ambaye alifaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka huu, amelazimika kusitisha masomo kutokana na kuhudhuria matibabu katika taasisi hiyo na sasa anasema anaendelea vizuri. Mtoto huyu ambaye kwa kipindi kirefu hakujulikana alikuwa akisumbuliwa na matatizo gani alikuwa akitoa maelezo ya maisha yake mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye ameahidi kusaidia matibabu ya moyo kwa watoto 92 akiwemo yeye Eric.

Ni kutokana na hatua hiyo ya Mkuu wa Mkoa Eric anasema mchango wa kiongozi huyo utakuwa msaada mkubwa kwake na kwa familia nyingi ambazo zimekuwa hazina uwezo wa kujitibu kutokana na gharama kubwa. Akisimulia hali ilivyokuwa, Eric nasema kila alipokuwa akienda shule, kwa kuwa kuna umbali kidogo na shule yao iko milimani alikuwa akikosa nguvu na kujikuta akikaa chini kupumzika.

“Wanapopita wanafunzi wenzangu wananikokota au kunibeba hadi shuleni ingawa kuna waliokuwa wanadhani ninajifanya. Wakati mwingine wazazi wangu walikuwa wanapigiwa simu kwenda kunichukua, hali inapokuwa mbaya kwa kushindwa kutembea,” anasema.

Anasema mara nyingi alipokuwa akifikwa na hali hiyo na kurudi nyumbani, wazazi walikuwa wakimpeleka katika vituo mbalimbali vya afya, lakini tatizo la moyo halikujulikana bali alikuwa akiambiwa kwamba ‘anasumbuliwa na tatizo la kifua’ na hivyo kupewa dawa za kifua hususani za kikohozi! Anasema baadaye madaktari walimshauri mama yake, kuchukua vipimo zaidi, ambapo kwa hatua ya awali alijichangisha na ndugu ili kupata fedha zitakazowezesha kupata vipimo kama cha kuangalia mamna moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph - ECHO).

Eliza Zacharia ambaye ni mama yake Eric anasema mtoto huyo alipofikishwa katika taasisi ya JKCI alipimwa na kubainika kuwa ana matundu mawili katika moyo. Anasema kabla ya msaada wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alishaanza kuona itakuwa vigumu kwa mwanae kutibiwa kutokanana gharama.

“Eric kwa kipindi chote alikua akilalamika mwili kukosa nguvu, kuchoka na hata kichwa kumuuma sana, lakini hakuna aliyewaza haraka kuwa inaweza kuwa ni matatizo ya moyo,” anasema Elizabeth na kuwaasa wazazi wengine na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanachukua vipimo vya uhakika pale watoto wao wanapolalamikia mtatizo ya kiafya.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi, anasema kati ya watoto 100 wanaozaliwa nchini mmoja ana tatizo la moyo. Anasema takwimu alizonazo zinaonesha kwamba watoto milioni mbili waliozaliwa Tanzania kwa mwaka jana 2018, watoto takribani 13,000 miongoni mwao wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ya moyo na wanahitaji upasuaji.

Anasema katika mwaka huu 2019 ambao haujaisha, JKCI iliweka lengo la kuwafikia watoto na watu wazima 400 kwa ajili ya upasuaji wa moyo lengo ambalo wameshalimevuka .

“Hadi sasa orodha ya wanaosubiri upasuaji ni 512 na taasisi hii inaamini kuwa wote watapatiwa matibabu kabla ya mwaka huu kuisha,” anasema Profesa Janabi.

Janabi anamshukuru Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kusaidia gharama za matibabu kwa watoto ambapo amekuwa akileta wadau mbalimbali wakiwemo wasanii wa muziki kwa ajili ya kuchangia gharama za matibabu. Watoto 40 katika ya 60 ambao Makonda aliahidi kulipia gharama zao kwa mara ya kwanza kabla ya kuongeza wengine 32 wameshafanyiwa upasuaji na wengi wao wamerudi majumbani kuendelea na majukumu mengine, waliobakia wodini ni wachache wakiendelea na mazoezi.

Makonda anasema amekuwa akitafuta wadau mbalimbali kusaidiana nao katika kutibu hao watoto hao ili watoke salama ikiwa ni moja ya njia ya kurudisha faraja kwa familia wakiwemo akina mama ambao wanalazimika kucha shughuli na kukaa wodini na watoto wao.

Jitihada za kusaidia watoto hao kupata matibabu, zimemwezesha Makonda kupata michango kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo Kampuni ya wasafi, ambapo jumla ya watoto 32 wameongezeka katika idadi ya ahadi yake ya awali na hivyo kufiki watoto 92 wataofanyiwa upasuaji kwa gharama hizo za wadau. Makonda pia ameunda kamati ya kuchangia huduma za afya, ikisimamiwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei na tayari kampuni 100 zimeorodheshwa ili kuweza kuchangia matibabu.

“Kampuni zote zitakapopata barua kutoka katika ofisi yangu naomba wasisite kuchangia, hiki ni kipindi cha kutoa shukrani kwa Mungu na sadaka kwa kuwasaidia walio wahitaji,” anasema Makonda.

Anasisitiza kwamba kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa mwaka ni wakati mwafaka wa kushukuru kwa mengi mema ambayo Mungu amekuwa akiwatendea binadamu. Makonda kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo kampuni ya Wasafi wamechangia shilingi milioni 80 kwa ajili ya kusaidia huduma za matibabu ya moyo kwa watoto.

Mwanamuziki, Nassib Abdul maarufu kama Diamond ameahidi kusaidia watoto 10 huku wasanii wengine wakichangia kwa viwango tofautitofauti. Diamond anatoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kwa ajili ya kuchangia huduma za matibabu ya moyo kwa watoto ili kuwanusuru na madhila ya kiafya wanayopitia na kuwawezesha wazazi wao, hususani akina mama kurejea katika shughuli zao mbalimbali.

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi