loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Miaka minne ya JPM ilivyonogesha TTCL

BILA kuandikia mate, ‘ukirudi leo nyumbani TTCL (Shirika la Mawasiliano Tanzania) utagundua kwamba kumenoga kwelikweli!’ Ukiacha maofisi kadhaa, miaka minne iliyopita ni Watanzania wachache waliokuwa wanafikiria kupata huduma ya mawasiliano hususani ya simu za mkononi kupitia shirika hilo kongwe.

Lakini hali imebadilika sana kwani huduma karibu zote zinazotolewa na kampuni zingine za binafsi za mawasiliano zinatolewa kwa uhakika na kwa bei nzuri na shirika hili la mawasiliano la umma.

Unapoingia katika jengo la makao makuu ya TTCL utagundua pia mabadiliko makubwa ya kimwonekano ambayo hayakuwepo miaka minne iliyopita. Kwa sasa kuna mpaka makumbusho ya kisasa ya vifaa vya mawasiliano ndani ya jengo hilo.

Mwonekano wa kuvutia ndio pia utauona katika majengo ya takribani ofisi zote za shirika hili ambalo lipo kila mkoa na karibu kila wilaya kama si kata na kijiji. Meneja Uhusiano wa TTCL, Puyo Nzalayaimisi, anasema mafanikio ya shirika unaweza kuyaona katika kuongezeka kwa idadi ya wateja ambayo ni ishara tosha kwamba shirika liko vizuri kulinganisha na hali ilivyokuwa mwaka 2015.

“Mimi nayaona mafanikio kwa mtazamo wa huduma tunazotoa, kwa maana ya kwamba idadi ya watumiaji wa huduma zetu inapoongezeka ni ishara tosha kwamba tumefanikiwa… Tumeweza kuongeza idadi ya wateja kwa zaidi ya asilimia 200 kwa kipindi cha miaka minne,” anasema.

Katika kipindi hicho anasema huduma za simu za mkononi katika shirika hilo zimeongezeka kutoka 339,840 Desemba 2015 hadi kufikia 1,283,249 Septemba 2019 sawa na ongezeko la asilimia 278. Kwa upande wa watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu za mezani anasema idadi ya watumiaji iliongezeka kutoka 157,576 Desemba 2015 hadi watumiaji 223,787 Septemba 2019, sawa na ongezeko la asilimia 42.

Nzalayaimisi anasema ujio wa Rais John Magufuli madarakani ndio hasa msingi wa mafanikio wa TTCL sambamba na uteuzi mzuri uliofanyika kwa kumpata mtendaji mchapa kazi, Waziri Kindamba.

Baadhi ya wafanyakazi wa TTCL waliozungumza na mwandishi wa makala haya wanasema Kindamba, alisaidia sana kuwafanya wafanyakazi wa shirika hilo ambao walikuwa wamekata tamaa kupata ari mpya ya kufanya kazi.

“Ukweli ni kwamba moja mafanikio makubwa ya shirika kwa upande wa sisi wafanyakazi ni kupatikana kwa ajira za kudumu kwa sababu mwanzo watu walikuwa na ajira za mikataba... Mtu unakaa unajiuliza siku yako ya kuondoka ni lini lakini kwa sasa mtu unajua una uhakika na ajira na haki zako,” asema mmoja wa wafanyakazi wa Shirika hilo.

Nzalayaimisi anasema agizola Rais Magufuli la kuwataka viongozi wa serikali na taasisi za umma kupenda kutumia laini za TTCL nalo limechagiza ongezeko la watumiaji wa mawasiliano ya simu za mkononi ya TTCL.

Anasema bahati nzuri wote wanaojiunga na TTCL hawajajuta kwa uamuzi huo kwani wanapata huduma bora na kwa bei nzuri ya ushindani. Mohammed Makalla, muuzaji wa laini za TTCL mitaani anakiri kwamba wateja wanaonuna laini za simu za TTCL wanaongezeka kwa kiasi kikubwa na wengi wanasifia huduma zinazotolewa na shirika hilo.

“Zamani ulikuwa unaweza ukamaliza siku bila kuuza hata laini moja lakini sasa hivi wanakuja wanajiunga kwa siku unaweza kuuzia wateja watano mpaka wanane laini kwa siku,” anasema Makalla.

TTCL ilianzishwa 1993 ikiondolewa kutoka Kampuni mama ya Posta na Simu Tanzania ili ijitegemee katika kutoa huduma ya mawasiliano ya simu pekee. Ilianza rasmi kazi kama kampuni inayojitegemea Januari 1, 1994 sambamba na kuanzishwa kwa Shirika la Posta Tanzania, Benki ya Posta na Tume ya mawasiliano ambayo kwa sasa inatambulika kama Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

TTCL nayo lilipitia katika ubinafsishwaji wa makampuni ya umma ambapo Februari, 2001 Kampuni za Consortium MSI na Detecon ya Ujerumani zilinunua asilimia 35 ya hisa za kampuni kutoka serikalini.

Miaka 16 baadaye, yaani baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani alianza juhudi za kuipaisha TTCL kama alivyofanya kwa mashirika mengine ya umma likiwemo la ndege (ATCL) kutoka kuwa shirika la wazee na linalochungulia kaburi kuwa shirika bora la mawasiliano ya simu kwa rika zote. Mbali na kumteua Mtendaji Mkuu mpya, Magufuli pia alirudisha hisa zote serikalini ambapo kufikia mwaka 2018 TTCL ikawa inamilikiwa na serikali kwa asilimia 100 ya hisa zote.

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi