loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Jafo ataka Tarura iongezewe fedha za ujenzi wa barabara

WATAALAMU wa Mfuko wa Barabara wametakiwa kuangalia namna ya kurekebisha kanuni ya mgawo wa fedha za barabara, ili kuongeza mgawo wa fedha kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) kutoka asilimia 30 za sasa hadi asilimia 40.

Kwa mujibu wa kanuni za mgawo wa fedha za barabara zilizopo kwa sasa, asilimia 30 ya fedha hizo inaelekezwa Tarura, wakati Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ukipewa asilimia 70. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, (pichani) alitoa rai hiyo jijini hapa juzi wakati wa kukabidhi magari 22 kwa Tarura.

Alisema Tarura kuongezewa kiwango cha fedha za ujenzi wa barabara kutaongeza ufanisi katika utendaji kazi wa wakala huo na kuboresha barabara za mijini na vijijini ambazo nyingi zina changamoto na ndiko wazalishaji wa mazao waliko.

“Road Fund (Mfuko wa Barabara) mnafanya kazi nzuri, ila wataalamu nendeni mkaangalie ile kanuni, haiwezekani Tarura iliyokuwa ikihudumia mtandao wa barabara wa kilomita 108,000 na sasa inahudumia kilomita 135,000 bado tukaendelea na kanuni ile ile ya asilimia 30 kwa asilimia 70,” alisema.

Aidha, Jafo ameutaka Mfuko wa Barabara kutumia fedha za dharura kuimarisha barabara kabla ya mvua za masika hazijaanza na kurekebisha haraka maeneo ambayo yameharibiwa na mvua za vuli.

“Maeneo mengi nimeona hata kwa RC (mkuu wa mkoa) na DC (mkuu wa wilaya) unakuta gari linapelekwa hata miaka haijafika unaambiwa limekufa, tena utaambiwa lime ‘nock’ injini, hii ina maana halikupata ‘service’ inavyotakiwa, kwa hiyo madereva mnaopewa magari haya hakikisheni mnayatunza.”

“Isitokee meneja yeyote wa Tarura akalazimisha gari litembee wakati limeshapitisha muda wa kufanya ‘service’, dereva unatakiwa kukataa hali hiyo na liegeshe kwa sababu gari likiharibika wewe utakuwa wa kwanza kubeba lawama,” alisema.

Jafo pia alikemea tabia ya baadhi ya viongozi kunyanyasa madereva wao kwa kuhodhi fedha zilizotengwa kwa ajili ya mafuta na matengenezo.

“Siipendi tabia ya kunyanyasa madereva, kuna mabosi fedha ya mafuta na matengenezo anakaa nazo yeye, hajui gari inaoshwaje na mwishowe dereva ndio anawajibika kufanya marejesho, hii ni aibu, wakati mwingine dereva anapata ajali kwa sababu mmemsababishia msongo wa mawazo,” alisema.

Naye Mtendaji Mkuu wa Tarura, Victor Seff, alisema magari hayo yamenunuliwa na serikali kupitia Mfuko wa Barabara, ikiwa ni katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa magari ya usimamizi.

“Magari haya 22 ni ya awamu ya pili katika mkakati wa mwaka wa fedha uliopita, awamu ya kwanza tulinunua magari 26 na yalishakabidhiwa, hivyo kufanya hadi sasa Tarura kuwa na magari 48 kwa gharama ya Sh bilioni 4.3,” alisema.

Alisema mwaka huu wa fedha wamepanga kununua magari 19 kwa ufadhili wa Mfuko wa Barabara, hali itakayofanya sasa kuwa na upungufu wa magari 337 kwa nchi nzima.

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umeanza rasmi ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi