loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kitabu cha Mkapa chaadimika ndani ya saa 12

KWA mara ya kwanza ndani ya miaka 30, Kitabu cha Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kiitwacho ‘’My Life, My Purpose, kilichozinduliwa juzi jijini Dar es Salaam na Rais John Magufuli, kimevunja rekodi ya kuhitajika sokoni, ambapo nakala ,1,000 ya vitabu vilivyoletwa nchini kwa ajili ya uzinduzi huo, viliisha ndani ya saa 12.

Kwenye mahojiano maalum jana jijini Dar es Salaam na HabariLeo, Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya Mkuki na Nyota, Mkuki Bgoya ambao ndio wachapishaji wa kitabu hicho, alisema haijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo miaka 30 iliyopita, kwa kitabu kupendwa sokoni kama hicho.

“Hata sisi hatujui nini kimetokea, tumeshangaa ndani ya saa 12 tangu kuzinduliwa kwa kitabu hicho, nakala tulizozileta zaidi ya 1,000 kwa ajili ya tukio la uzinduzi zimeisha sokoni, hatukutegemea, kwa sababu tunachapia nje ya nchi, hivyo tuliona tusafirishe vichache hivyo kwa ndege, na mzigo mkubwa uko majini unakuja kwa meli”,alisema Bgoya.

Alisema haijawahi kutokea, kupata mwitikio mkubwa wa kitabu kama huo. Aliwatoa wasiwasi wananchi na wale wote wanaokihitaji, kuwa kitabu siyo kwamba kimeisha, bali nakala walizozitanguliza nchini, ndizo zimeisha. Alisema ndani ya wiki tatu kuanzia sasa, vitabu hivyo vitapatikana nchi nzima.

“Niwatoe wasiwasi wananchi na wadau wa kusoma vitabu, kitabu cha Mkapa kipo, sio kwamba kimeisha, tulisafirisha nakala chache kwa ndege kwa ajili ya uzinduzi na nakala za kutosha ziko. Mzigo ulishapakiwa kwenye meli, ziko majini, vitaingia mdani ya muda huo na tutasambaza nchi mzima”,alisema Bgoya.

Alisema mwitikio wa watu kukipenda kitabu hicho, umetokana na mwandishi wake ambaye kila mtu anapenda kusoma ameandika nini. Kwamba wengine wanasoma kwa ajili ya kuongeza uelewa wa mambo.

Kwamba hata viongozi wanakitafuta kwa ajili ya kujua masuala mbalimbali, yaliyoainishwa na jinsi ya kukabiliana na changamoto. Bgoya alisema Rais John Magufuli na marais wastaafu waliohudhuria kwenye uzinduzi huo, wameongeza hamu ya wananchi, taasisi, mashirika binafsi, shule na mabalozi, kuwa na hamasa ya kukisoma. Alisema hiyo imeonesha wazi kuwa usomaji wa vitabu kwa wananchi hususan Watanzania unawezekana, iwapo hamasa itatolewa.

Hata hivyo, alisema nakala zilizokuja nchini zimeuzwa Dar es Salaam na chache ziliuzwa Dodoma. Kwamba mikoa mingine hazikuuzwa, kwa sababu zimeisha na kwamba nakala zinazokuja ziko nyingi, zitatosha kusambazwa nchi nzima na pia zitauzwa mtandaoni.

Wakati Bgoya akisema hayo, maduka yote ya vitabu jijini Dar es Salaam yaliyopata nakala za kitabu hicho, yamemaliza kuuza na bado mahitaji ni makubwa. Watu wengi hivi sasa wanahaha kukipata, hata kwa bei ya juu. Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa jana kwenye maduka makubwa na maarufu ya kuuza vitabu jijini Dar es Salaam, ulibaini yalikuwa yamemaliza nakala walizopata tangu juzi. Akizungumza na gazeti hili, mwananchi aliyekuwa akizunguka kutafuta kitabu hicho, Joseph Mwakipesile alisema amezunguza maduka makubwa yote ya katikati ya jiji, hajakipata na ameenda duka moja eneo la Slipway, nako kimeisha.

“Nimezunguka vya kutosha nimeambiwa vimeisha, sasa nasubiri baada ya wiki tatu nimeambiwa vitakuwa vifika”,alisema Mwakipesile.

Baadhi ya maduka hayo ni pamoja na Novel Idea Bookshop, Book Mart, Dar es Salaam Bookshop, TPH bookshop, MAK Books and Brains, Elite Bookstore na mengineyo. Katika kitabu hicho, Mkapa amezungumzia mambo mengi yaliyotokea katika maisha yake, kuanzia udogo wake, familia, elimu, urais, baada ya kumaliza muda wake madarakani na jinsi anavyotumika kutatua migogoro nje ya nchi.

Katika kitabu hicho, watu mashuhuri duniani wametoa maoni yao na kuwataka watu kukisoma na baadhi yao ni aliyekuwa Rais wa Botswana, Festus Mogae ambaye alisema kitabu hicho ni moja ya vitabu muhimu vinavyopaswa kusomwa, kwani Mkapa ameeleza utendaji kazi wake kwa serikali ya Tanzania, huku akitaja mafanikio, changamoto na ushauri kwa viongozi wa sasa na wajao.

Rais mstaafu wa Finland, Martti Ahtisaari ni miongoni mwa viongozi waliotoa maoni yao kwenye kitabu hicho na kushauri watu wakisome, kwani Mkapa ameelezea kwa undani jinsi ya kufanya kazi na kutatua changamoto zilizopo, sambamba kuelezea mtazamo wake na ushauri kwa viongozi wa baadaye.

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umeanza rasmi ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi