loader
Picha

Majaliwa: Wauzieni mbolea wakulima kwa bei elekezi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka mamlaka husika, kuhakikisha wakulima wanauziwa mbolea kwa bei elekezi iliyowekwa na serikali. Majaliwa alitoa maelekezo hayo jijini hapa wakati wa kuahirisha Mkutano wa 17 wa Bunge.

Bunge limeahirishwa hadi Januari 28 mwaka 2020. Alisema serikali imetoa bei elekezi kwa mbolea aina ya DAP na UREA, ambazo ziko katika Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja.

“Mamlaka husika hakikisheni bei elekezi za mbolea zinafahamika kwa wakulima wote katika maeneo yote na wauzaji wanauza kwa kuzingatia bei hizo kama ilivyoelekezwa na Serikali.”

Alisema makisio ya mahitaji ya mbolea kwa msimu wa 2019/2020 ni tani 586,604 na hadi kufikia Oktoba 31 mwaka huu, upatikanaji wake umefikia tani 328,709 ambapo tayari tani 136,457 zimenunuliwa na wakulima kote nchini. Aidha, Majaliwa alisema Serikali inaimarisha mifumo ya masoko ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji na kuimarisha viwanda vya ndani hususan vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

“Hatua hizi zitasaidia kuongeza thamani ya mazao na hivyo kuimarisha bei. Kwa sasa, tunaendelea na msimu wa mauzo wa zao la korosho, baada ya mazao ya pamba na kahawa kumaliza mauzo. Minada ya korosho inaendelea vizuri. Viongozi wa mikoa na wilaya wasimamie malipo kwa wakulima na kuhakikisha kwamba wanalipwa kwa wakati hususan utaratibu wa kulipa ndani ya siku 7 baada ya siku nne za mnada” alisema.

Majaliwa alisema kuelekea msimu wa kilimo wa 2019/2020, hali ya upatikanaji wa chakula nchini imeendelea kuimarika kutokana na uzalishaji mzuri wa mazao ya chakula kwa msimu 2018/2019. Kwa msimu wa kilimo 2018/2019 uzalishaji ulifikia tani milioni 16.41, ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.84. Uzalishaji huo umeiwezesha nchi kujitosheleza kwenye mahitaji yake ya chakula kwa asilimia 119.

“ Pamoja na uzalishaji huo mzuri, kumekuwepo na mahitaji makubwa ya nafaka katika baadhi ya maeneo kutokana na hali ya mvua kutokuwa nzuri na hivyo kuwepo kwa dalili za bei za nafaka kupanda kwenye maeneo hayo. Serikali imetoa maelekezo kwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa kuhakikisha inasambaza nafaka kwenye maeneo yenye upungufu ili kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei,”alisema Majaliwa.

Majaliwa aliwasisitiza maofisa masuhuli kuzingatia maeneo ya kipaumbele, yaliyoainishwa katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na kuhakikisha Kamati za Mipango na Bajeti katika mafungu yao, zinatekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Serikali nayo kwa upande wake itaandaa mipango ya kisekta, kitaasisi na kimaeneo ambayo utekelezaji wake utachochea ujenzi wa uchumi wa viwanda, mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu. Majaliwa pia aliwataka maofisa masuuli kuzingatia udhibiti wa matumizi na kuhakikisha wanatumia Mfumo wa kielektroniki wa Ununuzi wa Umma. “Hivyo, kila taasisi nunuzi ihakikishe inatumia mfumo huo kabla ya Desemba 31 mwaka huu” alisema.

Aidha, aliwataka watumishi wa serikali kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo ili kuiwezesha nchi yetu kufikia malengo ya kujenga uchumi imara, unaojitegemea na wenye kuweza kuhimili ushindani. Alisema Serikali itaendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta zinazogusa wananchi moja kwa moja na kuhakikisha kuwa matunda ya kukua kwa uchumi, yanawafikia Watanzania wote popote walipo. Alisema serikali ya Rais John Magufuli, imepata mafaniko katika nyanja ya miundombinu ya usafiri, miundombinu ya nishati, miundombinu ya elimu.

“Kwa kufanya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu. Katika kipindi cha Januari hadi Juni 2019, kwa shule za msingi, Serikali imejenga madarasa 473, matundu ya vyoo 1,405, nyumba za walimu 24 na kukamilisha maboma ya madarasa 2,760. Kwa shule za sekondari, Serikali ilijenga madarasa 465, matundu ya vyoo 736, nyumba za walimu 23 na kukamilisha maboma ya madarasa 2,392 , pia inaendelea kusomesha kwa wingi katika fani na ujuzi adimu na maalumu na Uanzishwaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi,”alisema Majaliwa.

Alisema kwa upande wa miundombinu ya afya, serikali imejenga vituo vya afya zaidi ya 352, hospitali mpya za wilaya 67 na hospitali za mikoa 7 na za kanda 3 na kuanza maandalizi ya ujenzi wa hospitali tatu za Uhuru (Dodoma), Tunduma (Songwe) na Ubungo (Dar es Salaam).

SERIKALI imetoa ripoti ya uchunguzi wa Maabara ya Taifa ya ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi